To Chat with me click here

Tuesday, June 4, 2013

MADHARA YA PROPAGANDA CHAFU ZA UDINI UCHAGUZI MKUU MWAKA 2010



Dar es Salaam,Tanzania

Rais wa Tanzania, Ndg. Jakaya Mrisho Kikwete.
SAKATA la Video inayodaiwa kuwa ilitoboa siri ya Rais Kikwete kutinga Ikulu kwa msaada wa kura za Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba, imeendelea kukigawa chama hicho baada ya Naibu Katibu Mkuu Chama hicho Tanzania Bara, Julius Mtatiro kukataa kuzungumzia video hiyo, alikataa katakata na kuwashauri waandishi wawasiliane na Profesa Lipumba amabye pia aliwahi kukataa kuzungumzia video hiyo.

Itakumbukwa kuwa kumekuwepo tuhuma dhidi ya Rais Kikwete na CCM kuwa mwaka 2010 waliendesha propaganda chafu za udini zenye lengo la kuwagawa Watanzania hususan Wakristo na Waislamu kwa manufaa yao ya kisiasa.

Mwelekeo huo wa kisiasa wa Rais Kikwete na CCM unadaiwa kutokana na hatua ya viongozi wa Kanisa Katoliki nchini kupitia Idara ya Uchungaji kutoa waraka maalumu uliowataka Watanzania kuchagua viongozi waadilifu.

Waraka huo haukuifurahisha CCM, ambayo imekuwa inagubikwa na tuhuma nyingi za ufisadi. Makada na viongozi wa CCM walijaribu kuupinga kwa kuupotosha, wakisema unaingiza mambo ya dini katika siasa.

Kanisa Katoliki lina utaratibu wa muda mrefu wa kutoka nyaraka kuelekeza waamini na wananchi juu ya mambo ya msingi katika jamii.

Katika hali hiyo, Rais Kikwete na CCM wanadaiwa kukimbilia kwa viongozi wa Kiislamu na kuwaomba wawaunge mkono kwa kuwajaza maneno ya uongo, kwamba Wakatoliki walikuwa wamewaagiza waumini wao kupigia kura wagombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Inadaiwa waliwafitinisha zaidi kwa kuwaeleza kuwa aliyekuwa mgombea kiti cha rais wa CHADEMA katika uchaguzi huo, Dk. Willibrod Slaa ambaye ameshawahi kuwa Padri, alikuwa ametumwa na Kanisa Katoliki ili kuendeleza utawala wa Kikristo nchini.

Propaganda hizo hazikuishia kwa viongozi na waumini wa Kiislamu tu, bali zilielekezwa pia kwa viongozi na wafuasi wa CUF ambao walirubuniwa na kushawishiwa kumpigia kura “Muislamu mwenzao” Rais Kikwete, huku wakiahidiwa kuwa mwaka 2015 Waislamu wa CCM nao watampigia kura mgombea wa CUF kwa hoja kuwa CCM watakuwa wamesimamisha mgombea Mkristo. Licha ya madai hayo ya udini kuwa wazi kwa muda mrefu, lakini wakati wote Rais Kikwete na CCM wamekuwa wakikanusha tuhuma hizo na kuziita kuwa uongo na uzushi.

No comments:

Post a Comment