 |
| Mhe. John Mnyika |
YASADIKIKA
KUWA LILIRUSHWA NA POLISI ALIPOSIMAMA
VITUKO
na matukio ya hatari kwenye mikutano ya CHADEMA vimeendelea kushika kasi.
Jana
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alinusurika kupigwa na bomu la machozi
lililorushwa na polisi waliokuwa wakizuia kufanyika mkutano ulioitishwa na
chama hicho.
Tukio
hilo lilitokea katika eneo la Mabibo kwenye viwanja vya Sahara ambapo bomu hilo
lilimpata mtu aliyekuwa karibu na Mnyika anayeitwa Thomas Jerome, aliyejeruhiwa
sehemu ya paja.
Baada
ya kurushwa kwa bomu hilo, polisi walitaka kumchukua majeruhi huyo ili wamweke
kwenye gari lao apelekwe hospitalini, lakini Mnyika aliwaelekeza wafuasi wa
CHADEMA kumchukua kwa madai kitendo kilichofanywa na askari hao kililenga
kuficha ushahidi wa jambo hilo.
Polisi
waliokuwemo eneo la tukio waliamua kukubaliana na matakwa ya wafuasi wa CHADEMA
waliomchukua Jerome na kumpeleka hospitali ambako hali yake inadaiwa inaendelea
vizuri.
Akielezea
hali ilivyokuwa akiwa katika mkutano mwingine uliofanyika Ubungo, Mnyika
alisema polisi walifika katika viwanja vya Sahara wakiwa na magari matatu kwa
lengo la kutawanya wafuasi wa CHADEMA wasifanye mkutano wakidai haukuwa na
baraka za jeshi hilo.
Mnyika
alisema polisi hao walisema sababu ya kuuzuia mkutano huo ni uwepo wa ziara ya
Makamu wa Rais katika Wilaya ya Kinondoni, hivyo walikuwa wameelekeza nguvu zao
katika ziara hiyo, kwamba hawakuwa na uwezo wa kuulinda mkutano wa CHADEMA.
“Nikiwa
nimejiandaa kupanda jukwaani ndiyo polisi walikuja kusema tuache tusifanye
mkutano, nilisogea karibu na gari kumlalamikia ofisa wa polisi kwani kitendo
cha kuahirisha mkutano kwa barua waliyoileta saa sita mchana siku ya mkutano
wakati sisi tuliwapa taarifa siku nne zilizopita ilikuwa sio haki.
“Nilimwambia
ofisa huyo wa polisi kuwa nilikuwa najadiliana kwa simu na viongozi wakuu wa
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na Inspekta Jenerali wa Polisi
Said Mwema kumlaumu kutumika vibaya kwa Jeshi la Polisi.
“Nilipokuwa
bado najibizana naye bila fujo zozote, bomu lilirushwa kutoka ndani ya gari ya
polisi na kupita karibu na mimi likamjeruhi mtu aliyekuwa karibu yangu, ki
ukweli nimeshangazwa sana na matumizi mabaya ya silaha za moto,” alisema.
Aliongeza
kuwa katika purukushani zilizotokea baada ya bomu kupigwa, alipoteza nyaraka
mbalimbali alizokuwa amebeba kama ushahidi kuwaonyesha wafuasi wa chama hicho
hasa jinsi serikali ya CCM na wabunge wake walivyopitisha kodi ya huduma za
simu, na kodi ya laini za simu.
Slaa anena
Aidha
katika mkutano huo ambao awali ulitangazwa kuwa ungehutubiwa na Katibu Mkuu wa
chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, haukuweza kuhutubiwa naye kwa kile alichosema
kuwa watu wake wa usalama walimwambia mapema hali si salama kwenye mkutano huo.
“Nilipata
taarifa kutoka vyanzo vyangu kuwa polisi walikuwa na mpango wa kuleta fujo,
hivyo nikaona kwa kuwa wanatuwinda nisingeenda kuhutubia, pengine bomu
lililomkosa Mnyika lilikusudiwa kwangu au kwa mwingine,” alisema Dk. Slaa
alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu baada ya kutoonekana mkutanoni.