Aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa Ndg. John Tendwa |
Harare. Siku moja baada ya kutangazwa rasmi kwamba
aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa amestaafu kwa mujibu
wa sheria, amejitokeza na kueleza yaliyo moyoni mwake.
Katika
mahojiano maalumu na vyanzo vyetu vya habari jijini Harare jana, Tendwa alisema
amepokea kwa mikono miwili kustaafu kutoka katika nafasi hiyo nyeti katika
siasa za Tanzania, huku akisema anajiona mwenye bahati kufanya kazi na marais
wawili katika nafasi yake.
Tendwa
amefanya kazi chini ya uongozi wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na baadaye Rais
Jakaya Kikwete. Nafasi ya Tendwa, imechukuliwa na Jaji Francis Mutungi ambaye
alikuwa jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma.
Akizungumzia
kuhusu viongozi wa vyama vya upinzani kupokea kwa nderemo kustaafu kwake, Tendwa
alisema wala hashangai kuyasikia hayo kwani inaonyesha kwamba kazi yake alikuwa
akiifanya vyema na mujibu wa sheria.
“Unajua
unapokuwa msajili na ukaona wadau wote wanakushangilia hapo ujue kuna tatizo
kubwa, nimekuwa ninafanya kazi yangu vizuri sana kwa kuzingatia misingi ya
sheria ambayo imewekwa kwa mujibu wa sheria na kanuni,”alisema Tendwa.
Alisema
kwamba, “Unajua kuvilea vyama ni kazi kubwa sana ndugu yangu, maana kuna wakati
hata Chama Cha Mapinduzi (CCM) walikuwa wanasema ninaegemea na kuvipendelea
sana vyama vya upinzani. Leo nimestaafu nasikia vyama vya upinzani vinasema
kwamba nilikuwa nawapendelea CCM, hiyo inaonyesha kwamba nilikuwa ninafanya
kazi yangu sawa sawa.”
Kitu
gani ambacho Tendwa hatakisahau?
Alisema
kwamba katika miaka yake 13 ambayo amekuwa msajili hatomsahau waziri mmoja wa
CCM.
Hata
hivyo, vyanzo vyetu vya habari vilimbana kumtaja waziri huyo, lakini agoma kwa
madai kwamba hapendi kuendeleza malumbano naye baada ya kustafu kwake utumishi
wa umma.
Tendwa
alisema katika utumishi wake, waziri huyo alikuwa akimpatia wakati mgumu sana
kwa kumpakazia kwamba yeye ni mpinzani.
“Katika
miaka yangu 13 ofisini sitaweza kumsahau huyo waziri maana alikuwa ananipakazia
kwamba mimi ni mfuasi wa vyama vya upinzani. Ninamshukuru Mungu kwamba baadaye
alikuja kuniomba msamaha, lakini ilikuwa imenisumbua sana katika kazi zangu,”
alisema huku akionyesha masikitiko
Kwa nini vyama
vinashuka?
Kuhusu
kushuka na kupanda kwa vyama vya siasa hasa vile vya upinzani nchini baada ya
uchaguzi kumalizika, Tendwa alisema katika kipindi chake cha uongozi aligundua
kuwa migogoro ndani ya vyama hivyo ndio chanzo kikubwa cha kupoteza mvuto kwa
wananchi.
“Tatizo
la vyama vingi vya upinzani Tanzania vinadhani kuwapata wabunge basi ndio
vinakuwa vimechukua Serikali, vinasahau kujizatiti na kujipambanua mbele ya
macho ya wapigakura kuwa vinasimamia kitu gani, badala yake nimekuwa vikiishia
kwenye migogoro isiyo ya lazima,” alisema Tendwa.
Tendwa
alielezea jinsi ambavyo NCCR-Mageuzi ilivyokuwa na nguvu sana katika Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 1995, lakini baada ya kuingia kwenye migogoro chama hicho
kikapoteza mvuto.
“Badala
ya kujiingiza kwenye migogoro vinatakiwa kujipanga kisayansi, lazima wajue
kwamba siasa ni sanyasi,” alisema.
Alisema
hata CUF kilianza kupoteza mvuto kwa jamii baada ya kupata wabunge na kuanza
kuibuka migogoro ya ndani.
Tendwa
alisema anajivunia kitengeneza muundo wa ofisi ambayo inazingatia maadili.
Alisema
wakati anakabidhiwa ofisi alikuwa peke yake ndiye mwanasheria mwenye kiwango
cha shahada ya chuo kikuu, lakini hivi sasa msajili mteule atakuta zaidi ya
wanasheria 16 katika ofisi zote tano za kanda pamoja na makao makuu.
Pia
alisema aliweza kuleta nidhamu ya matumizi ya fedha pamoja na kuleta weledi
katika kujenga misingi imara ya ofisi hiyo ambayo imekabidhiwa jukumu
kuvisimamia na kuvilea vyama vya siasa nchini.
Ushauri kwa mrithi
wake
Tendwa
alisema hawezi kumfundisha kazi Jaji Mutungi kwani anaamini atafanya kazi yake
kwa mujibu wa sheria na taratibu kama ambavyo miongozo inavyotaka.
“Mutungi
atafanya kazi kwa mujibu wa sheria, siku zote atafuata sheria na kutafsiri
sheria maana yeye ni Jaji. Ninawaomba wadau wampatie ushirikiano maana sasa
anakuja kufanya kazi na wanasiasa,” alisema Tendwa.
Alisema
endapo Jaji Mutungi ataanza kubezwa na wanasiasa anatakiwa kujua ndani ya moyo
wake kwamba anafanya kazi yake sawasawa.
“Ila
kama ataona wanasiasa wanamsifia basi atakuwa kuna sehemu ambazo hatekelezi
vyema majukumu yake. Kufanya kazi na wanasiasa kunahitaji busara na sio kufuata
vitabu vya sheria vinasemaje,” alimshauri Jaji Mutungi.
Alisema
baada ya kustaafu ana mpango wa kufanya kazi za ushauri katika siasa za
kimataifa na sio siasa za maji taka.
“Nahitaji
muda kidogo kufikiri nitafanya nini ila napenda sana kuwa ‘international
consultant’ kwenye masuala ya siasa, lakini pia ikumbukwe kwamba mimi ni
mwanasheria ambaye nimekuwa katika masuala ya uwakili kwa takriban miaka 23.
Muda utaongea nifanye nini, ngoja kwanza nikabidhi ofisi,” alisema Tendwa.
No comments:
Post a Comment