Makamu wa Rais,Dk Mohamed Bilal akizindua rasimu ya katiba mpya |
Dar es Salaam/Moshi. Chadema kimepinga
kauli ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kuhusu
hatima ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 kikisema mchakato wa sasa wa Mabaraza ya
Katiba, usiwe kikwazo cha mjadala wa muundo wa Serikali Tatu.
Mkurugenzi
wa Mawasiliano wa Chadema, John Mnyika alisema Dar es Salaam jana kuwa hatima
ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 utakaotokana na mchakato wa mabadiliko ya Katiba
unaoendelea, siyo suala la kusubiri.
Akizungumza
na mwandishi wetu juzi kuhusu kauli ya Waziri wa Katiba na Sheria Mathias
Chikawe kwamba endapo mapendekezo ya Serikali Tatu yatapitishwa, kuna hatihati
ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 kufanyika, Jaji Warioba alisema: “Tuachieni muda… hayo
mengine ni hisia tu. Ni kweli tunayajua lakini acheni tumalize hili kwanza (la
Mabaraza ya Katiba). Hii ndiyo hatua tuliyopo sasa.”
Lakini
jana Mnyika alisema: “Hatuwezi kusubiri hadi Mabaraza ya Katiba yakamilishe
mchakato kama alivyoeleza Jaji Warioba katika gazeti lenu la Mwananchi toleo la
leo, (jana),” alisema Mnyika kwa simu.
Jaji
Warioba alitaka suala la muundo wa Serikali Tatu utakavyokuwa lisiwe hoja kwa
sasa kwa kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba inachokifanya ni kukusanya maoni
kupitia Mabaraza ya Katiba na kisha kuandaa rasimu itakayopelekwa bungeni kwa
ajili ya majadiliano na kwamba mjadala huo utawachanganya wananchi endapo
utaingizwa katika hatua hii ya ukusanyaji maoni.
Lakini
Mnyika alisema: “Mijadala hii haiwezi kusubiri mpaka hatua ya Mabaraza ya
Katiba, inapaswa kuanza wakati huu kupitia mabaraza yanayosimamiwa na Tume na
Mabaraza yanayoendeshwa na makundi ya kijamii. “Pia, masuala hayo ya mpito
pamoja na marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ni mambo ambayo
yanapaswa kutolewa ufafanuzi wa ziada na Serikali zaidi ya kauli ambayo
Waziri wa Sheria na Katiba Mathias Chikawe ameitoa kupitia gazeti la lenu la
leo (jana).”
Alisema
kimsingi bado kunahitajika mjadala wa masuala ya mpito kwa sababu kuna
uwezekano kwamba Katiba Mpya, ya Muungano au ya Zanzibar na ya Tanganyika,
isiwe tayari kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, endapo suala la Serikali tatu
litapita.
Alisema
kwa upande mwingine, rasimu ya Katiba iliyotolewa imeibua mjadala juu ya mkwamo
wa kikatiba (constitutional stalemate), ambao ni muhimu upatiwe suluhisho
akisema chama chake kinapendekeza mchakato wa Katiba Mpya ya Tanganyika uanze
mara moja ili uende sambamba na huu wa Katiba Mpya ya Muungano. Alisema ilikuwa
vyema yote yakajadiliwa katika Bunge la Agosti 27, mwaka huu.
Waziri
Chikawe alikaririwa na gazeti hili juzi akisema: “Uwepo wa Serikali tatu
utafumua mfumo mzima wa utendaji ndani ya Serikali. Hatuwezi tena kufanya
uchaguzi wa Rais na wabunge 2015, hatuwezi kufanya chochote nje ya Katiba ya
Serikali Tatu kwa kuwa kinachofuata ni kuunda Katiba nyingine inayohusiana na
Serikali tatu.
Juzi,
Waziri Chikawe alitoa ufafanuzi juu ya utata wa hoja zake kwa kuipongeza Tume
ya Jaji Warioba kwa kazi inayofanya huku akisema anaunga mkono msimamo wa CCM
wa kutaka kuendelea na muundo wa Muungano wa Serikali mbili.
