Paul Kagame; Rais wa Rwanda |
Aliyekuwa Rais wa Marekani Bill
Clinton, hivi majuzi amemtetea Kagame kutokana na tuhuma zinazomkabili za
kuwasaidia waasi wa M23 nchini DRC.
Kwa muda wa miezi takriban minne
kumekuwa na maneno ya kejeli kutoka kwa Serikali ya Rwanda na kwa hakika maneno
hayo yanatoka mdomoni mwa Rais Paul Kagame na maofisa wa ngazi za juu katika
Serikali yake.
Kagame amekuwa mbogo baada ya Rais
Jakaya Kikwete kumshauri afanye mazungumzo na wapiganaji wa Kihutu
waliokimbilia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) baada ya kutuhumiwa kufanya
mauaji ya kimbari nchini mwake mwaka 1994.
Inakadiriwa kuwa Watutsi na Wahutu
800,000 wenye msimamo wa wastani waliuawa wakati huo, ingawa takwimu hizo zina
utata, kwani wako wanaodai kuwa nchi hiyo wakati huo ilikuwa na idadi ndogo ya
watu ambao idadi hiyo inasemekana ndio waliouawa.
Pia, wapo wale ambao wanaweza
kushangaa kwa nini Kagame amekuwa hivyo na kuikosea heshima Tanzania, nchi
ambayo imekuwa mstari wa mbele kupokea wakimbizi wake toka miaka ya 1960 na kwa
nini Rais Kikwete alitoa ushauri huo.
Kagame hakupendezwa na ukweli huo
kwani kila mara amekuwa akikataa kuwa hana mkono katika mapigano yanayoendeshwa
na vikundi vya msituni vinavyoanzishwa nchini DRC kila inapotokea hali kutulia.
Kikwete amekuwa akijua jambo hili kwa
muda mrefu kwani amekuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa kipindi cha miaka
kumi na amekuwa akihudhuria mikutano ya kutafuta amani ya DRC bila mafanikio
kwa sababu kila kikundi kinapoingizwa katika jeshi la DRC na kudai kuwa
kimemaliza vita kinazuka kikundi kingine ambacho nacho kinaanzisha mapambano
dhidi ya serikali.
Kofi Annan, Katibu Mkuu wa zamani wa
Umoja wa Mataifa (UN) alikuwa mkuu wa shughuli za kijeshi za umoja huo kabla
hajapanda cheo na kuwa katibu mkuu wa umoja huo, alipotembelea Rwanda baada ya
kumalizika kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe, msafara wake ulirushiwa nyanya.
Hiyo ilikuwa ni kama kumpa
ujumbe kuwa hakuna alichofanya wakati ule Watutsi walipouawa na Wahutu
mwaka 1994.
Masikini! Annan angefanya nini wakati
alipokuwa akiyaomba mataifa makubwa kuingilia kati ili kusitisha mauaji kila
moja lilikuwa likiangalia maslahi yake na ulikuwepo mpango wa uchelewashaji wa
makusudi.
Baadaye Annan alipokuwa akigombea
Ukatibu Mkuu wa UN ni Rwanda pekee katika nchi za Afrika ndiyo iliyopinga na
hata alipokuwa akiomba kuongezewa muda ni nchi hiyo iliyokuwa kinara wa
kumpinga wakati ukweli ni kuwa mambo yote yaliyokuwa yakifanyika wakati huo
Kagame alikuwa akiyajua.
Aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Rwanda,
Meja Jenerali Kayumba Nyamwasa, alinukuliwa na Shirika la Utangazaji la
Uingereza (BBC) akiwa uhamishoni Afrika Kusini akithibitisha kuwa vikundi
vyote vimekuwa vikianzishwa na Kagame kwa nia ya kuhakikisha kuwa Wahutu na
jeshi la zamani la nchi hiyo ambalo kwa sehemu kubwa linaundwa na waliokuwa
vijana wa Inteharamwe hawapati muda wa kujijenga.
Kwa maneno mengine, Kagame ameifanya
ardhi ya DRC kama uwanja wa mapambano kati yake na wapinzani wake ambao wako
mashariki mwa nchi hiyo.
Jenerali Nyamwasa, ambaye kabla ya
kukimbilia Afrika Kusini alikuwa Balozi wa Rwanda nchini India anasema kuwa
Kagame ndiye aliyeamrisha kutunguliwa kwa ndege iliyokuwa imebeba ujumbe wa
nchi hiyo pamoja na Rais Juvenal Habyarimana na Cyprian Ntyaramira wa
Burundi ambao ulikuwa umetokea Tanzania kwenye mkutano wa kujadili amani ya
nchi hiyo.
Baada ya vita kumalizika na hatimaye
RPF kuchukua uongozi, Ufaransa, mtawala wa zamani wa Rwanda ilimtuhumu
Kagame kwa kusababisha mauaji ya kimbari kwani Wahutu wasingianzisha chinja
chinja ya Watutsi kwa wakati huo kwani mazungumzo yale yalikuwa yanaelekea
ukingoni na hatua ya mwisho ingekuwa kwa RPF kuwa chama cha kisiasa ambacho
kingeshiriki kwenye uchaguzi.
Nia ya Kagame ilikuwa ni kuchukua
uongozi Rwanda kwa nguvu kwa sababu kwa mizania ya siasa za nchi hiyo ambazo
zimejikita zaidi kwenye ukabila ingekuwa vigumu kwa Watutsi walio wachache
kushinda.
