To Chat with me click here

Friday, April 4, 2014

PROPAGANDA YA KATIBA MPYA: UFISADI WA CCM




HAPO mwanzo, wakati Tanganyika inapata uhuru kulikuwapo na chama cha ukombozi wa Waafrika wa Tanganyika (TANU) ambacho kiliweza kuwaunganisha wananchi! Baadaye, TANU iliungana na ASP kuunda Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kwa falsafa yake kiliamua kuandaa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Katiba ya 1977 iliipa CCM haki ya kipekee ya kushika hatamu za uongozi (kama ilivyokuwa kwenye Ibara ya 10 ya Katiba ya JMT, 1977).

Katiba ya 1965 na ya 1977, TANU kwa upande wa Tanganyika ilijipendelea na haikuruhusu maoni ya wananchi isipokuwa ilichukua mamlaka wa watu na kuyafanya kuwa sehemu ya itikadi ya chama kwa madai ya kuwashirikisha wakulima na wafanyakazi.

Kwa upande wa Zanzibar, baada ya mapinduzi ya Januari 11 na 12, 1964 vyama vyote vya siasa vilipigwa marufuku na ASP iliendesha nchi kwa kutumia mawazo na maoni ya watu 14 (maarufu kama, Baraza la Watu 14 au Baraza la Mapinduzi). Fikra za watu wawili (Nyerere na Karume) zilitawala fikra za wananchi wote wa Tanzania!

Mwaka 1977, kama kawaida ya vyama vinavyopora uhuru, haki na usawa wa wananchi kwa muundo wa chama kushika hatamu, CCM ilijipa haki za kipekee (exclusive rights) za kutawala na kwa kutumia katiba iliyotungwa kukidhi utashi huo iliendelea kufaidi haki za kipekee kwa muda mrefu hata sasa!

Japokuwa CCM ilifanya ufisadi mkubwa kwenye mfumo wa serikali zake (ya muungano na ya mapinduzi), jambo kubwa lililowekwa na CCM kwenye Katiba ya 1977 ni nafasi ya kipekee ya kuongoza mabadiliko!

Mkakati wa kujipa mamlaka ya kipekee katika kufikia mujtamaa wa watu kwa uhuru, haki na usawa ulikuwa ufisadi wa kutisha ambao CCM imeendelea kuutumia hata wakati huu nchi inapotarajia kuandika Katiba Mpya!

Kazi ya kuandika katiba ya wananchi ni kazi ngumu kama kuna mikingamo inayotokana na ufisadi wa kimfumo na wa kimuundo uliyojengwa kwa miaka mingi na chama kinachoongoza kwa propaganda, hila, mizengwe, woga na ukiritimba wa kisiasa!

CCM imejenga mazingira ya kutumia uongo wa kimasilahi na kuwafanya wanachama wake waamini kila chama hicho kinachoamini na kukitetea! Tazama, wakati lilipofanyiwa upitizi Azimio la Arusha, mwenyekiti wa wakati huo, Ali Hassan Mwinyi alisema: Azimio la Arusha, kama tunavyojua, limetangazwa mwaka 1967. Hii leo tuko katika mwaka 1991.

Imepita miaka mingi, zaidi ya 20 tangu kutangazwa kwa Azimio la Arusha. Na katika kipindi cha miaka 20 yametokea mabadiliko mengi duniani na pia katika hali ya maisha yetu (rejea hotuba ya Februari,25, 1992, Diamond Jubilee, Dar es Salaam).

Hotuba ya mzee Ali Hassan Mwinyi, ililenga katika kuonesha mabadiliko yaliyotokea na yanayohitaji mabadiliko katika kufanya upitizi wa marekebisho ya Azimio la Arusha ili kwenda na wakati!

Inashangaza, CCM iliona busara kubadilisha falsafa ya kuendesha Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kwa kubadilisha baadhi ya miiko na maadili ya uongozi wa umma kwa kuzingatia mabadiliko ya wakati. Huku ikisisitizwa kwamba, ‘kila zama na kitabu chake.’


Kitabu cha CCM kilikuwa kuwaruhusu makada wa chama hicho kutawala uchumi ili kwenda na wakati lakini ilikuwa kinyume na kuwarudishia wananchi mamlaka yao waliyoyapora kwa ukiritimba wa siasa. CCM hiyo hiyo inaogopa mabadiliko ya katiba!

