BABA wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere,
alimaliza siku zake za mwisho katika hali ya masikitiko kutokana na vitendo vya
mwisho vya watu aliowaamini sana.
Wakati Watanzania wakiadhimisha miaka
15 tangu kufariki kwa Mwalimu katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas jijini
London, Uingereza mwaka 1999, taarifa mpya zimeibuka kuhusu namna alivyotumia
siku zake za mwisho.
Katika mahojiano ambayo vyanzo vya
habari hii vilifanya na watu waliokuwa karibu naye ikiwamo familia yake na watu
aliokuwa akifanya nao kazi, mambo makubwa mawili yameelezwa kumuumiza Mwalimu.
Mambo hayo ni mchango mdogo wa serikali
za Tanzania na Afrika Kusini kwa taasisi yake ya Mfuko wa Mwalimu Nyerere (MNF)
na ubinafsishaji wa iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).
Mmoja wa viongozi wa MNF aliyezungumza
na vyanzo vyetu vya habari kwa masharti ya kutotajwa jina, alisema
Mwalimu alihuzunika sana wakati alipokwenda nchini Afrika Kusini kutafuta fedha
za taasisi hiyo na kuambulia mchango kidogo sana.
“Wakati Nelson Mandela akiwa Rais wa
Afrika Kusini, Mwalimu alikwenda kutafuta fedha kule akiwa na matumaini makubwa
sana. Unajua Tanzania ilijitolea sana kwa ajili ya Uhuru wa Afrika Kusini.
“Afrika Kusini ina uwezo mkubwa wa
kiuchumi. Mwalimu alitaraji makubwa sana kutokana na uhusiano baina ya nchi
hizi mbili. Cha ajabu, alipokwenda kule serikali ilimpa kiasi cha dola 60,000
(takribani shilingi milioni 60 wakati huo).
“Hebu fikiria uwezo wa kiuchumi wa
Afrika Kusini na mchango ambao Mwalimu na Tanzania kwa ujumla walikuwa nao kwa
Taifa hilo na halafu Mwalimu anapewa dola 60,000. Nyerere returned a broken man
(Nyerere alirudi akiwa amefadhaika sana),” alisema kiongozi huyo.
Kiongozi huyo alieleza pia kwamba kwa
upande wa Serikali ya Tanzania, msaada pekee ambao MNF iliupata ni kiwanja
kilichopo jirani na Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam kilichotolewa
wakati wa Serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi, na hawakuwahi kupokea fedha
yoyote kutoka serikalini hadi leo.
“Hebu fikiria, serikali yake mwenyewe
ya Tanzania haikumpa hata senti moja kwa ajili ya MNF. Serikali ya Rais
Benjamin Mkapa haikuwahi kumpa kitu na nafahamu serikali ya Jakaya Kikwete pia
haijawahi kuchangia MNF. Hilo ndiyo tatizo,” alisema kiongozi huyo.
Kutokana na hali hiyo, kiongozi huyo
alimnukuu Mwalimu Nyerere akisema mwaka mmoja kabla ya kifo chake; “Siku
nikifariki dunia, kesho yake tu MNF itakufa”.
Vyanzo vyetu vya habari vimeelezwa pia
namna wasaidizi wa karibu wa Mwalimu walivyoshangazwa na ukweli kuwa katika
kitabu cha Mandela cha The Long Walk to Freedom, Mwalimu alitajwa mara moja tu
kwenye kitabu hicho.
Katika kitabu hicho, Mandela alimtaja
Mwalimu wakati akieleza kuhusu harakati zake za kutafuta kuungwa mkono na nchi
za Afrika katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, ambapo alitembelea
Tanganyika huru kutafuta kuungwa mkono.
