To Chat with me click here

Tuesday, October 22, 2013

UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA UFANYIKE 2015


Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba  

Jana  gazeti la Mwananchi lilichapisha habari katika ukurasa wa kwanza ikisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeomba kuongezewa muda wa mwezi mmoja kutokana na ugumu wa kazi ya uchambuzi wa maoni yaliyotolewa na wananchi na asasi mbalimbali. Kama mambo yangekwenda kama ilivyotarajiwa hapo awali, Tume hiyo iliyoanza kazi Mei 1 mwaka jana, chini ya Jaji Joseph Warioba ingekamilisha kazi yake Novemba 1, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Sura ya 83 ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Tume hiyo ilitakiwa kufanya kazi kwa miezi 18. Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Augustino Ramadhan alisema juzi kwamba wamepeleka serikalini ombi la kuongezewa muda wa kufanya kazi kutokana na kukabiliwa na kazi ya ziada ya kuchambua maoni hayo. Pamoja na Serikali kukiri kupokea ombi hilo, hadi tunakwenda mitamboni jana ilikuwa haijatoa jibu la kulikubali wala kulikataa.

Sisi hatuoni sababu yoyote inayoweza kuisukuma Serikali kulikataa ombi hilo, hasa kutokana na kujitokeza kwa mambo mengi ambayo hayakutarajiwa kabla na wakati wa mchakato wa Katiba Mpya. Mikutano ya Mabaraza ya Katiba iliyofanyika nchi nzima, kwa mfano ilizua tafrani kubwa ambapo wajumbe wa mabaraza hayo waligawanyika kwa misingi ya kisiasa na kiitikadi. Tume hiyo ililazimika kutumia muda mwingi kujielekeza katika kutoa tafsiri na kufafanua vifungu katika Rasimu ya Kwanza ya Katiba. Pia Tume ilitumia muda mrefu kuratibu mijadala ya Rasimu hiyo, kwani wajumbe wengi wa mabaraza hayo walikuwa wakijadili hoja zilizotokana na misimamo ya vyama vyao badala ya kujadili rasimu yenyewe.

Hivyo, Serikali haina budi kukubali ombi hilo la tume haraka iwezekanavyo, pamoja na ukweli kwamba kuiongezea tume mwezi mmoja kuchambua maoni ya wananchi na asasi mbalimbali ni kuongeza gharama za mchakato huo. Lakini, wahenga waliposema maji ukiyavulia nguo ni sharti uyaoge, walipatia kabisa usemi huo, kwani kama tumeamua kama taifa kupata Katiba Mpya itakayotuvusha miaka 50 mingine ijayo lazima tubebe gharama hizo za kutuletea demokrasia ya kweli.

Ni vyema tukatambua kwamba hatua ya tume ya kuomba kuongezewa mwezi mmoja siyo ya ajabu. Sheria inaipa tume hiyo fursa ya kuongezewa miezi miwili nje ya muda uliowekwa. Kinachotakiwa sasa ni Serikali kujipanga vizuri na kutekeleza mambo mbalimbali kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2015. Mambo hayo ni pamoja na kuandaa, kurekebisha na kupitisha sheria mbalimbali kwa lengo la kuondoa sheria kandamizi na kuweka sheria zitakazowezesha kuwapo mazingira linganifu ya ushindani wa kisiasa. Kwa mfano, inahitajika sheria mpya ya Tume Huru ya Uchaguzi.

Moja ya mambo muhimu ambayo Serikali inapata kigugumizi kuyatolea uamuzi ni suala la kufanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa sambamba na Uchaguzi Mkuu wa 2015. Muda uliobaki kati ya sasa na 2014 (ambao ulipangwa kufanyika) hautoshi kufanya maandalizi na uchaguzi ulio huru na haki. Uchaguzi huo ni vyema usimamiwe na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. Hivyo, Tamisemi iliyokuwa ikisimamia chaguzi za Serikali za Mitaa na kusababisha malalamiko mengi kutoka kwa wananchi itakuwa imeondolewa mzigo huo mzito. Kufanya uchaguzi huo wakati mmoja na Uchaguzi Mkuu kutapunguza gharama kwa kiasi kikubwa kama ilivyo katika nchi nyingi barani Afrika na kwingineko.

No comments:

Post a Comment