To Chat with me click here

Thursday, August 29, 2013

ZAIDI YA WATU 40 WAFARIKI KWENYE AJALI KENYA



Ajali ya barabarani Kenya
Takriban watu 41 wanadaiwa kuuawa baada ya basi moja la abiria lililokuwa likitoka Nairobi kuelekea Homabay Magharibi mwa Kenya kuanguka na kubingirikia mara kadhaa katika eneo la Narok.

Polisi wamethibitisha kuwa miongoni mwa waliouawa ni watoto wanne. Mkuu wa polisi wilayani Narok Patterson Maelo amesema kuwa dereva wa basi hilo alishindwa kulithibiti katika eneo la kona na hivyo basi hilo kupoteza mwelekeo na kuanguka.
 
Maafisa wa shirika la msalaba mwekundi ambao tayari wamefika katika eneo la tukio hilo wamesema kuwa watu wengine 33 waliojeruhiwa wamesafirishwa hadi hospitali ya wilaya ya Narok kwa matibabu.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ni miongoni wa viongozi waliotuma risala zao za rambi rambi kwa jamaa na marafiki wa abiria waliouawa.

Katika ripoti iliyochapishwa katika mtandao wake wa twitter, Rais Kenyatta ametoa amri kwa idara ya polisi kuchukua hatua dhidi ya wamiliki wa magari ya umma wanaokiuka sheria za barabarani.

MTOTO WA MIAKA 6 ANG'OLEWA MACHO UCHINA!



Mtoto aliyeng'olewa macho nchini Uchina
Polisi nchini Uchina imetangaza kuwa itatoa zawadi kwa yeyote atakayetoa habari zitakazowasaidia kumkamata mama mmoja ambaye anashukiwa kumng'oa macho mvulana mwenye umri wa miaka sita.

Shambulio hilo linasemekana kutokea tarehe 24 mwezi huu katika eneo na Fenxi, iliyoko katika mkoa wa Shanxi.

Mvulana huyo anasemekana alikwenda kucheza na watoto wengine lakini wazazi wake walimpata baadaye huku macho yake yote yakiwa yamengolewa huku akivuja damu. Mvulana huyo kwa sasa anaendelea kupata matibabu hospitalini.
 
Idara ya polisi nchini humo imetoa zawadi ya zaidi ya dola elfu kumi na sita kwa yeyote atakayetoa habari, kuhusu aliyehusika na shambulio hilo.

Wazazi wa mtoto huyo wanasemekana kuwa wakulima. Mamake amesema mtoto huyo aliwaambia kuwa wakati alipokuwa akitembea alishambuliwa na mama mmoja ambaye hakumfahamu. 
 
Polisi walipata macho ya mvulana huyo karibu na eneo la tuko. Uchunguzi wa awali umebainisha kuwa sehemu ya mboni au Cornea kwa Kiingereza ilikuwa imengolewa, na hivyo kuashiria ulanguzi wa viungo vya kinadamu. Hata hivyo polisi wanasema hawajatambua chanzo cha shambulio hilo.

TOA MAONI YAKO

MWANAJESHI WA UN AUAWA NA WAASI (M23) DRC



Umoja wa Mataifa umesema kuwa mwanajeshi wake mmoja wa kutunza amani ameuawa na wengine watatu kujeruhiwa kufuatia mapigano makali kati ya na wapiganaji wa waasi Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Wanajeshi wa serikali ya Congo
Msemaji wa Umoja wa Mataifa mjini New York, Farhan Haq, hata hivyo hajatangaza uraia wa wanajeshi waliouawa au kujeruhiwa.

Wanajeshi hao wa Umoja wa Mataifa walitumia ndege za helicopta kuwasukuma nyuma wapiganaji wa M23 karibu na mji wa Goma, ambao ndio mji mkubwa zaidi katika eneo hilo la Mashariki. Watu themanini waliuawa kwenye mapigano hayo wiki iliyopita.
 
Mwaka wa 2012, waasi wa M23 waliuteka mji huo kwa muda kabla ya kuondoka kufuatia shinikizo kutoka kwa jamii ya kimataifa. Umoja wa Mataifa Umetuma kikosi maalum katika eneo hilo lenya utajiri mkubwa wa madini kukabiliana na waasi hao.
 
