Dar es Salaam. Watu
waliopokea mgawo wa fedha zilizochotwa kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow
ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) huenda wakalazimika kulipa mamilioni ya Shilingi
ambayo ni kodi ya mapato ya fedha walizopewa, imefahamika.
Hata
hivyo, habari zinasema malipo hayo ya kodi yatafanywa kwa kuzingatia matokeo ya
uchunguzi wa vyombo vya dola ambao unawashirikisha maofisa wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) kuhusu uhalali wa fedha walizolipwa.
Naibu
Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema juzi kuwa wote waliopokea mgawo wa
fedha zilizochotwa kutoka katika akaunti hiyo watapewa fomu za kuthibitisha
mapato yao ili wakatwe kodi kutokana na fedha hizo ambazo pia zinapaswa
kuhakikiwa na vyombo vya usalama kwamba ni mapato halali.
Alisema
taratibu za kufuatilia fedha hizo zimekwishaanza na ifikapo Desemba 31 wahusika
watapewa fomu ili kuthibitisha mapato yao ili hatua za kuwatoza kodi zianze.
Askofu Eusebius Nzigirwa |
Msingi
wa maelezo ya Nchemba umejengwa kwenye Sheria ya Mapato ya Kodi (Income Tax
Act) ya 2012 ambayo inaelekeza mlipaji wa kodi kuwasilisha ankara za hesabu za
mapato yake kwa TRA kila ifikapo mwisho wa mwaka na hesabu hizo huiwezesha
mamlaka hiyo kutathmini kiwango cha kodi inayopaswa kulipwa na mhusika.
“Hotuba
ya Rais (Jakaya Kikwete) imetupa nguvu kuendelea na juhudi ambazo tayari
tulikwishazianza tangu awali, maana amesisitiza kwamba lazima kodi ilipwe na
sisi hilo ni jukumu letu, tutafuatilia ili kuhakikisha kwamba fedha za
walipakodi zinarejeshwa,” alisema Nchemba.
Ikiwa
wote waliotajwa watalazimika kukatwa asilimia 30 ya fedha walizopewa kama kodi
ya mapato, TRA itakusanya zaidi ya Sh9.3 bilioni ambazo zinatokana na karibu
Sh31 bilioni zilizotawanywa kwa watu na kampuni mbalimbali kutoka kwenye
akaunti ya mmiliki wa VIP Engineering, James Rugemalira.
Askofu Methodius Kilaini |
Miongoni
mwa waliokiri kupokea fedha hizo ni aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye alipata mgawo wa Sh1.6
bilioni akisema fedha hizo zilikuwa ni za mchango wa kulipa mkopo wa shule
anayoisimamia.
Hata
hivyo, hatua yake hiyo tayari imemgharimu baada ya Rais Jakaya Kikwete kutengua
uwaziri wake kutokana na kile alichokiita kuwapo kwa makosa ya kimaadili hasa
ikizingatiwa kuwa fedha hizo ziliingizwa kwenye akaunti yake binafsi.
Taarifa ya PAC
Kamati
ya Hesabu za Serikali (PAC) ikiwasilisha taarifa yake bungeni kuhusu suala hilo
mwezi uliopita, pia iliwataja wengine waliochukua fedha hizo kutoka VIP
Engineering kuwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Mbunge wa Bariadi
Magharibi (CCM), Andrew Chenge (Sh1.6 bilioni), aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini
ambaye pia ni mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (Sh40.4 milioni) na Mbunge
mstaafu wa Sumbawanga (CCM), Paul Kimiti (Sh40.4 milioni).
Jaji Aloysius K Mujulizi |
Wengine
ni aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona (Sh40.4 milioni),
aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Tanesco, Dk Enos Bukuku (Sh161.7 milioni), Majaji
wa Mahakama Kuu, Profesa Eudes Ruhangisa (Sh404.25 milioni) na Jaji Aloysius K
Mujulizi (Sh40.4 milioni) pamoja na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usajili wa Vizazi
na Vifo (Rita), Philip Saliboko (Sh40.4 milioni).