Wakati wa utawala wa Makaburu wa Afrika
Kusini, ilikuwa marufuku kutaja hadharani jina la Nyerere au Tanzania kwa vile
ilionekana kama ni uchochezi. Lakini pia Makaburu walitaka kuzuia ushawishi wa
Nyerere kwa watu Weusi wa kule. Ndiyo maana Mwalimu alitaraji makubwa sana
kutoka huko.
“Ni sawasawa na utawala wa Mkapa.
Watanzania wote wanafahamu kuwa isingekuwa Mwalimu, Mkapa huenda asingeupata
urais wa Tanzania. Alitaraji huyo ndiye angeisaidia MNF kuliko pengine rais
yeyote. Cha ajabu, serikali ya Mkapa haikuchangia kitu. Afadhali hata Mzee
Mwinyi ambaye alichangia kiwanja,” kilisema chanzo hicho cha habari hii.
Katika mahojiano mengine na aliyekuwa
Katibu Myeka wa Mwalimu, Samwel Kassori, ilibainika pia namna Mwalimu
alivyohuzunishwa na suala la kuuzwa kwa NBC kwa mojawapo ya makampuni kutoka
nchini Afrika Kusini.
“Lakini moja kubwa ninalokumbuka ni
kuhusu mchakato wa uuzwaji wa benki ya NBC mwaka 1997 mwezi Aprili wakati
wa utawala Mkapa ambapo Mwalimu aliwahi kulengwalengwa na machozi akipinga
benki hiyo kuuzwa kwa ABSA Group kutoka Afrika ya Kusini.
“Wakati huo nakumbuka serikali
ilipanga kumwandalia Mwalimu sherehe ya kitaifa ya siku yake ya kuzaliwa
(birthday) ya kutimiza miaka 75 ambazo zingefanyika katika ukumbi wa Diamond
Jubilee wa Jijini Dar es Salaam, na jambo hilo lilimshtua kidogo akaniagiza
nichunguze fedha hizo zingetoka wapi na kwanini afanyiwe sherehe kubwa kiasi
hicho na pia tetesi zilikuwa zimezagaa kuwa NBC inauzwa.
“Wakati huo Waziri wa Fedha alikuwa
Daniel Yona, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo alikuwa Peter Ngumbulu na Gavana wa
Benki Kuu (BoT) alikuwa Dk. Idris Rashid.
“Baada ya kupata taarifa za kwamba
benki hiyo iko mbioni kupigwa bei, Mwalimu aliomba maelezo kutoka kwa wahusika
ambao ni Waziri wa Fedha, Katibu Mkuu na Gavana wa BoT.
“Majibu ya serikali yalikuwa kwamba NBC
inauzwa kwa sababu taasisi za fedha za Kimataifa za Fedha (IMF) na Benki ya
Dunia (WB) ziliagiza Benki hiyo kuuzwa.
“Baada ya kupata maelezo hayo Mwalimu
alikasirika kweli kweli, akaniita na tukiwa nyumbani kwake Msasani aliniagiza
kumpigia simu Rais wa (WB) wakati ili azungume naye.
“Baada ya kumpata Rais huyo wa (WB)
ambaye bado alikuwa akimwita Mwalimu Mr. President (Mheshimiwa Rais), alikana
IFM pamoja na Benki ya Dunia kushinikiza au kutoa masharti kuuzwa kwa NBC.
“Namnukuu Rais huyo wa WB
aliniambia:”Mr Kasori do me a favour could you request President Nyerere to
come to our headquarters in Washington and read the documents from
Tanzania government, they are too voluminous but will try to make executive
summary of the same”
“Maana yake ni kwamba walitaka Mwalimu
akajioonee mwenyewe nyaraka zilizotumwa katika taasisi hizo za kimataifa kuhusu
uuzaji wa NBC na walisema wangelipa gharama zote muhimu za safari hiyo.
“Baada ya mazungumzo ya simu siku mbili
baadaye tulifunga safari na Mwalimu hadi Washington nchini Marekani ambapo
tulikutana na Rais wa WB kwa kikao cha siku nzima na kupitia nyaraka muhimu
zilizowasilishwa kwao na serikali ya Tanzania.
