Mwenyekiti wa Tume ya mabadiliko ya katiba Jaji Warioba. |
SIKU
moja baada ya Ikulu ya Rais Jakaya Kikwete kutoa taarifa ya kejeli na kumsuta
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, mwenyekiti huyo naye ameibuka
kujibu mapigo.
Katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Jaji Warioba alisema ameiona taarifa
ya serikali kuhusu Tume ya Mabadiliko ya Katiba, lakini ameshangazwa na maudhui
na lugha iliyotumiwa na Ikulu dhidi yake.
Majibu
ya Jaji Warioba kwa Ikulu ya Rais Kikwete, yalitokana na taarifa ya Kurugenzi
ya Mawasiliano Ikulu, ambayo ilimwita Jaji Warioba mnafiki kwa kujifanya
hajui ukomo wa tume yake.
Ikulu
ilitoa taarifa hiyo baada ya gazeti moja juzi kumkariri Jaji Warioba akidai
kuwa tume yake ilifukuzwa kazi na kwamba haikupewa muda wa kuandaa na
kuwasilisha nyaraka za kukabidhi ofisi na madaraka na kwamba wajumbe wa tume
hiyo waliporwa magari ambayo yamewekwa Ikulu.
Akitoa
ufafanuzi wa taarifa ya Ikulu ya juzi, katika taarifa hiyo, Warioba alifafanua
hivi:
“Kwanza,
tume iliwaheshimu sana waheshimiwa marais
wetu. Mafanikio ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba yametokana na jinsi Mheshimiwa
Rais wa Jamhuri na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar walivyoiunga mkono na kuisaidia
tume. Milango yao ilikuwa wazi wakati wote. Wakati wowote mimi kama mwenyekiti
nilipoomba kuonana nao nilipata nafasi haraka na tume ilipoomba chochote,
pamoja na kuongezewa muda hawakusita. Na wakati wote hawakutoa shinikizo la
aina yoyote. Makatibu wakuu viongozi nao waliisaidia tume kwa kiwango
hicho. Heshima yangu na wenzangu kwa waheshimiwa marais na makatibu wakuu
viongozi ni kubwa.
“Pili,
tume ilikuwa haijamaliza kazi yake wakati inakabidhi ripoti kwa Mheshimiwa
Rais. Tume iliendelea na kazi ya kuandaa Randama ya Rasimu, Bango Kitita
la Rasimu na maelezo niliyotoa kwenye Bunge Maalumu. Serikali ilijua tulikuwa
tunafanya kazi hiyo na nyaraka hizo zilikabidhiwa bungeni siku ya kuwasilisha
Rasimu.
“Tatu, wajumbe wa tume
hawajatoa madai ya kulipwa shilingi milioni mia mbili. Hakuna mjumbe yeyote aliyetoa dai
kama hilo na serikali inajua,” alisema Jaji Warioba.
Alisema
alichozungumza ni muda wa kuandaa makabidhiano na kuandaa safari ya wajumbe kurudi
makwao. Alisema aliwasilisha rasimu Machi 18, 2014, tume ilivunjwa Machi 19,
2014 wakati wajumbe wako Dodoma.
“Pamoja
na lugha ya kejeli iliyotumiwa na serikali na kuniita mnafiki, busara ya
kawaida ingeonyesha umuhimu wa serikali kujipa muda wa kufanya maandalizi ya
kuwarudisha wajumbe nyumbani. Hata kama sheria ilitaja muda wa kuvunja
tume bado ilikuwa ni wajibu serikali kufanya mipango ya safari ya wajumbe baada
ya kumaliza kazi. Sheria haikuizuia serikali kufanya hilo. Huo ni wajibu wa
serikali na utaratibu wa kawaida unaotumiwa na serikali kwa tume zote
inazoziunda,” alisema.
Jaji
Warioba alimalizia taarifa yake kwa kusema inaonekana Tume ya Mabadiliko ya
Katiba iliwekewa utaratibu tofauti na tume nyingine zilizopita na kuhoji
kulikoni?
Katika
taarifa yake juzi, Ikulu ilisema kuwa muda wa mwisho wa uhai wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba ulijulikana, hivyo mtu kujitia kwamba ameisahau siku
hiyo ni mnafiki wa hali ya juu.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo, moja ya mijadala mikali ya awali kuhusiana na mchakato
wa Katiba Mpya ulihusu lini Tume ya Mabadiliko ya Katiba imalize muda wake.
Ilisema
wengine walitaka tume imalize muda wake baada ya kukabidhi Ripoti ya Tume na
Rasimu ya Katiba, wengine wakitaka tume baada ya Mwenyekiti wake, Jaji Warioba,
kuwasilisha rasimu yake bungeni na hata wengine wakitaka wajumbe wa tume wawe
sehemu ya Bunge Maalumu la Katiba.