Pia
wamo aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Emmanuel Daniel Ole
Naiko (Sh40.4 milioni), Ofisa wa TRA, Lucy Appollo (Sh80.8 milioni), Askofu
Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini (Sh80.9 milioni),
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Eusebius Nzigirwa
(Sh40.4 milioni) na Padri Alphonce Twimannye Simon (Sh40.4 milioni).
Wanastahili kulipa kodi?
Kumekuwa
na hoja za kitaalamu kwamba waliopokea fedha hizo hawastahili kulipa kodi
yoyote kutokana na madai kwamba hawabanwi na sheria za kodi kwa kuwa malipo
waliyopokea hayaangukii katika maeneo matatu yanayopaswa kutozwa kodi ambayo ni
uwekezaji, mishahara au biashara.
Akizungumzia
hilo Nchemba alisema hata fedha za misaada kutoka kwa wafadhili hutozwa kodi,
hivyo hakuna jinsi ambavyo watu waliopokea fedha hizo watakwepa wajibu wa
kutozwa mapato ya Serikali.
“Hivi
majuzi tu kuna shirika moja kutoka nje ya nchi lilitoa misaada ya vifaa vya
uwindaji, tuliwatoza kodi kwa hicho kisingizio kwamba eti walipewa msaada,
hakiwezi kusababisha wasitozwe kodi, mapato yoyote yanatozwa kodi, tofauti huwa
ni kiwango kinachotozwa tu,” alisema Nchemba.
Kuhusu
hoja kwamba fedha hizo ni chafu, naibu waziri huyo alisema madai hayo siyo ya
kweli. “Fedha hizi ziliwekwa pale BoT kutoka Tanesco, tatizo ni jinsi
zilivyotolewa pale, sasa unawezaje kusema fedha hizo ni chafu? Hizi ni fedha za
hapa nchini na hazitokani na mapato ya bangi au dawa za kulevya,” alisema.
Hata
hivyo, alisema kwa wale watakaofikishwa katika vyombo vya sheria na kufunguliwa
mashtaka kuhusu mgawo waliopewa, Serikali haitachukua kodi kwani watakuwa
wameingia katika mkondo tofauti wa kushughulikiwa kisheria.
Ufafanuzi wa TRA
Mkurugenzi
wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alisema hatua ya
mamlaka yake kuwapelekea fomu waliopokea fedha hizo ni kuwapa fursa ya kueleza
vyanzo vya mapato ya fedha zilizoingizwa kwenye akaunti zao.
“Hatuwezi
kufahamu ni kiasi gani au ni kodi ya aina gani hawa watu wanaweza kutozwa,
ndiyo maana tunawapelekea fomu ili waonyeshe vyanzo vya mapato yao na baada ya
hapo wataalamu wetu watachunguza iwapo fedha zilizoingia kwenye akaunti zao
zinapaswa kutozwa kodi na kama ni kodi basi ni ya aina gani,” alisema Kayombo
na kuongeza:
“Kuna
wale wanaosema kwamba fedha walizopewa ni mchango au msaada, hayo yote
yatafuatiliwa na ikumbukwe kwamba kazi hii inafanywa na vyombo vya dola na sisi
maofisa wetu wanachukua taarifa kusika kwa kuzingatia matokeo ya uchunguzi
unaofanywa,” alisema.
Alisema
kwa mujibu wa sheria za kodi na sheria nyingine za nchi, mapato yanayotozwa
kodi lazima yawe ni halali, hivyo TRA inachukua tahadhari ili kukwepa
kuhalalisha mapato ambayo baadaye yanaweza kuja kuonekana kupatikana kwa njia
zisizo halali.
“Leo hii ukikata kodi
katika fedha fulani maana yake unaihalalisha, sasa baadaye ikija kubainika kuwa
fedha hizo zilipatikana kwa njia haramu tunaweza kujikuta tunaharibu taratibu
za kiuchunguzi. Hivyo, ndiyo maana wataalamu wetu wanafanya kazi kwa ukaribu na
vyombo vingine,” alisisitiza Kayombo.
No comments:
Post a Comment