To Chat with me click here

Monday, October 1, 2012

RUFAA YA LEMA KUSIKILIZWA KESHO

RUFAA ya kupinga kuvuliwa ubunge wa aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), inatarajiwa kusikilizwa kesho na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa, wakiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande.

Majaji wengine waliopo katika kusikiliza rufaa hiyo inayovuta hisia za watu wengi ni pamoja na Jaji Natalia Kimaro na Salum Massati, wote wa Mahakama ya Rufaa nchini.

Rufaa hiyo ambayo ilipaswa kusikilizwa Septemba 23, mwaka huu, ilisogezwa mbele hadi Oktoba 2, kutokana na mawakili wa pande zote mbili kupatwa na dharura, ambapo jopo hilo liliridhika na hivyo kusogeza mbele tarehe.

Jopo hilo lilizingatia barua iliyoomba kusogezwa mbele kwa shauri hilo hadi Oktoba 2, kutokana na mawakili, Tundu Lissu, anayemtetea Lema na kaka yake, Alute Mughwai, anayewatetea walalamikaji kufiwa na baba yao mzazi.

Tundu Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), anashirikiana na Wakili Mwandamizi Method Kimomogoro katika kumtetea mrufani, Godbless Lema.

Kwa upande wake Wakili Mughwai anashirikiana na Wakili Modest Akida kuwawakilisha wadaiwa katika shauri hilo ambao ni wanachama watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mussa Mkanga, Agness Mollel na Happy Kivuyo.

Wanachama hao walifungua shauri lililotengua ubunge wa Lema wakidai kuwa wakati wa kampeni alimdhalilisha aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk. Batilda Burian, kwa kutumia lugha za matusi.

Awali, Lema kupitia wakili wake, Method Kimomogoro, anayesaidiana na Lissu, aliwasilisha katika mahakama hiyo hoja 18 za madai, akipinga ubunge wake kutenguliwa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Aprili 5, mwaka huu.

Katika baadhi ya madai hayo, Lema aliiomba Mahakama ya Rufaa kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu, huku akiitaka mahakama hiyo imtangaze kuwa mbunge halali wa Jimbo la Arusha Mjini.

Aidha, aliitaka mahakama hiyo ya juu, iwaamuru walalamikiwa katika shauri hilo walipe gharama za rufaa hiyo pamoja na gharama za kesi iliyomalizika katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.

Katika madai mengine, Lema anamlalamikia Jaji Gabriel Rwakibarila, aliyesikiliza kesi hiyo kuwa alitoa uamuzi wake kwa kuzingatia maneno ya uvumi, huku akipuuza ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.

MWASISI WA NCCR-MAGEUZI AFARIKI DUNIA

Mwasisi wa NCCR, Ndg. Emmanuel Ole Sirikwa
MWASISI wa Chama cha NCCR- Mageuzi, Emmanuel Ole Sirikwa (70) amefariki dunia katika Hospitali ya AICC, iliyopo mkoani Arusha. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Mussa Kombo Mussa, alisema Ole Sirikwa alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kupooza (stroke), hadi alipofariki Septemba 28, mwaka huu hospitalini hapo.

Alisema hadi mauti yanamkuta, marehemu Ole Sirikwa alikuwa kamishna wa NCCR Mageuzi Mkoa wa Arusha, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na mmoja wa wajumbe wa Baraza la Wadhamini wa chama hicho.

“Marehemu Ole Sirikwa alikuwa mwasisi wa chama aliyekuwa na kadi namba 3 ya NCCR-Mageuzi, akitanguliwa na wenye kadi namba 1 na 2 ambao wamekisaliti chama na kuhamia kwingine kutokana na misukosuko ya kijamii.

“Chama kimempoteza mtu muhimu ambaye hakuyumba na aliendelea kubaki ndani ya chama chake, hali iliyotufanya baadhi yetu kumuona kama mzee wa boma la chama,” alisema Musa na kuongeza:

“Marehemu Ole Sirikwa alibaki ndani ya chama kwa sababu ya kuheshimu na kuthamini kile alichokianzisha, huku akiamini lengo na madhumuni yake bado hayajafikiwa, sisi tuliobaki tutaendeleza na kuyasimamia mazuri yote ili kufikia lengo alilokusudia,” alisema.

Mussa alisema kutokana na umuhimu wa marehemu Ole Sirikwa, chama kimeamua kuenzi uvumilivu na misimamo yake kwa kuuita ukumbi wa mikutano uliopo makao makuu jina la Ukumbi wa Sirikwa.

Alisema mazishi yanatarajiwa kufanyika Oktoba 3, 2012 kijijini kwake Olijilah, Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, yakiongozwa na Mwenyekiti chama hicho taifa, James Mbatia.

