RAIS
Jakaya Kikwete amesema Serikali ya Tanzania iko tayari kukabiliana na mtu
yeyote atakayejaribu kuichezea au kuichokoza kwa namna yoyote ile, ikiwamo
kumega ardhi yake, itamfundisha kama ilivyomfundisha aliyekuwa Rais wa Uganda,
Idd Amin Dada, katika Vita ya Kagera.
Kikwete
alisema serikali ilimshikisha adabu Amin alipojaribu kumega sehemu ya ardhi ya
Tanzania, hivyo haitosita kufanya hivyo tena kwa asiye na nia njema na
Tanzania.
Kiongozi
huyo mkuu wa nchi alitoa onyo hilo jana wakati akizungumza na wananchi katika
maadhimisho ya Siku ya Mashujaa yaliyofanyika kitaifa katika makaburi yaliyopo
Kambi ya Kaboya, wilayani Muleba, mkoani Kagera.
Rais
Kikwete alisema serikali iko tayari kukabiliana na kupambana kwa nguvu yoyote
ile bila kuogopa mtu anayejaribu kuichezea nchi ya Tanzania kwa lengo la
kukwaza amani na utulivu uliopo hivi sasa.
“Laleni
usingizi salama. Msisikilize maneno ya mitaani, kwa sababu jeshi letu liko
imara kabisa kulinda nchi yetu na mipaka yake. Yeyote atakayejaribu kuivamia
ama kuichokoza nchi yetu atakiona cha mtema kuni. Nchi iko salama na jeshi liko
imara kulinda nchi yetu.
“Ujumbe
wetu mkubwa wa leo ni kwamba tuko tayari wakati wote na saa yoyote kuilinda
nchi yetu na mipaka yake. Hatuna nchi nyingine. Hivyo, kamwe hatuwezi kumruhusu
yeyote kuichezea nchi yetu, ama kuichezea ama kuimega nchi hii. Kama
tulivyoshughulika na Amin naye tutashughulika naye vivyo hivyo,” alisema.
Rais
Kikwete alisema shughuli ya kulinda amani ni ghali. “Na moja ya gharama hizo ni
makaburi haya ya ndugu zetu ambao wamelala hapa baada ya kupoteza maisha yao
katika vita dhidi ya nduli Idi Amin. Tutaendelea kuwaenzi kwa sababu hawa
walijitolea maisha yao kulinda mipaka ya nchi yetu, kulinda amani ya nchi yetu
na usalama wake na wetu sote,” alisema Kikwete.
Kiasi
cha askari 619 waliopoteza maisha yao wamelazwa kwenye makaburi hayo ya Kaboya.
Rais
Kikwete amesema kuwa serikali yake kwa ushauri wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania
inaangalia jinsi gani ya kuwahudumia vizuri zaidi askari wa Tanzania ambao
walipata vilema katika vita hiyo na bado wanaendelea kuishi.
“Nimesikia
kuna malalamiko kuhusu ubora wa jinsi tunavyowahudumia, hivyo tutazungumza na
Jeshi kuhusu njia bora zaidi ya jinsi ya kuwahudumia. Hawa ni mashujaa wetu, ni
watu waliojitolea maisha yao kuweza kulinda uhuru wetu. Tunaendelea kuwashukuru
na kuwaenzi. Hii ndiyo sababu sherehe za leo ni sherehe kubwa kwa nchi yetu,”
alisema.
Rais
Kikwete alishuhudia sherehe za kumbukumbu hizo ambapo miongoni mwa mambo
mengine, ametembelea makaburi ya askari wa Tanzania waliopoteza maisha yao
wakati wa kuikomboa nchi kutokana na uvamizi wa Amin wa Uganda na kuona silaha
zilizotumika katika vita hiyo mwaka 1978/79.
Naye
Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania ( JWTZ ), Davis Mwamunyange, alisema
jeshi lake liko makini na lina uwezo mkubwa wa kupambana dhidi ya wale
wanaotaka kuivunja amani iliyopo.
Alisema
uwepo wa amani na utulivu nchini umechangia watu washiriki kikamilifu kwenye
shughuli za maendeleo pasipo kuhofia chochote, hivyo anayetaka kuivuruga JWTZ
haitamuachia wala kumuonea huruma.
Mwamunyange
alisema JWTZ wako mstari wa mbele kuwalinda na kuwatetea kwa hali na mali
wananchi wa Tanzania ili kuhakikisha wanakuwa katika hali ya utulivu na amani.
Naye
Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Mehtodius Kilaini, alisema ni
wajibu wa viongozi wa dini na serikali kutambua wajibu wao katika kutenda haki
na kutetea wananchi.
Askofu
Kilaini alisema hayo wakati akiongoza sala ya kuwaombea mashujaa 619 waliouawa
katika vita ya Kagera kati ya mwaka 1978 na 1979 wakitetea taifa lao.
Alisema
ushindi wa nchi unatokana na umoja, mshikamano na uvumilivu baina ya viongozi
na wananchi wanaoungana kutetea masilahi ya taifa lao kutoka kwa adui.
Aliongeza
kuwa ili nchi iendelee pamoja na kustawi vizuri kwa jamii yake, amani ni msingi
mkubwa unaopaswa kuzingatiwa.
Askofu
Kilaini aliwataka viongozi wa dini na serikali kuhubiri amani pamoja na
kutekeleza wajibu wa majukumu yao kwa wakati na kufuata utaratibu ulio sahihi
kwa wananchi wake.