Chemba ya Bunge la Afrika Mashariki inavyoonekana wakati kikao kikiendelea |
Arusha. Kikao cha Bunge la
Afrika Mashariki (EALA), jana kilivunjika kwa mara ya pili baada ya Wabunge wa
Tanzania, kutoka ndani ya ukumbi wakipinga kanuni kuvunjwa juzi.
Baada
ya wabunge wa Tanzania kutoka nje, Spika wa Bunge hilo, Margareth Zziwa
aliahirisha Bunge kwa dakika 15 ili kuweka mambo sawa, lakini jitihada za
kuwashawishi ziligonga mwamba na kuamua kuahirisha Bunge hadi leo.
Hata
hivyo, Mbunge wa Tanzania, Makongoro Nyerere hakuungana na wenzake kugoma kwani
alibakia ukumbini na kuungana na wabunge 32 wa Burundi, Kenya, Uganda na
Rwanda.
Awali,
Mbunge Abdullah Ali Hassan Mwinyi alitoa msimamo wa wabunge wa Tanzania kuwa
walitoka, kupinga kitendo cha wabunge wengine kudharau kiti cha Spika juzi na
kutoka nje ili kushinikiza hoja yao.
Mwinyi
alisema ili kushinikiza kuheshimiwa kiti cha Spika, wameamua kutoka nje ya
ukumbi huo kwa kuonyesha hawaungi mkono, tabia ya baadhi ya wabunge kushinikiza
hoja zao, kujadiliwa na Bunge hata kwa kukiuka kanuni na taratibu.
“Jana(juzi)
ilikuwa ni mara ya pili wenzetu, kudharau kiti cha Spika na kutaka kutoa hoja
na kujadiliwa bila kufuata kanuni, sasa tumeona ni vizuri na sisi kwa kupinga
kuvunjwa kanuni, tutoke ili kuonyesha tunapinga mchezo huu,” alisema Mwinyi.
Mwinyi
alisema kitendo cha wabunge wenzao kutoka nje ya ukumbi kwa kukataliwa kuvunja
taratibu, kinadhalilisha kiti cha Spika na hata wabunge wenyewe.
Mbunge
mwingine wa Tanzania, Twaha Taslima alisema kanuni zipo wazi kuwa kama mbunge
ana hoja na kutaka Bunge lijadili mambo ambayo si ya dharura ni lazima
aiwasilishe saa 24 kabla kwa Spika.
“Sasa
jana(juzi), Mbunge wa Kenya, Peter Mathuki alitaka hoja yake ya kutaka
utaratibu wa kufanyika bunge kwa mzunguko ijadiliwe kitu ambacho hakikuwa
sahihi,” alisema Taslima.
Muthuki,
juzi aliungwa mkono na nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC), isipokuwa Tanzania.
Jana
aliwasilisha hoja hiyo kwa kufuata utaratibu lakini haikujadiliwa baada ya
wabunge wa Tanzania kutoka nje.
Katika
hoja hiyo, msimamo wa wabunge wa Tanzania na Kamati ya Uongozi ya Bunge ni kuwa
vikao vyote vifanyike katika ukumbi wa Bunge, Arusha baada ya kukamilika.
Wabunge
wa Tanzania ambao jana walitoka ni Shyrose Bhanji, Profesa Nderakindo Kessy na
Taslima. Wabunge wanne hawakuwapo.
Kwa
mujibu wa kanuni za Bunge hilo, kama wabunge watatu wa nchi moja, wakitoka nje
kupinga jambo lolote basi kikao kinaahirishwa kwa dakika 15 na wasiporejea
bunge linaahirishwa.
Akizungumzia
mgogoro huo, Ofisa Habari wa EALA, Bobi Odiko alisema kilichotokea jana si
ukiukwaji wa taratibu na kuongeza kuwa ana imani mambo yatakuwa sawa na vikao
vitaendelea leo kwa amani.
No comments:
Post a Comment