To Chat with me click here

Monday, December 29, 2014

Dr. SLAA: JK AWAOMBE RADHI WATANZANIA!


Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amemtaka Rais Jakaya Kikwete, kuwaomba radhi Watanzania kwa madai ya kuingizwa kwa wawekezaji wasiojali maslahi ya wazalendo.

Kutokana na hilo alisema kuna uwezekano wa kuwapo kwa kashfa nyingine zaidi ya ile ya akaunti ya Tegeta Escrow katika eneo la Magereji, barabara ya kwenda Wazo Hill, jijini Dar es Salaam kwa madai ya mwekezaji kuwanyang’anya eneo la shughuli za ufundi wa magari wakazi wa Kata ya Wazo takribani 4000 na vijana ambao wamewekeza kiasi cha Shilingi bilioni 35 kwa maendeleo yao ya ufundi wa magari  kwenye eneo hilo.

Dk. Slaa alitoa kauli hizo wakati akihutubia katika mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Mkanada jijini humo jana kwa lengo la kuwashukuru wakazi wa kata hiyo kwa uchaguzi wa serikali za mitaa uliomalizika hivi karibuni na hivyo kuelezwa kero hizo ambazo wananchi hao wanakabiliana nazo ikiwa ni pamoja na eneo hilo kudaiwa kutwaliwa na mwekezaji huyo na kuwaondoa vijana hao kwa bati 20 na mifuko ya saruji 20.

Dk. Slaa alisema kuwa wawekezaji wazuri ni wale wanaohakikisha wazalendo wananufaika na wao pia na siyo kuwa wauaji na wasiojali utu wa watu akisema hiyo ni Escro nyingine zaidi ya ile ya uchotwaji wa mabilioni ya Shilingi.

“Haiwezekani watu wamewekeza kwa bilioni 35 wewe unawatoahalafu unawapa mifuko kumi ya saruji na mabati 20,” alisema Dk. Slaa.

Alisema kutokana na hilo, Rais awaombe samahani Watanzania huku akihoji kwamba inakuwaje Rais Kikwete tangu atangaze kuwapo kwa majina 40 ya wanaouza dawa za kulevya na wanaosafirisha wanyama nchi za nje, lakini hadi sasa hajayaweka wazi kwa wananchi.

Aliongeza kuwa, hotuba ya Rais Kikwete kwa wazee wa Mkoa wa dare s Salaam Jumatatu iliyopita ilikuwa na udhaifu mkubwa kwani dhahiri ilionyesha kumtetea mmiliki mpya wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Herbinder Sethi, bila kuangalia maslahi ya taifa.

Dk. Slaa pia alimtaka Rais Kikwete kuwashughulia baadhi ya viongozi ndani ya CCM wanaodaiwa kuhusika kwenye biashara ya kusafirisha wanyama.
Baadhi ya wakazi hao walidai kuwa, sakata la mgogoro wa mpaka wa ardhi katika eneo la Chasimba, bado bichi kwani wananchi hao walitaka kuondolewa kwa utapeli.

Wakazi hao wana mgogoro wa muda mrefu na kiwanda cha Saruji cha Wazo baada ya kudaiwa kuwa walilivamia eneo hilo.

Walisema katika awamu ya kwanza walitaka kuwahamishia eneo la Bungu kwa Masista watu 1,000, lakini baadaye waligundua kuwa eneo hilo kwa mujibu wa ramani za mipango miji liliwekwa kwa ajili ya shughuli za biashara, nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa na kwa ajili ya nyumba wakubwa.

Hata hivyo, wakazi hao walipohoji kuhusu hilo na watu wengine 3500 kwamba watawapeleka wapi, hakukuwa na majibu na hivyo madiwani kutoridhishwa na hilo huku wakitaka wananchi hao kuungana pamoja kwa ajili ya kufuatilia suala hilo.

Dk. Slaa aliitaka serikali kuangalia suala la kujenda viwanda vya ndani kusaidia wazalendo badala ya kuwaondoa kwenye maeneo kama hayo ambayo wanaendesha shughuli zao kwa ajili ya masuala ya kiuchumi na ajira zao.

No comments:

Post a Comment