CCM imepora uhuru wa wananchi kuwa na maoni (kama ilivyo kwenye Ibara ya 18); CCM imejivika mamlaka ya kuwasemea wananchi badala ya kuwaruhusu wananchi wawe huru kueleza fikra zao. Hii inatokana na falsafa ya ‘zidumu fikra sahihi’ kama zilivyoatamizwa kwenye bongo (zilizotekwa) za wanachama na wananchi waliyo wengi na kuimbishwa tangu 1977!

Tangu mwanzo, sehemu kubwa ya fikra hizi za mamlaka ya CCM zilijengwa na makada waliopewa dhamana ya ujenzi wa chama dola ambacho kilichukua dhamana ya uongozi wa siasa na maamuzi yote yenye taathira kwa nchi na watu.

Kwa kuwa ufisadi ni uharibifu, wa aina yoyote iwayo; CCM imeharibu mfumo na muundo wa ufinyanzi wa hoja mbadala kwenye kufikia utashi wa watu wengi katika ujenzi wa jamii ya watu waliyo sawa na huru.

Tazama, kwenye Bunge Maalumu la Katiba; CCM ina wajumbe zaidi ya asilimia 80 na imewekeza hata kwa wale wajumbe wanaodhaniwa ni huru wanaotokana na wajumbe 201.

Ufisadi wa kununua baadhi ya wajumbe umeripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba wenye dhamana na serikali ya CCM wakiwamo mawaziri waandamizi wamehusika katika kununua wajumbe wa makundi maalum ili wapate uungwaji mkono wa ukiritimba.

Ukiachilia mbali uharibifu wa fikra za baadhi ya makada wa CCM juu ya muundo na mfumo wa serikali na muungano sawia; kuna kila sababu ya kuliangalia suala la haki ya nchi ambayo mara zote ni watu wanaowakilishwa na sehemu ndogo ya watu waliyopata nafasi ya kuingia kwenye Bunge Maalumu la Katiba.

Wajumbe wachache, kama 640 kwa makadirio wawe na taathira ya kuamua hatma ya katiba (sheria kuu) ya nchi kwa utashi wa chama kinachoongoza kwa ufisadi wa kimfumo na wa kimuundo! Huu utakuwa ni wendawazimu kwa watu wenye akili timamu kudhani kwamba inaweza kuwa rahisi kulazimisha utashi wa kifisadi pasipokuwa na matokeo au taathira hasi juu yake!

Hata kama baadhi ya makada wa CCM wamelishwa kasumba ya kudhani kwamba, sauti ya wengi wanaowakilisha wachache ni sauti ya Mungu! Sidhani kama itakuwa muafaka kwa chama chenye wanachama wasiozidi milioni sita kuwakilisha mawazo na maoni ya wananchi wanaokadiriwa milioni 45 wa Tanzania!

Haiwezekani kwa CCM kupora uhuru, haki na usawa wa watu milioni 45 kwa utashi wa watu milioni 6! Huu ni ufisadi wa kisiasa na unyang’anyi usiyokubalika katika nchi inayohitaji mabadiliko ya fikra na ya mapinduzi katika kuwaondoa watu kutokana na unyonge wa kutawaliwa na fikra za kifisadi!

CCM, kama chama chenye dhamana ya kusimamia mchakato wa uandikaji wa Katiba Mpya, lazima ijitazame upya na itafakari kwa kina juu ya mujtamaa na mustakabali wa Tanzania kwa misingi ya uhuru wa watu, haki ya watu, na usawa wa watu kwa mujibu wa haki ya asili.

Kinyume chake, kuna hatari ya kutengeneza uasi utakaoatamizwa kwenye fikra za wananchi juu ya mwendo wa kifisadi unaofanywa na CCM katika ujenzi wa Tanzania yenye kuzingatia uhuru, haki, usawa na uadilifu katika kufikia utashi wa watu na nchi.

CCM inaweza kuleta mabadiliko yanayohitajika, iepuke propaganda na iache ufisadi wa kimfumo na kimuundo! 

No comments:

Post a Comment