Wakati huo huo, Mkuu wa Idara ya Kampeni na Uchaguzi, Faustine Sungura, alisema kitendo cha vyama vingine kuzindua kaulimbiu na kuzifanyia kampeni nchi nzima ni dalili za kuanza kupata hofu ya uchaguzi ujao.

Sungura alisema NCCR Mageuzi imejipanga kujibu kwa vitendo kwa kuibuka na ushindi wa wabunge mwaka 2015, licha ya kutofanya operesheni wakati huu.

“Sisi NCCR Mageuzi tumejipanga na mipango yetu ipo ndani ya chama, tunafanya kampeni zetu kisiri, hatuhitaji maandamano na mziki mkubwa kwenye gari, tunataraji kuwa na mavuno mazuri kuanzia 2014 hadi 2015,” alisema.

MANISPAA YA ILALA YASHINDWA KUFIKIA LENGO

KAIMU Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Dk. Severine Assenga, amesema manispaa yake imeshindwa kufikia lengo la kukusanya Sh bilioni 26 kutoka katika vyanzo vyake vya mapato kwa mwaka wa fedha wa 2011/12.

Assenga alitoa taarifa hiyo juzi jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kikao cha kupitisha bajeti ya matumizi ya mwaka wa fedha uliomalizika Juni 30, mwaka huu kwa ajili ya ukaguzi utakaofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh.

Alisema manispaa yake imeshindwa kufikia kiwango hicho kutokana na sababu mbalimbali na kusema kuwa hata hivyo imefanikiwa kukusanya Sh bilioni 17 pekee, ambazo ni sawa na asilimia 70 ya mapato yote.

“Tumeshindwa kufikia malengo kutokana na kuwepo kwa sababu mbalimbali, ikiwemo ukusanyaji mbaya wa mapatao ya leseni za biashara ambao Serikali kuu haijaruhusu kukusanya,” alisema.

Aliongeza kuwa sababu nyingine ya kushindwa kufikia malengo ni kuwapo kwa matumizi makubwa ambapo fedha nyingi hutumika katika maendeleo kama ujenzi wa vituo vya afya, shule na ulipaji wa mishahara ya watumishi.

Assenga alibainisha kuwa uwezo wa manispaa hiyo wa kulipa madeni yake si wa kuridhisha na pia uzalishaji wa madeni mapya umekuwa ukikua kwa kasi kubwa na kusema kuwa manispaa inahitaji kuchukua hatua za makusudi ili kukabiliana na hali hiyo.

"Mapendekezo yetu ni kupunguza matumizi na kutenga kiasi cha kutosha kwenye bajeti kila mwaka ili kulipa madeni yanayotukabili. Halmashauri yetu inatakiwa kuweka mikakati endelevu ya kudumu ili kuweza kuinua mapato ya ndani kwa kiwango kikubwa,” alisema.

WASSIRA SASA AWASHA MOTO KWA DR. SLAA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Bw. Stephen Wassira, amesema watoto wa kaka yake ambao juzi walitangaza kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bi. Lilian na Bi. Esther Wassira, wana haki ya kujiunga na chama chochote cha siasa.

Alisema kitendo cha Katibu Mkuu wa chama hicho Dkt. Willibrod  Slaa kutumia jina na cheo chake wakati akiwapa kadi wanachama hao ni upotoshaji unaofanywa na CHADEMA ili kujipatia umaarufu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Bunda, mkoani Mara, Bw. Wassira alimshukia Dkt. Slaa na kumtaka awe makini kuwaita wake za watu chumbani na kuwapa kadi bila maofisa wengine wa chama hicho kushuhudia tukio hilo.

“Namhadharisha Dkt. Slaa kwani alichokifanya kinaweza kuleta mtafaruku katika ndoa za watu, Lilian na Esther ni watoto wa kaka yangu George Wassira si mimi, hawa ni watu wazima na wote wana haki ya kuchagua chama wanachokitaka,” alisema.

Aliongeza kuwa, Dkt, Slaa anaishi kwa kutafuta matukio bila kutumia akili ambapo mume wa Bi. Lilian ni mwanachama wa CHADEMA hivyo uamuzi aliochukua mkewe hauna uhusiano wowote na ukoo wao.

“Hata Makongoro Nyerere awliwahi kujiunga NCCR-Magezui wakati hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere (baba yake), akiwa hai, je, tatizo lilikuwa wapi na yeye ni mtu mzima,” alisema.

Alisema siku zote Dkt. Slaa na viongozi wengine wa CHADEMA wamekuwa wakichukizwa na jinsi anavyojibu hoja zao hivyo wanachokifanya ni kumtafutia tuhuma lakini wameshindwa kufanikiwa hivyo wamezna kuwachonganisha katika ukoo.

