To Chat with me click here

Monday, December 29, 2014

KAFULILA: ESCROW INAZAMISHA NCHI


Mbunge wa Kigoma Kusini(NCCR-Mageuzi),
David Kafulila.

Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, amesema kashfa ya kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), itaendelea kutafuna uchumi na kuongeza umaskini nchini kutokana na serikali kusuasua kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika.

Kafulila, ambaye ndiye mbunge aliyeibua mjadala kuhusu kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow, bungeni, alisema hayo alipokuwa akitoa tathmini ya kufunga mwaka 2014 jana.

Kutokana na hali hiyo, alisema wahisani hawatachangia bajeti ya mwaka huu na ya mwaka ujao na hivyo, kuiweka serikali katika wakati mgumu.

“Hii itaidhoofisha CCM na kuijenga Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) 2015 na hivyo, uchaguzi kuwa mgumu na wa kihistoria,” alisema Kafulila.

Alisema mwaka 2014 umemalizika Bunge likiwa limejijengea imani kubwa kwa wananchi, huku serikali ikiporomoka kutokana na namna Bunge lilivyosimamia sakata la akaunti hiyo na serikali ilivyosuasua kushughulikia.

Kafulila alisema hakuna matumaini ya kiuchumi katika mwaka ujao wa 2015 kwa sababu nchi itakuwa na mahitaji makubwa ya uchaguzi, vitambulisho vya taifa na kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa, mambo ambayo yatahitaji fedha nyingi, ambazo hakuna.

Alisema sababu mojawapo iliyochangia uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika Desemba 14, mwaka huu, kuharibika ni serikali kukosa fedha.

Kafulila alisema wakati kukiwa na mambo hayo makubwa yanayohitaji fedha, serikali mpaka sasa ipo taabani kifedha kiasi, ambacho hata kandarasi za barabara zimesimamishwa kutokana na ukata. 

Alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inakusanya Sh. bilioni 800 kwa mwezi wakati mahitaji ya mishahara peke yake ni takriban Sh. bilioni 500, hivyo zinabaki Sh. bilioni 300, ambazo hazitoshi hata kunulia karatasi na mafuta kuendesha ofisi za serikali nchini kote.

Kafulila alisema licha ya uchumi kukua, maendeleo hayaonekani kwa sababu unakuzwa na sekta za madini, utalii, mawasiliano, ambazo hazibebi watu wengi, pia kero ya maji, ambayo kwa mujibu a utafiti wa taasisi ya Synovate, ni kero namba moja Tanzania, lakini serikali imeshindwa kabisa, ingawa ipo kwenye nchi ya 11kwa mito mingi duniani.

“Bado tunakosa wawekezaji wa kimkakati kwa mfano wa uamuzi wa serikali kuchukua mkopo wa dola bilioni 10 kwa ujenzi wa bandari ya Bagamoyo wakati pesa hiyo ingetosha kujenga reli ya kati ya kimataifa kwa dola bilioni sita na ziada ya dola bilioni nne zingetosha kupanua na kuimarisha bandari ya dare s Salaam, Mtwara, Tanga,” alisema Kafulila.

No comments:

Post a Comment