Maelfu
ya watoto wakiwa na umri wa hadi miaka minane wanafanya kazi kwenye migodi
midogo midogo nchini Tanzania wakiwa wanakabiliwa na kitisho kikubwa kwa afya
na maisha yao, lilisema shirika la Human Rights Watch (HRW) katika ripoti yake
iliyotolewa siku ya Jumatano (tarehe 28 Agosti).
"[Watoto
hao] wanachimba na kutoboa chini kabisa, wanabanja mawe, wanafanya kazi chini
ya ardhi kwa zamu ya hadi masaa 24, na wanasafirisha na kubeba mifuko mizito ya
dhahabu ghafi," ilisema HRW. "Watoto wanakabiliwa na hatari ya
kujeruhiwa kwa miamba inapopasuka na ajali za vifaa, na pia madhara ya muda
mrefu ya kiafya kutokana na kutumia madini ya zebaki, kuvuta vumbi na kubeba
mizigo mizito."
Kundi
hilo la haki za binadamu linasema watoto wengi wanaofanya kazi kwenye migodi
ama ni mayatima au watoto wengine walio kwenye mazingira hatari ambao wanakosa
mahitaji ya lazima na msaada. Wasichana wanaoishi karibu na maeneo ya machimbo
pia wanakabiliwa na unyanyasaji wa kingono na shinikizo la kuwa makahaba, HRW
iligundua.
"Wavulana
na wasichana wa Kitanzania wanamiminika kwenye migodi ya dhahabu kwa matumaini
ya maisha bora, lakini wanajikuta wamenaswa kwenye mduara mbaya wa hatari na
fadhaa," alisema Janine Morna, mtafiti mwenza wa haki za watoto kwenye
HRW. "Tanzania na wafadhili wanapaswa kuwaondoa watoto hawa kwenye migodi
na kuwapeleka skuli au vyuo vya mafunzo ya amali."
"Kuwaandikisha
watoto kazi hatari za uchimbaji madini ni moja ya aina mbaya kabisa za ajira za
watoto chini ya makubaliano ya kimataifa, ambayo Tanzania ni sehemu yake,"
ilisema HRW.
Tanzania
ni ya tatu barani Afrika kwa uzalishaji wa dhahabu na madini hayo ya thamani ni
chanzo kikuu cha fedha za kigeni kwa nchi hiyo, ambapo usafirishaji wake nje ya
nchi kwa miezi sita ya kwanza ya mwaka 2013 ulifikia dola bilioni 1.8, kwa
mujibu wa benki kuu.
Human
Rights Watch yenye makao yake makuu nchini Marekani ilifanya utafiti wake ndani
ya mwezi Oktoba na Disemba 2012 kwenye maeneo ya migodi kaskazini magharibi na
kusini mwa Tanzania, na katika miji ya Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya. Watafiti
walitembelea maeneo 11 ya uchimbaji madini kwa ajili ya ripoti hii.
No comments:
Post a Comment