WAKATI
kampeni za uchaguzi mdogo Chalinze zikikaribia ukingoni kwa wapiga kura
kumchagua mbunge wao siku ya
Jumapili ijayo, Mkuu wa Mila wa jamii ya Wamasai wa Tanga, Morogoro na Pwani, Chifu Tiku Moreto,
amempa baraka za ushindi mgombea wa CHADEMA, Mathayo Torongey, akimtaka atimize
wajibu wake kwa kutenda haki kwa wote.
Katika
tendo hilo lililofanyika juzi asubuhi, kwa faragha katika makazi ya kiongozi
huyo wa kijadi, maeneo ya Kibaha Vijijini, kijijini Gumba, Chifu Moreto,
alimfanyia dua ya kimila, kisha kumtakia kila la heri mgombea huyo, ambapo
alimpatia kitu mfano wa kalamu kama ishara ya uongozi unaosimamia haki.
Kabla
ya tendo hilo la kimila, kiongozi huyo wa kimila alitoa nasaha zake kwa msafara
wa viongozi wa CHADEMA waliofika kijijini hapo, wakiongozwa na Makamu
Mwenyekiti wa CHADEMA, Said Issa Mohamed, ambapo Chifu Moreto alisema pia
anamtakia baraka za Mungu, Torongey.
“Mimi
kama kiongozi wa kimila, wote mnaogombea ni wa kwangu…yule mwenzako wa CCM naye
alikuja hapa…natambua kuwa wewe ni Mmasai mwenzangu, lakini mimi kama kiongozi
sina CHADEMA wala CCM, wote ninyi ni wa kwangu. Sina cha chama tawala wala
upinzani. Nakutakia mafanikio mema katika uchaguzi huu.
“Ni
kweli kuwa CCM imekuwa na udhaifu mwingi, ona hata hapa kwangu wanataka
kupauza. Ni kwa sababu tu mimi ningali hai hapa, lakini nasema kuwa mimi kama
kiongozi wa mila sina cha chama tawala wala upinzani,” alisema Chifu Moreto
kupitia kwa mtafsiri wake.
CHADEMA wazungumza
Mapema
akitoa nasaha za msafara wao kwa niaba ya Makamu Mwenyekiti, Mohamed, mmoja wa
makamanda wa chama hicho waliofika kwa chifu huyo, Alphonce Mawazo,
alisema kuwa migogoro ya wakulima na wafugaji imekuwa ikisababishwa na uongozi mbovu,
unaoweka sera zinazosababisha makundi hayo mawili kukosa haki zao za msingi.
Alisema
kuwa katika maeneo mengi, wafugaji wamekuwa kama wakimbizi kwenye maeneo yao,
hivyo kujikuta wakigombania ardhi ya malisho ya mifugo yao na wakulima ambao
nao wanahitaji maeneo hayo kwa ajili ya kilimo.
“Baba yetu chifu…mimi
natoka jamii ya wafugaji kama ninyi…ingawa sisi Usukumani tunafuga na kulima
pia. Sisi watu wa jamii ya wafugaji mifugo yetu ndiyo benki yetu, mifugo yetu
ndiyo M-Pesa zetu, mifugo yetu ndiyo inatupatia wake, mifugo yetu ndiyo kila
kitu, sasa kwa sera za CCM, chama kilichoko madarakani sasa, wafugaji miaka
michache ijayo tutakosa pa kukimbilia.
“Wakati
ule wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, serikali ilijali watu wake, wafugaji
tuliletewa mabwana mifugo, wakulima tuliletewa mabwana shamba, leo hakuna tena
mambo hayo…badala yake sera wanazotuletea ni kupunguza mifugo, sasa wanataka
kuvunja kabisa benki zetu, wachukue hata kilichobaki.
“Kabla
ya sera hizi mbovu walianza kwa kupora ardhi…eti leo hii serikali yetu haiwezi
kutenga maeneo kwa ajili ya wakulima na wafugaji, lakini inao uwezo wa kupora
ardhi kwa ajili ya kumpatia mwekezaji aliyetoka China au Marekani maelfu ya ekari, huku watu
wake wakitaabika kwa kukosa ardhi ya kilimo au kufugia, baba yetu nchi hii
imekuwa ya hovyo, serikali haijali watu wake tena,” alisema Mawazo.
Naye
mgombea Torongey alimshukuru kiongozi wake wa kimila kwa baraka na heri
alizomtakia kwenye uchaguzi, akikubali maagizo aliyopewa ya kuwatumikia
wananchi wote kwa haki, bila kuwabagua.
No comments:
Post a Comment