Sababu ya pili ambayo ndiyo
iliyowafanya RPF wakatae au watumie nguvu ilikuwa ni juhudi ya Marekani ambayo
ilikuwa mfadhili mkuu wa RPF kuhakikisha kuwa ushawishi wa Ufaransa katika eneo
la Maziwa Makuu unaondoshwa kwa gharama yoyote.
Waandishi hao wanabainisha kuwa wakati
huo kulikuwa na vita vya kijasusi baina ya Marekakani na Ufaransa ambavyo
baadaye vilibadilika na kuwa ni vita vya kijeshi.
Kagame alikuwa Mkuu wa Idara ya
Usalama wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda kabla ya kujiunga na RPF. Ufaransa ikimsaidia Habyrimana na
Marekani ikiwasaidia RPF ambao tayari walikuwa wakisaidiwa na Uganda
walijipatia taarifa za kijasusi kutoka kwa Serikali ya Rwanda na wapiganaji
wake.
Majasusi wa Marekani ambao walikuwa
wakitumia njia za kijasusi za siri za kunasa taarifa za mawasiliano katika eneo
la Afrika Mashariki walifanikisha mipango ya RPF katika uwanja wa mapambano.
Marekani ilikiri kuwa kuanzia 1994
ilikuwa ikiwasaidia RPF kwa kuwapatia silaha na Kagame alipewa simu ya
satelaiti aina ya Motorola INMARSAT ambayo licha ya kufungwa kitaalam
(encryption) ili mawasiliano yake yasinaswe na wapiganaji wa Serikali ya Rwanda
au yeyote yule, kwa bahati mbaya shirika la Ujasusi la Kimataifa la Ufaransa,
DGSE (Direction Generale de la Securite Exteriure) lilifanikiwa kunasa
mawasiliano yale na Ufaransa iliituhumu Marekani kwa kutoa kombora
lililoiangusha ndege iliyokuwa imembeba Rais Habyarimana.
Kwa maana nyingine, ni kuwa Kagame
hawezi kukwepa mkono wa sheria wakati utakapofika kwani taarifa muhimu za namna
mambo yalivyokuwa yakienda katika uwanja wa mapambano, mawasiliano yake
yamehifadhiwa na taasisi hiyo ya kijasusi ya Ufaransa.
Waandishi hao wamebainisha kuwa kwa
kuwa Rais Mobutu Seseseko wa Zaire (sasa DRC) alikuwa akimsaidia Jonas
Savimbi ambaye Wamarekani walikuwa wameishamchoka na walimtaka aache vita ili
utulivu urejee Angola, nao wavune madini na mafuta huko wakiwa na sababu ya
kumwondoa Mobutu madarakani ili kukata mizizi ya usaidizi aliokuwa akiupata
Savimbi, ambaye wakati huo alikuwa kiongozi wa UNITA, iliyokuwa ikipigana vita
vya msituni dhidi ya Serikali ya Angola chini ya MPLA.
Sababu nyingine ilikuwa kwa Mobutu
kuwasaidia Wahutu ambao walikuwa kipenzi cha Ufaransa ilibidi aondolewe ili
kuhakikisha kuwa Wamarekani wanalishika na kulidhibiti eneo lote la Maziwa
Makuu.
Ikumbukwe kuwa wakati huo Rais Bill
Clinton ambaye hivi majuzi amemtetea Kagame kutokana na tuhuma zinazomkabili za
kuwasaidia waasi wa M23 nchini DRC, ndiye aliyekuwamadarakani wakati huo
na alifanya juhudi kubwa kuhakikisha kuwa shughuli za kijasusi zinaendeshwa
katika mtindo ambao utakuwa na manufaa zaidi kiuchumi na siyo kisiasa kama
ilivyokuwa wakati wa vita baridi.
DRC ilikuwa muhimu kwa majasusi
wa Marekani, hasa kwa uzarishaji wa madini ya coltan ambayo hutumika
kutengenezea simu za mkononi, madini hayo hayapo sehemu nyingine yoyote duniani
zaidi ya DRC.
Clinton alihakikisha kuwa anafanya
kila awezalo kuondoa ushawishi wa Ufaransa nchini Sudan kwa kuwataka viongozi
wa SPLA wakati huo, Kanali John Garang na wengine wadai uhuru kamili na
siyo utawala wa shirikisho kutoka Sudan ili mradi Ufaransa ikose mafuta
yaliyokuwa yakichimbwa kutoka Sudan Kusini.
Waandishi hao wamebainisha kuwa
Marekani ilitoa dola 100 milioni ili kumsaidia Laurent Kabila kuanzisha jeshi
la watoto waliokuwa wakijulikana kama Kadogoo wakiwa na malengo ya
kumwondoa Mobutu.
Kufikia mwaka 1997, Shirika la
Kijasusi la Marekani (NSA) lilikuwa imejenga vituo vya kuendesha shughuli za
kijasusi ili kunasa taarifa za mawasiliano kupitia simu, nukushi, redio katika
sehemu mbalimbali za eneo la Maziwa Makuu kama vile, Fort Portal nchini Uganda,
Kigali Rwanda na Kongo Brazaville.
Ufaransa ambayo ilikasirishwa na jinsi
Marekani ilivyofanikisha kuwaondoa vibaraka wake katika DRC na Rwanda
ilihakikisha kuwa inawaandaa wanajeshi ambao walimpindua Rais Pascal
Lissouba wa Congo Brazaville ambaye alikuwa ni kipenzi cha Marekani.
No comments:
Post a Comment