Wanajeshi hao wa Umoja wa Mataifa MONUSCO, wanapambana na wapiganaji hao wa waasi kwa ushirikiano na wanajeshi wa serikali. Jeshi hilo la Monusco limelazimika kufanya mashambulio ya anga na ardhini ili kuzuia waasi hao wa M23 kukaribia Goma na ripoti zinasema mapigano makali yanaendelea katika maeneo ya milima ya Kibati, takriban kilomita kumi na tano Kaskazini mwa Goma.
 
Watu wapatao laki mbili wanasemekana kuishi katika eneo hilo la Kibati. Wapiganaji wa M23 wamesema kuwa wanajeshi wa Congo na wenzao wa Umoja wa Mataifa walifanya mashambulio ya anga na ardhini katika maeneo wanayoyadhibiti, Kaskazini mwa Goma.
 
Daktari mmoja mjini Goma, Isaac Warwanamiza, ameliambia shirika la habari la AP kuwa aliona miili ya watu themanini na wawili, ishirini na tatu zikiwa za wanajeshi wa serikali. Umoja wa Mataifa una zaidi wanajeshi elfu kumi na nane nchini Congo.

WATOTO WA KITANZANIA WAKABILIWA NA 'HATARI KUBWA' KWENYE MIGODI YA DHAHABU, YASEMA HUMAN RIGHTS WATCH




Maelfu ya watoto wakiwa na umri wa hadi miaka minane wanafanya kazi kwenye migodi midogo midogo nchini Tanzania wakiwa wanakabiliwa na kitisho kikubwa kwa afya na maisha yao, lilisema shirika la Human Rights Watch (HRW) katika ripoti yake iliyotolewa siku ya Jumatano (tarehe 28 Agosti).

"[Watoto hao] wanachimba na kutoboa chini kabisa, wanabanja mawe, wanafanya kazi chini ya ardhi kwa zamu ya hadi masaa 24, na wanasafirisha na kubeba mifuko mizito ya dhahabu ghafi," ilisema HRW. "Watoto wanakabiliwa na hatari ya kujeruhiwa kwa miamba inapopasuka na ajali za vifaa, na pia madhara ya muda mrefu ya kiafya kutokana na kutumia madini ya zebaki, kuvuta vumbi na kubeba mizigo mizito."

Kundi hilo la haki za binadamu linasema watoto wengi wanaofanya kazi kwenye migodi ama ni mayatima au watoto wengine walio kwenye mazingira hatari ambao wanakosa mahitaji ya lazima na msaada. Wasichana wanaoishi karibu na maeneo ya machimbo pia wanakabiliwa na unyanyasaji wa kingono na shinikizo la kuwa makahaba, HRW iligundua.

"Wavulana na wasichana wa Kitanzania wanamiminika kwenye migodi ya dhahabu kwa matumaini ya maisha bora, lakini wanajikuta wamenaswa kwenye mduara mbaya wa hatari na fadhaa," alisema Janine Morna, mtafiti mwenza wa haki za watoto kwenye HRW. "Tanzania na wafadhili wanapaswa kuwaondoa watoto hawa kwenye migodi na kuwapeleka skuli au vyuo vya mafunzo ya amali."

"Kuwaandikisha watoto kazi hatari za uchimbaji madini ni moja ya aina mbaya kabisa za ajira za watoto chini ya makubaliano ya kimataifa, ambayo Tanzania ni sehemu yake," ilisema HRW.

Tanzania ni ya tatu barani Afrika kwa uzalishaji wa dhahabu na madini hayo ya thamani ni chanzo kikuu cha fedha za kigeni kwa nchi hiyo, ambapo usafirishaji wake nje ya nchi kwa miezi sita ya kwanza ya mwaka 2013 ulifikia dola bilioni 1.8, kwa mujibu wa benki kuu.

Human Rights Watch yenye makao yake makuu nchini Marekani ilifanya utafiti wake ndani ya mwezi Oktoba na Disemba 2012 kwenye maeneo ya migodi kaskazini magharibi na kusini mwa Tanzania, na katika miji ya Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya. Watafiti walitembelea maeneo 11 ya uchimbaji madini kwa ajili ya ripoti hii.

BUNGE LA EALA LAKWAMA BAADA YA WABUNGE KUSUSIA KIKAO!