Alisema
mchakato wa kuandika Katiba Mpya unapaswa kuangaliwa kwa jicho pana zaidi ya
lile la Uchaguzi Mkuu wa 2015.
“Kuna
mambo mawili hapa. Mosi ni msimamo wa chama changu cha Mapinduzi (CCM) kuhusu
Rasimu ya Katiba na pili msimamo wa Serikali ambayo mimi ni Waziri tena mwenye
dhamana ya Katiba,” alisema na kuongeza:
“Msimamo
wa CCM ni Serikali mbili na wanachama wote nikiwamo mimi tunajua hivyo. Lakini
kuna suala la Serikali ambayo ndiyo iliyoamua kuunda Tume ya Mabadiliko ya
Katiba. Kwa kadri ya uelewa wangu, Serikali haijatoa msimamo na inaunga mkono
kazi inayofanywa na Tume.”
Alisema
mambo hayo mawili hayapaswi kuchanganywa na kuwa kila chombo (CCM na Serikali)
kinaweza kutoa kauli au msimamo kadri kinavyoona inafaa.
Licha
ya kusema kwamba jukumu la kisheria la kuandaa Uchaguzi Mkuu ni la Tume ya
Taifa ya Uchaguzi, alisisitiza kuwa ili ufanyike mwaka 2015 chini ya muundo wa
Serikali Tatu unaopendekezwa na Tume ya Warioba, basi itabidi yafanyike
mabadiliko makubwa ya sheria mbalimbali kazi ambayo haiwezi kufanywa kwa
kukurupuka.
Hata
hivyo, alisema maoni yake hayana maana kuwa Uchaguzi Mkuu hauwezi kufanyika
mwaka 2015, bali yanalenga kuonyesha kazi kubwa iliyopo mbele.
Butiku
Mjumbe
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Joseph Butiku amesema baadhi ya viongozi wakuu
serikalini hawataki tume itoe ufafanuzi kuhusu mapendekezo ya muundo wa
Serikali tatu kwa kuwa unagusa vyeo vyao.
Aidha,
amesema hakuna haja ya kuwa na hofu kwani tayari Zanzibar imekwishaanza
kujitegemea ikiwa na bendera yake, wimbo wake wa taifa na sasa inaidai Serikali
yake kamili.
Butiku
alitoa kauli hiyo juzi wakati wa kikao cha Baraza la Katiba la Wilaya ya Moshi
Vijijini, ambacho kilitawaliwa na mvutano mkubwa miongoni mwa wajumbe kuhusu
suala la kuwapo kwa Serikali tatu, huku wajumbe ambao ni madiwani, viongozi na
wafuasi wa CCM wakitaka Serikali mbili.
Alisema
kwa hali ilivyo sasa, tayari Zanzibar ina Serikali yake yenye mihimili yote ya
dola na tume ilichokipendekeza ni kuiondoa Serikali ya Tanzania Bara kwenye
‘tumbo’ la Muungano.
Butiku
alisema sababu hasa ya Zanzibar kutaka kuwa na nchi yao ni hofu ya kumezwa na
Tanzania Bara katika Muungano wa Serikali mbili na hofu hiyo bado haijakwisha
na inazidi kukua.
Butiku
aliyataja mambo ambayo Zanzibar iliyafanya kwa baraka za marais wa wakati huo
licha ya kwenda kinyume cha Katiba kuwa ni pamoja na kuwa na bendera yao pamoja
na wimbo wa taifa.
Alisema
Baba wa Taifa, hayati Julius Nyerere alifariki akiwa na imani kuwa Serikali
tatu zitavunja Muungano na alifanya hivyo kwa sababu alitaka kuwapo kwa nchi
moja.
Butiku
alisema hata Mwalimu Nyerere katika kitabu chake alichoandika baada ya Kundi la
Wabunge la G55 kutaka Serikali ya Tanganyika, alizungumzia kuwa na Serikali
moja au Shirikisho.
No comments:
Post a Comment