“Tulirudi nyumbani baada ya wiki moja
na Mwalimu aliniagiza kwanza niwatafute Yona, Ngumbulu na Dk. Rashid ili
azungumze nao kabla ya kukutana na Rais Mkapa.
“Basi baada ya mimi kufanya mawasiliano
nao wote hakuna aliyeitikia wito wa Mwalimu “walimpuuza” na badala yake
walimtuma Donald Kamori ambaye alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC.
“Nakumbuka vizuri kikao na Kamori kilifanyika
Msasani nyumbani kwa Mwalimu Nyerere, Aprili 13 mwaka huo 1997, na Kamori
alikuwa mtaalamu aliyebobea katika masuala ya fedha na ndiye kati ya wataalamu
wazawa walioanzisha BoT.
“Kamori akiwa na nyaraka na takwimu za
kitaalamu. Alimweleza Mwalimu bila ya kuficha kuwa kuiuza NBC serikali ilikuwa
inafanya makosa makubwa katika sekta ya fedha kwa kuwa Benki hiyo ilikuwa
inaendeshwa kwa faida kubwa. Uuzwaji wake ungeleta athari ya moja kwa serikali
pamoja na taasisi zake nyeti.
“Mwalimu alitikisa kichwa kwa
masikitiko makubwa, akasema ‘ooooh kweli nimesomesha Watanzania’ alikuwa
amevutiwa sana na maelezo ya kitaalamu ya Donald Kamori.
“Baada ya kupata maelezo ya kutosha
kutoka kwa Kamori, Mwalimu aliomba kukutana na Rais Mkapa na kikao kilifanyika
Ikulu ambapo alitetea NBC isiuzwe kwani ndiyo ilikuwa nguzo ya serikali hasa
wakati inapoishiwa fedha katika mambo “nyeti yanayohusiana na usalama wa
nchi” ilikuwa inakopa fedha NBC.
“Majadiliano na Mkapa yalichukua muda
mrefu sana kuhusu suala hilo na itoshe kusema kwamba baada ya majadiliano hayo
marefu likazaliwa wazo la kugawanywa kwa hiyo na kuanzishwa kwa
Benki ya NMB ambayo serikali ina hisa hadi leo.
“Kilichomsikitisha zaidi Mwalimu ni
kwamba baada ya juhudi zote hizo Kamori alifukuzwa kazi kama Mkurugenzi
Mtendaji wa NBC na kurudishwa BoT bila kupangiwa kazi yoyote. Hakuwa na
ofisi pale akifika anasoma magazeti aliyojinunulia na kurudi zake nyumbani.
“Alitishwa sana na kuhojiwa ni kwanini
alikwenda kumweleza Mwalimu na kumwonyesha nyaraka za uuzwaji wa NBC kwa Benki
ya ABSA ya Afrika ya Kusini?
“Kamori alinipigia simu akanieleza
masahibu yaliyomkuta na mimi nikaufikisha ujumbe wake kwa Mwalimu, baada ujumbe
huo Mwalimu alisikitika sana, akahoji ni kwanini wanafanya mambo hayo
“kumfedhehesha” akiwa hai?
“Huyo Kamori alikuwa mzalendo kweli
kweli ni kati ya Watanzania walioipenda nchi yao. Siku hiyo hiyo aliacha kazi
akasema hawezi kupokea mshahara asioufanyia kazi na akaenda kufanya kazi zake
sijui kwa sasa atakuwa wapi.
“Sakata la kuuzwa kwa NBC kwa kweli ni
kati ya mambo yaliyowahi kumchanganya akili Mwalimu na kwa upande wangu uuzwaji
wa benki ile ulifungua milango ya ufisadi mwingine uliokuja kufanyika miaka ya
baadaye,” alisema.
No comments:
Post a Comment