“Hatimaye,
ilikubaliwa kuwa shughuli za tume zingefikia ukomo wake baada ya Mwenyekiti
wake kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalumu la Katiba kama
inavyoelekezwa katika kifungu cha 31 (1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
“Kifungu
hicho kinasema kuwa baada ya kuwasilishwa kwa Rasimu ya Katiba kwenye Bunge
Maalumu chini ya Kifungu cha 20(3) (cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba) Rais,
kwa amri itakayochapishwa katika Gazeti la Serikali, atavunja tume.
“Mheshimiwa
Warioba aliwasilisha Rasimu ya Katiba katika Bunge Maalumu la Katiba Jumanne ya
Machi 18, mwaka huu, 2014 na siku iliyofuata Jumatano, Machi 19, 2014 na kwa
mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Rais alitia saini tangazo la Serikali
la Kuvunja Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Hivyo,
tokea mwanzo wa mchakato mzima wa Katiba Mpya na utendaji kazi wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba hapakupata kuwepo, hata wakati mmoja, shaka kuhusu siku ya
tume hiyo kumaliza kazi zake.
“Mwenyekiti
wa Tume, wajumbe wote wa Tume, Sekretarieti ya Tume na Watanzania wote waliijua
fika siku ya mwisho ya Tume kukamilisha shughuli zake. Kwa mtu kujitia
ameisahau siku hiyo leo ni kiwango cha juu sana cha unafiki,” alisema Salva
Rweyemamu.
Kuhusu
wajumbe kutakiwa kurudisha magari,
Ikulu ilikiri kuwa kweli wajumbe wa tume walitakiwa kurudisha
Ikulu magari ambayo walikuwa wanatumia kikazi kwa sababu kazi ya tume ilikuwa
imemalizika.
Pili,
alisema tume ilijua toka mwanzo kuwa baada ya kumaliza kazi yao, magari ambayo
walikuwa wanatumia wajumbe na maofisa wa tume hiyo yalikuwa yanatakiwa kupelekwa
Dodoma kwa matumizi ya shughuli za Bunge Maalumu la Katiba ambalo linakabiliwa
na shida kubwa ya usafiri.
“Serikali
ilichukua uamuzi kuwa magari hayo yapelekwe Dodoma kwa sababu lisingekuwa jambo
la busara kwa serikali kutumia fedha za umma kununua magari mengine mapya
wakati yale ya tume bado yanafaa kufanya kazi na wala hakuna bajeti ya kufanya
manunuzi ya magari mapya.
“Hivyo,
ni kweli magari hayo yako Ikulu, Dar es Salaam, yakisubiri kukamilika kwa
taratibu za kuyapeleka Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma,” ilisema Ikulu.
Kuhusu
madai kwamba tume haikupata muda wa kukabidhi ofisi na nyaraka, Ikulu ilisema
hili nalo ni jambo la kutunga na kuzusha tu.
Alisema
Jaji Warioba alikabidhi rasmi Ripoti ya Tume na Rasimu ya Katiba kwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa
Zanzibar Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein, Desemba 30, 2014, mbele ya wananchi
katika viwanja vya Ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam.
“Hivyo,
toka siku hiyo, Tume haikuwa tena na kazi ya kuandaa Ripoti ama Rasimu kwa
sababu kazi hiyo ilikuwa imekwisha na wala isingeweza kuibadili tena Rasimu ya
Katiba.
“Kwa
maana hiyo, toka Desemba 30, mwaka jana, kupitia miezi ya Januari, Februari
mpaka Machi 18, mwaka huu, Sekretariati ilikuwa na muda wa siku 77, zaidi ya
miezi miwili na nusu, kufanya maandalizi ya kukabidhi nyaraka na ofisi kwa
sababu ilijua kazi yake ilikuwa inamalizika siku ambayo Mwenyekiti wa Tume hiyo
angewasilisha Rasimu ya Katiba katika Bunge Maalumu la Katiba.
“Sasa
katika muda wote huo, Sekretarieti ya Tume ilikuwa inafanya nini badala ya
kuandaa ripoti ya makabidhiano na wakati maofisa wake walikuwa wanaendelea
kulipwa mshahara na serikali? Kwa nini walalamike hadharani leo kwa jambo
ambalo lilikuwa ni la wajibu wao na wakashindwa kulifanya kwa wakati?” alihoji
Salva.
Ikulu
katika taarifa hiyo, pia ilijibu madai kwamba wajumbe wa tume walitakiwa
kulipwa kiinua mgongo cha sh milioni 200 kila mjumbe.
Alisema
hakuna shaka kuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wamefanya kazi nzuri
sana na wanastahili pongezi nyingi za wananchi.
Lakini
kama wanadhani kuwa serikali ina uwezo wa kumlipa kila mjumbe kiinua mgongo cha
sh milioni 200, basi wanajidanganya kwani wananchi wa Tanzania hawawezi kuelewa
maana kabisa ya malipo hayo makubwa kupindukia.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment