VITA
ya urais mwaka 2015
ndani ya chama tawala – CCM, inatajwa kuwa ngumu na kutabiriwa kwamba inaweza
kukiathiri kutokana na tabia ya uhasama inayojengeka siku hadi siku.
Inatabiriwa
kwamba kuna kila dalili za CCM kupasuka vipande vipande kama tabia ya siasa za
fitna na kupakana matope zitaachwa ziendelee kuimomonyoa.
Baadhi
ya wanasiasa wanajiona kuwa na haki ya kucheza rafu na kuchafua wenzao kwa
gharama zozote ili mradi waonekane hawafai kupitishwa na chama hicho kugombea
urais wa mwaka 2015.
Mizizi
ya siasa chafu za kupakana matope ina kina kirefu ndani ya CCM na haijaanza
juzi, bali ni staili
iliyotumiwa na kundi maarufu la mtandao lililomwingiza Rais Jakaya Kikwete
madarakani mwaka 2005.
Wapo
wanasiasa ambao hadi sasa wanaugulia majeraha yaliyosababishwa kwa makusudi na
kundi la mtandao mwaka 2005 kwa lengo la kuhakikisha kwamba hawapati nafasi ya
kuteuliwa kuwa wagombea wa nafasi ya urais kwenye mchuano huo uliokuwa na
wagombea 11.
Walioumizwa
na wanaodaiwa kuendelea kuwekewa macho mawili mawili hadi leo ni wale
walioonekana kuwa na ushawishi na nafasi pana ambayo kwa njia moja au nyingine iliibua
hofu kubwa kwa kundi hilo na mgombea wao kwa kuamini kwamba wangekuwa kikwazo
kikubwa kwao kukidhi malengo yao.
Chini
ya kundi hilo, tuliona kashfa mbalimbali zikiwaandama wanasiasa waliokuwa na
majina makubwa kwa kuibuliwa mambo yasiyo na vichwa wala miguu.
Katika
hili CCM imejiwekea ‘laana’ ambayo lazima itakuja kukigharimu chama hicho,
kwani uchafu huo ulipokuwa ukifanyika, chama kilifumbia macho na kujifanya
kwamba hakioni wakati wanachama wake wakiumizwa na kundi hilo na chama kukaa
kimya bila kutoa tamko lolote.
Baadhi
ya vyombo vya habari viligeuka kuwa wakala namba moja wa kundi la mtandao kwa
kuhakikisha vinapeleka ujumbe hasi kwa wananchi dhidi ya wagombea walioonekana
kuwa tishio kwa kundi hilo la mtandao.
Tuliona
namna aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Katibu wa Umoja wa Nchi Huru za
Kiafrika (OAU, sasa AU), Dk. Salim Ahmed Salim alivyoandamwa kila kona kuanzia
maisha yake binafsi kwa kudaiwa kumdhulumu na kumnyima haki zake mmoja wa
watu waliokuwa wasaidizi wake.
Haikuishia
hapo Watanzania wakaaminishwa kwamba Dk. Salim, aliyeipatia nchi hii heshima
kubwa kimataifa, si Mtanzania na ndugu zake wana vyeo vya juu huko Arabuni huku
yeye akidaiwa kuwa mwanachama wa chama cha Hizbul, kilichouunga mkono utawala
wa Sultani huko Zanzibar.
Hayakuishia
kwa Dk. Salim, kundi hilo linaloonekana kutaka kutumia tena staili hiyo ya
kupakana matope kwenye uchaguzi mkuu ujao lilimwandama aliyekuwa Waziri Mkuu
wakati huo, Frederick
Sumaye, kwa kumpaka matope katika masuala mbalimbali likiwemo la kujilimbikizia
utajiri wa matrilioni hadi kuwapora wanakijiji ardhi huko Mvomero na Kibaigwa.
Hata
hivyo, muda na wakati ulibainisha ukweli wa hayo baada ya kundi hilo kupata
walichotaka na ghafla hatukusikia tena ‘uchafu’ wala ‘wizi’ wa kina
Sumaye.
Hofu
na tabia za kundi hili zinatajwa kuanza kuchukua kasi tena wakati huu wa kuelekea
uchaguzi mkuu ujao. Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Nyerere
aliwahi kuonya kuwa: “Ukila nyama ya mtu huwezi kuacha tabia hiyo, itaendelea.”
