Waziri Mkuu - Mizengo Pinda |
Kiasi cha dola za Marekani milioni 125 (shilingi bilioni
200) zinadaiwa kuchotwa kutoka katika akaunti hiyo na kulipwa kwa kampuni ya
Pan African Power (PAP) katika mazingira ambayo duru za kibunge pamoja na zile
za kibalozi zinaona kwamba yana harufu ya ufisadi.
Vyanzo vya habari hii vimeambiwa kwamba tayari serikali
imepelekewa taarifa rasmi kwa maandishi kutoka kwa nchi wahisani zikieleza
kwamba hazitatoa fedha hizo za msaada, kiasi cha dola za Marekani milioni 559
(shilingi bilioni 900) hadi pale matokeo ya uchunguzi wa suala hilo kutoka
Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) yatakapofahamika.
Mmoja wa mabalozi wanaounda kundi la wahisani hao aliyezungumza
na vyanzo vyetu vya habari kwa masharti ya kutotajwa jina,
alilithibitishia kwamba tayari wamepeleka taarifa Hazina kuhusu maamuzi yao
hayo.
“Ni kweli kwamba tumewapa serikali taarifa rasmi kuhusu
uamuzi wetu. Hili jambo kwanza lilikuwa katika hatua ya mazungumzo tu lakini
sasa tumeamua kuliweka katika maandishi. Ni matumaini yetu kwamba serikali
itatuelewa,” alisema.
Alipotakiwa na mwandishi wa habari hizi kueleza nini hasa
kimeandikwa ndani ya taarifa hiyo, Balozi huyo alisema hataweza kusema chochote
kuhusu kilicho ndani.
“Mimi ni mwanadiplomasia. Nina haki zangu zinazonilinda.
Kilichomo ndani ya taarifa yetu kwa serikali yenu ni kwa ajili ya wana
diplomasia pekee. Siwezi kukwambia wewe kilichomo,” alisema.
Juhudi zetu kumpata Waziri wa Fedha, Saada Mkuya na Naibu
wake, Adam Malima, ziligonga mwamba juzi usiku na hadi tunakwenda mitamboni,
hawakupatikana. Katika mkutano baina ya wahisani na serikali uliofanyika
Novemba mwaka jana katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere
jijini Dar es Salaam, nchi wahisani ziliahidi kuchangia kiasi hicho cha fedha
kwa mwaka huu wa fedha.
Fedha hizo zilitakiwa kuchangia katika maeneo anuai kama
vile upunguzaji wa umasikini, ukuzaji wa ajira na pia katika kusaidia mapambano
dhidi ya rushwa. Kundi la wahisani wanaosaidia bajeti ya Tanzania linaundwa
na nchi na taasisi 12 tofauti ambazo ni Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB),
Canada, Denmark, Umoja wa Ulaya, Finland, Ujerumani, Ireland, Japan, Norway,
Sweden, Uingereza na Benki ya Dunia (WB).
Mtandao huu unafahamu kwamba nchi wahisani hazijafurahishwa
na suala la mgao wa fedha hizo zilizowekwa BoT kutokana na ugomvi baina ya
kampuni ya kufua umeme ya IPTL na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Wiki iliyopita, vyombo vya habari viliripoti namna mmiliki
wa PAP, Harbinder Sethi Singh, ambaye ni mfanyabiashara mwenye historia ya
utata, alivyojipatia mabilioni hayo ya shilingi katika mazingira yenye utata.
Kwa mfano, Singh alimlipa mmoja wa waliokuwa wabia wa IPTL,
James Burchard Rugemalira, malipo ya hisa zake alizouza siku chache baada ya
serikali kuruhusu alipwe na BoT.
No comments:
Post a Comment