Wabunge wa Tanzania kwenye bunge la Afrika Mashariki(EALA) wakitoka ndani ya ukumbi wa bunge hilo jana kupinga wabunge wenzao wanaoshinikiza hoja zao kwa kutoka kwenye vikao vya bunge. Kutoka kushoto ni Mh.Twaha Taslima, Mh.Shyrose Bhanji,Mh.Abdullah Mwinyi na Mhe Nderakindo Kessy
Chemba ya Bunge la Afrika Mashariki inavyoonekana wakati kikao kikiendelea

 Arusha. Kikao cha Bunge la Afrika Mashariki (EALA), jana kilivunjika kwa mara ya pili baada ya Wabunge wa Tanzania, kutoka ndani ya ukumbi wakipinga kanuni kuvunjwa juzi.

Baada ya wabunge wa Tanzania kutoka nje, Spika wa Bunge hilo, Margareth Zziwa aliahirisha Bunge kwa dakika 15 ili kuweka mambo sawa, lakini jitihada za kuwashawishi ziligonga mwamba na kuamua kuahirisha Bunge hadi leo.

Hata hivyo, Mbunge wa Tanzania, Makongoro Nyerere hakuungana na wenzake kugoma kwani alibakia ukumbini na kuungana na wabunge 32 wa Burundi, Kenya, Uganda na Rwanda.

Awali, Mbunge Abdullah Ali Hassan Mwinyi alitoa msimamo wa wabunge wa Tanzania kuwa walitoka, kupinga kitendo cha wabunge wengine kudharau kiti cha Spika juzi na kutoka nje ili kushinikiza hoja yao.

Mwinyi alisema ili kushinikiza kuheshimiwa kiti cha Spika, wameamua kutoka nje ya ukumbi huo kwa kuonyesha hawaungi mkono, tabia ya baadhi ya wabunge kushinikiza hoja zao, kujadiliwa na Bunge hata kwa kukiuka kanuni na taratibu.

“Jana(juzi) ilikuwa ni mara ya pili wenzetu, kudharau kiti cha Spika na kutaka kutoa hoja na kujadiliwa bila kufuata kanuni, sasa tumeona ni vizuri na sisi kwa kupinga kuvunjwa kanuni, tutoke ili kuonyesha tunapinga mchezo huu,” alisema Mwinyi.

Mwinyi alisema kitendo cha wabunge wenzao kutoka nje ya ukumbi kwa kukataliwa kuvunja taratibu, kinadhalilisha kiti cha Spika na hata wabunge wenyewe.

Mbunge mwingine wa Tanzania, Twaha Taslima alisema kanuni zipo wazi kuwa kama mbunge ana hoja na kutaka Bunge lijadili mambo ambayo si ya dharura ni lazima aiwasilishe saa 24 kabla kwa Spika.

“Sasa jana(juzi), Mbunge wa Kenya, Peter Mathuki alitaka hoja yake ya kutaka utaratibu wa kufanyika bunge kwa mzunguko ijadiliwe kitu ambacho hakikuwa sahihi,” alisema Taslima.

Muthuki, juzi aliungwa mkono na nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), isipokuwa Tanzania.

Jana aliwasilisha hoja hiyo kwa kufuata utaratibu lakini haikujadiliwa baada ya wabunge wa Tanzania kutoka nje.

Katika hoja hiyo, msimamo wa wabunge wa Tanzania na Kamati ya Uongozi ya Bunge ni kuwa vikao vyote vifanyike katika ukumbi wa Bunge, Arusha baada ya kukamilika.

Wabunge wa Tanzania ambao jana walitoka ni Shyrose Bhanji, Profesa Nderakindo Kessy na Taslima. Wabunge wanne hawakuwapo.

Kwa mujibu wa kanuni za Bunge hilo, kama wabunge watatu wa nchi moja, wakitoka nje kupinga jambo lolote basi kikao kinaahirishwa kwa dakika 15 na wasiporejea bunge linaahirishwa.

Akizungumzia mgogoro huo, Ofisa Habari wa EALA, Bobi Odiko alisema kilichotokea jana si ukiukwaji wa taratibu na kuongeza kuwa ana imani mambo yatakuwa sawa na vikao vitaendelea leo kwa amani.