Haiyumkini
kwamba kundi la mtandao ni kama mtu aliyeonja nyama ya mtu, hivyo ni vigumu
kuacha tabia hiyo.
Watanzania
watarajie kusikia kwa mara nyingine siasa chafu za kupakana matope kwa gharama
ya urais tu, tabia ambayo enzi za Mwalimu Nyerere haikuwahi kujitokeza.
Sumaye
anaweza kuwa mmoja wa wanasiasa wanaongoza kukaliwa kooni na wanamtandao kwa
kila hatua ya mguu wake unapokanyaga kuanzia pale alipotangaza kugombea urais
akiwa bado Waziri Mkuu hadi alipostaafu na wakati huu tunapoelekea uchaguzi
mkuu mwaka 2015.
Hadithi
ya Sumaye na kundi la mtandao inaweza kufananishwa na uhusiano uliopo kati ya
paka na panya ambao hata siku moja hawawezi kupikika chungu kimoja.
Sumaye
mwaka 2005 ndiye aliyejikuta akitengenezewa zengwe na kuachwa na ndege huko
Tabora na kulazimika kupanda kiberenge kwenda Kigoma kuwahi muda wa kupata
wadhamini wa fomu zake za kugombea uteuzi wa kugombea urais.
Sumaye
huyu ndiye aliyejikuta akihujumiwa na kundi la mtandao kwenye mkutano mmoja wa
hivi karibuni uliofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam, wakati
akiendelea kusubiri watu wajae alishitukia akiambiwa kwamba nafasi yake ya
mgeni rasmi imepewa aliyewahi kuwa Waziri wa Viwanda, Nazir Karamagi.
Hilo
halikuishia hapo, Sumaye alijikuta akifanyiwa hujuma kwa kile
kilichodaiwa mpango uliosukwa na wagombea urais, wafuasi wa kundi la mtandao
wakati alipoalikwa kuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa Chama cha Kuweka na
Kukopa (Saccos) huko mkoani Kagera na nafasi hiyo kupewa mtu mwingine katika
dakika za mwisho.
Mbali
ya hilo, ‘faulo’ aliyochezewa Sumaye na kundi la mtandao kumbariki Waziri Dk.
Mary Nagu kwenye kinyang’anyiro cha mjumbe wa NEC Hanang’ na kumwangusha
kiongozi huyo aliyemshika mkono na kumlea kisiasa, Dk. Nagu, ni mambo
yanayoonyesha nguvu kubwa ya mtandao inayojipenyeza kwa gharama yoyote hata kwa
watu wa karibu wa mwanasiasa huyo ili kuhakikisha safari yake kisiasa haifiki mbali.
Tukio
la hivi karibuni pia la kukamatwa na meno ya tembo kwa dereva mmoja anayedaiwa
kumwendesha kiongozi huyo, lilihusishwa na mikakati ya kumhujumu kiongozi huyo
katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015.
Dereva
huyo anadaiwa kutumia gari hilo baada ya kumwacha kiongozi huyo na mkewe uwanja
wa ndege waliposafiri kwenda nchini Marekani na yeye kwenda na gari hilo
Morogoro.
Hata
hivyo, Sumaye mwenyewe alipohojiwa na gazeti moja kutoka aliko safarini
Marekani kuhusu tukio hilo alisema: “Sijazungumza chochote, siwezi kusema sasa
ni njama za nani. Tukio hili limetokea nikiwa sipo nchini na sihusiki nalo kwa
lolote na sina mtu wa kumlaumu, naachia vyombo vya dola vifanye kazi yake
na sheria ichukue mkondo wake…ni uhalifu uliotokea, nasisitiza dola
ifanye kazi yake kama inavyotakiwa.”
CCM
inaweza tu kuondoka hapo ilipofikia kama italinda haki za wanachama wake wote
na kuacha woga wa kukemea na hata kuwachukulia hatua kali makada wa chama hicho
wanaotafuta uongozi kwa gharama za fitna na kuchafua wenzao kwa manufaa yao
binafsi.
No comments:
Post a Comment