To Chat with me click here

Monday, July 22, 2013

MIILI YA WANAJESHI WALIOUAWA DARFUR KUAGWA LEO




Miili ya askari saba wa Jeshi la  Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliouawa kwa kupigwa risasi katika Jimbo la Darfur, nchini Sudan, wakiwa kwenye operesheni za Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa (Unamid), itaagwa leo katika viwanja vya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), vilivyoko Upanga, jijini Dar es Salaam.

Miili hiyo ya Sajini Shaibu Othman, Koplo Oswald Chaula, Koplo Mohamed Ally, Koplo Mohamed Chikilizo, Private Rodney Ndunguru, Private Peter Werema na Private Fortunatus Msofe, iliwasili juzi nchini na kuhifadhiwa katika Hospitali Kuu ya Kijeshi ya Lugalo.

Kaimu Msemaji wa JWTZ, Meja Joseph Masanja, alisema jana kuwa ratiba ya kuiaga miili ya wanajeshi hao itaanza leo mapema. “Ratiba itaanza asubuhi majira ya saa tatu.

Kwa hiyo, siyo vibaya wananchi kwa jumla wakafika kuanzia majira ya saa mbili na nusu asubuhi kuwaaga mashujaa wetu. Na ninatarajia itaendelea mpaka mchana,” alisema. Wanajeshi hao waliuawa hivi karibuni wakiwa sehemu ya askari 36 na ofisa wao mmoja, baada ya kushambuliwa na wanaosemekana kuwa waasi, wakati wakisindikiza msafara wa waangalizi wa kijeshi kutoka eneo la Khor Abeche kwenda Nyala, ambako wenzao 17 vile vile walijeruhiwa.

Jitihada zinazofanywa na Umoja wa Mataifa (UN), ikiwa ni pamoja na Rais Jakaya Kikwete, kuzungumza na Rais wa Sudan, Omar al Bashir, akimtaka kuwasaka, kuwakamata na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wale wote waliohusika na mauaji hayo, bado hazijafanikiwa hadi sasa.

Tanzania ina wanajeshi 850 kwenye kikosi cha UN cha kulinda amani katika Jimbo la Darfur.

No comments:

Post a Comment