“Wanachukizwa ninavyojibu mambo yao hasa wanayosema katika majukwaa na kuhatarisha amani, mimi ni mzalendo wa kweli ambaye nalitumikia Taifa lengu kikamilifu na sina tuhuma za ufisadi ambao Dkt. Slaa ameufanya kuwa wimbo,” alisema.

Hata hivyo, aliwataka Watanzania waelewe kuwa ukoo wao msingi wake si vyama vya siasa bali kila mtu ana haki ya kuingia na kutoka katika chama chochote.

Alisema kitendo cha Dkt. Slaa kuhusisha ukoo huo na tukio la watoto hao kujiunga CHADEMA ni kuwadanganya Watanzania kuwa ukoo huo umegawanyika jambo ambalo si kweli.

WANAFUNZI WA BAOBAB WAFANYA ZIARA YA KIMASOMO BOA.

Meneja Masoko wa Benki ya Afrika Tanzania, Bw. Solomon Haule (aliyesimama kushoto), akizungumza na wanafunzi wa Kidato cha Sita katika Sekondari ya Baobab, waliofika Makao Makuu ya benki hiyo, Dar es Salaam juzi kwa ziara ya mafunzo.

UCHAGUZI CCM BALAA

NAGU AFANYA KWELI, MFUTAKAMBA CHALI

HATIMAYE kinyang'anyilo cha kumpata Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Wilaya ya Hanang’, mkoani Manyara, kimemalizika juzi baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dkt. Mary Nagu, kuibuka mshindi.

Katika uchaguzi huo, Dkt. Nagu alipata kura 648 wakati mpinzani wake Waziri Mkuu mstaafu Bw. Frederick Sumaye alipata kura 481 kati ya kura 1129, zilizopigwa ambapo kura 41 ziliharibika.

Uchaguzi huo ambao ulikuwa na mchuano mkali, ulisimamiwa na Mjumbe wa Kamati ya Siasa mkaoni hapa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa Bw. Elaston Mbwilo.

Nafasi nyingine iliyogombewa ni Mwenyekiti wa (CCM) wilayani hapa ambayo ilikuwa na wagombea watatu, Bw. Michael Bayo aliibuka mshindi na kuwashinda wenzake watatu.

Wagombea wengine walikuwa Bw. Hassan Hilbagroy na Bw. Goma Gwaltu, ambaye alikuwa akitetea nafasi yake ambapo Bw. Bayo alipata kura 647 na Bw. Hilbagroy (291).

Bw. Mbwilo pia alimtangaza Bi. Christina Mndeme (Mkuu wa Wilaya ya Hanang'), Bw. Anju Mang’ola, Mateo Darema na Bi. Hawa Hussen, kuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Halmashauri Kuu.

Awali mgombea wa nafasi ya ujumbe wa Mkutano Mkuu, Leonsi Marmo, alimwomba Bw. Mbwilo aondoe jina lake kwa sababu wagombea wenzake ni vigogo hivyo asingeweza kushinda.

KASHFA NYINGINE YAIBUKA TANESCO


KASHFA mpya imeibuka ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), baada ya kubainika kuwa vikombe vya kufungia nyaya za umeme vyenye thamani ya mamilioni ya fedha vimetelekezwa kutokana na baadhi ya vigogo wa shirika hilo kushindwa kunufaika na mradi huo.

Habari kutoka ndani ya shirika hilo zinaeleza kuwa vigogo hao wanadaiwa kuvikataa vikombe hivyo kwa maelezo kuwa ni vibovu, baada ya mzabuni kushindwa kuwaona vigogo hao. Wakati vigogo hao wakivikataa vikombe hivyo kwa madai kuwa ni vibovu, taarifa zinaeleza kuwa wataalamu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wamethibitisha kuwa vikombe hivyo ni vizuri na havina matatizo yoyote. Hatua ya Tanesco kupeleka vikombe hivyo kuthibitishwa na wataalamu wa Chuo Kikuu, Kitengo cha Uhandisi ilitokana na mvutano uliokuwapo baada ya vigogo walioshindwa kunufaika na mradi huo kutoa maelezo kuwa vikombe hivyo havina viwango bora. 

Hata hivyo, uchunguzi unaonyesha kuwa licha ya vigogo hao kuvikataa vikombe hivyo zaidi ya 40,000 vyenye thamani ya Sh900 milioni kwa madai kuwa vibovu, tayari shirika hilo limekuwa likivitumia katika nguzo zake zenye umeme mkubwa kwa miaka mingi. Mvutano wa viongozi hao ndani ya shirika hilo, umesababisha mradi wa kukarabati njia za umeme mkubwa bila ya kuzima umeme kwa kuondoa vikombe vilivyochakaa uliokuwa ukifanyika katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kusimamishwa mapema mwaka huu. 

