Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG)
mstaafu,Ludovick Utouh
|
MDHIBITI na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovick Utouh, amesema serikali
inatakiwa kuhakikisha fedha zake zilizokuwepo kwenye akaunti ya Tegeta Escrow
zinarudi kama ilivyokuwa kwa zile za EPA.
Katika mahojiano yake
na Raia Mwema yaliyofanyika jijini Dar es Salaam wiki hii, Utouh alisema kama
angepewa fursa ya kumshauri Rais Jakaya Kikwete kuhusu nini cha kufanya na
suala la Escrow bila shaka angemwambia ahakikishe anapata kwanza fedha
zilizopotea.
“Kwanza niseme kwamba
aliyetoa pendekezo kwa serikali kwamba iwabane walioiba fedha za EPA
wazirudishe kwanza kabla ya kufuata mikondo ya kisheria ni mimi. Hela kurudi ni
jambo la muhimu sana.
“Ushauri wangu ni
kwamba uchunguzi unatakiwa ufanyike na wale watakaobainika kufanya wizi basi
warudishe fedha walizoiba na halafu wapelekwe mahakamani.
“Watu wanaolalamika
kuhusu wezi wa EPA wanafanya hivyo kana kwamba watu walirudisha fedha na
wakaachiwa jambo ambalo si la kweli. Hela zilirudi na bado kesi zikaendelea
mahakamani na zinaendelea hadi hivi leo tunavyozungumza.
“Hivi kuna tatizo
gani kama mtu atarejesha fedha aliyochukua? Huyu mtu unaweza kumkuta na hatia
na ukampeleka jela lakini akifika kule atakula na kulala bure kwa gharama za
walipa kodi. Kama atalipa fedha alizoiba, ndizo fedha hizohizo zitatumika
kumhudumia.
“Ninachosema hapa,
kitu kizuri ni kipi? Kuendelea na kesi kwa miaka mingi na huku ukitumia fedha
za umma kuzihudumia au angalau kushinikiza kwanza hela zilizochukuliwa
zirudishwe na kesi zikaendelea kama kawaida?
“Kutaka hela
zirudishwe haina maana hata kidogo ya kusamehe watuhumiwa bali maana yake ni
kuhakikisha kile kilichochukuliwa kinapatikana kwanza,” alisema Utouh.
Katika mahojiano hayo,
Utouh alisema ni sahihi kwa ripoti ya CAG kuhusu suala la Escrow kusema fedha
zilizokuwepo katika akaunti ya Escrow ni za umma na pia si umma kwa vile huo
ndiyo ukweli.
“Kama ulifuatilia
mjadala ule wa bungeni, kitu cha kwanza ambacho kilisemwa na kipo kweli ni
suala la kodi. Ndani ya fedha zilizokuwepo kwenye akaunti ya Escrow kulikuwa na
kodi. Kodi ni mali ya umma. Hivyo kwenye eneo hilo la kodi, fedha za umma zipo.
“Jambo la pili lipo
kwenye historia ya kuanzishwa kwa akaunti hiyo. IPTL na Tanesco walikuwa na
mzozo kuhusu malipo ya capacity charge. Mgogoro ulikuwa mkubwa na wakaamua
kuweka fedha za malipo hayo kwenye akaunti ya Escrow huku wakisubiri shauri lao
kutoka katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro.
“Sasa, nizungumze
kama mfano tu, hypothetical, kwamba IPTL walikuwa wanaichaji Tanesco shilingi
30 kwa siku. Tanesco wakaona kwamba wanalaliwa kwa gharama hizo. Wanalipa zaidi
ya wanavyotakiwa kulipa.
“Wakaenda mahakamani
kushitaki. Uamuzi uliotoka ni kwamba, ni kweli Tanesco wamebambikiwa hizo
gharama. Inabidi gharama za capacity charge zikokotolewe upya. Sasa ofisi ya
CAG haina mamlaka ya kufanya ukokotoaji huo.
“Kwa hiyo, kama
ukokotoaji ungefanyika, labda tuseme IPTL ingetakiwa kutoza shilingi 20 kwa
siku, maana yake ile tofauti ya shilingi 30 inayotozwa na shilingi 20
inayotakiwa kutozwa, yaani shilingi 10, ingekuwa ya Tanesco.
“Hii maana yake ni
kwamba, katika kila shilingi 30 iliyokuwepo katika Escrow, ukiondoa zile za
kodi, shilingi 20 zilikuwa za IPTL kwa sababu ya umeme wake iliyouza na
shilingi kumi zilikuwa za Tanesco ambayo ni taasisi ya umma,” alisema.
No comments:
Post a Comment