To Chat with me click here

Thursday, October 16, 2014

UMOJA WA MATAIFA: KASI YA EBOLA INAZIDI JUHUDI ZA KUPAMBANA NAO

Mkuu wa kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachoshughulikia wito
wa dharura kuhusu maradhi ya Ebola, Bw. Anthony Banbury
ACCRA, Ghana

MKUU wa kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachoshughulikia wito wa dharura kuhusu maradhi ya Ebola, Anthony Banbury, amesema dunia haipigi hatua za haraka kudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo.

Akilihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kupitia mawasiliano ya video kutoka mjini Accra, Ghana, Bw. Banbury amesema ugonjwa huo unakwenda kwa kasi kubwa kuliko inavyodhaniwa.

Kwa mujibu wa DW, Bw. Banbury amesema kasi za ugonjwa huo ni kubwa na unaonekana kuzishinda juhudi za kuudhibiti. Bw. Banbury amesema ili kuudhibiti ugonjwa wa ebola, hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa sasa, kwa sababu kila siku idadi ya wanaoambukizwa inazidi kupanda.

Wakati huohuo, shirika la afya duniani WHO kupitia naibu mkurugenzi mkuu, Bruce Aylward, limesema maambukizi ya ugonjwa wa ebola huenda yakafikia 5000 hadi 10,000 kila wiki kuanzia wiki ya kwanza ya mwezi wa Desemba.

Kwa mujibu wa DW, vifo vya hivi karibuni vilivyoripotiwa vimefikia watu 4,447.Nchi tatu zilizoathirika zaidi na ugonjwa wa ebola Afrika Magharibi ni Liberia, Sierra Leone na Guinea.

Kwa upande wake, Rais wa Marekani, Barrack Obama, anatarajiwa kuwa na mazungumzo kuhusu Ebola kwa njia ya video, na viongozi wa Ujerumani, Italia, Ufaransa na Uingereza.

No comments:

Post a Comment