Baadhi ya wataalamu wa Tanesco wanaeleza kuwa vikombe hivyo kama vitatumika vina uwezo wa kutosheleza mahitaji ya kufunga vikombe vipya katika njia ya umeme mkubwa wa kutoka kwenye mtambo wa kuzalishia umeme wa Kidatu mkoani Morogoro hadi Ubungo jijini Dar es Salaam. Pia, kumalizia ukarabati wa njia ya umeme ya Arusha hadi Moshi mkoani Kilimanjaro iliyositishwa. 

Chanzo chetu kutoka ndani ya Tanesco kinaeleza kuwa vikombe vilivyopo katika njia ya umeme ya Kidatu hadi Ubungo havijabadilishwa kwa miaka mingi hali ambayo inafanya umeme kupotea njiani kwa asilimia nyingi. Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Tanesco, Felschami Mramba alisema kuwa mikataba ndani ya shirika hilo ni mingi na kusisitiza kuwa hawezi kulijibu suala hilo mpaka atakapowasiliana na kitengo cha ununuzi cha shirika hilo. 

“Kwa sasa sina maelezo ya kina ya mikataba, hasa kuhusu suala hilo unaloniuliza, lakini mpaka wiki ijayo nitakuwa nimefuatilia na kupata jibu sahihi,” alisema Mramba. Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulika Nishati, George Simbachawene alisema suala hilo halijafika kwake.

 Simbachawene alisisitiza: “Mambo yanayofika katika ofisi yangu huwa kama malalamiko yanayoletwa na watu kutoka Tanesco na sehemu nyingine. Nikiyapata naanza kufuatilia ili kujua nini kinaendelea.” Alisema kuwa Tanesco ni shirika linalojitegemea katika utendaji wake wa kazi na ndiyo maana lina bodi yake, ambayo hukaa na kupanga mambo mbalimbali ya kufanya.

 “Wakati mwingine wizara inaingilia utendaji wa Tanesco kama tunaona kuna mambo hayaendi sawa, ila hili la ununuzi kwa kweli sijui kwa sababu halijafika ofisini kwangu kama lalamiko,” alisema Simbachawene na kushauri kuwa atafutwe Mramba. Hoja ya kuvikataa vikombe hivyo ambayo imekuwa ikitolewa na baadhi ya vigogo hao wa Tanesco ni kwamba vikombe hivyo ni vizito na nguzo haziwezi kuvibeba, vibovu na kwamba havifai katika ule utaratibu wa kufanya matengenezo bila kuzima umeme. Tanesco imekuwa ikikumbwa na kashfa mbalimbali zikiwamo matumizi mabaya ya fedha za shirika kwa baadhi ya maofisa kutumia zabuni kujinufaisha. Hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Shirika hilo, Mhandisi William Mhando alisimamishwa kazi na Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo.

 Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Wakurugenzi ilieleza kuwa Mhando alisimamishwa kazi pamoja na watendaji wakuu wengine wa Tanesco ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka. 

 Viongozi wengine wa Tanesco waliosimamishwa kazi ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji Huduma za Shirika, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi wa Ununuzi, Haruni Mattambo. Matatizo mengine ambayo yanadaiwa kuikumba Tanesco ni pamoja na uchakavu wa mitambo ya Tanesco, hujuma za miundombinu na kuingiwa kwa mikataba mibovu

HALIMA MDEE AFUNGUKA ANTAKA NYUMBA YA MCHUNGAJI LAKWATARE IBOMOLEWE


Serikali imetakiwa kumdhibiti na kumuondoa, kisha kuibomoa nyumba ya Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mchungaji Getrude Lwakatare.

Rai hiyo imetolewa na Waziri Kivuli, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee.

Taarifa kwa vyombo vya habari jana ilieleza kuwa, wakati raia wengine wakibomolewa nyumba ambazo kama ilivyo ya Mchungaji Lwakatare, zilijengwa kinyume cha sheria, Mbunge huyo amehamia na kuishi kwenye nyumba yake.

Julai mwaka huu, nyumba za wananchi waliojenga katika maeneo tengefu ya ufukwe wa Jangwani, mto Ndumbwi na mto Mbezi, zilibomolewa katika operesheni iliyoendeshwa na Baraza la Mazingira la Taifa (Nemc).

Operesheni hiyo ilihusisha takriban nyumba 15 na kuta nane. Lakini cha kushangaza nyumba ya Mchungaji Lwakatare ambayo imejengwa  kinyume cha sheria haikuguswa