JESHI la Polisi nchini limemkamata
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
Wilfred Lwakatare, kwa tuhuma za kuhusika na matukio ya mashambulizi dhidi ya
watu hapa nchini.
Taarifa kutoka Ofisi za Makao Makuu ya
CHADEMA Kinondoni jijini Dar es Salaam zilieleza kwamba Lwakatare alikamatwa
saa 7 mchana na watu wanne waliojitambulisha kama maofisa wa Jeshi la Polisi
ambao walifika na gari aina ya Toyota Land Cruiser jeupe lenye namba za usajili
T 140 BLA likiwa na chata ya kitalii.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera
Senso, alisema Lwakatare amekamatwa kwa tuhuma zilizosambazwa kwenye mtandao. Naibu
Katibu Mkuu wa CHADEMA Zanzibar, Hamad Yusufu Musa, ambaye alishuhudia tukio la
kukamatwa kwake, aliliambia Tanzania Daima kuwa kiongozi huyo anatuhumiwa
kupanga njama za matukio ya kushambulia raia yaliyotokea hapa nchini.
Hata hivyo Musa hakusema ni matukio
gani yanayomhusisha kigogo huyo, lakini mtu aliyesambaza mkanda wa video katika
mitandao ya kijamii jana aliandika chini yake maneno yasemayo: ‘Mikakati ya
mateso ya Kibanda na mwandishi mwandamizi wa gazeti la Mwananchi, mhusika mkuu
huyu hapa.’ akimaanisha Lwakatare.
Akizungumza na
Tanzania Daima jana, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema
kukamatwa kwa Lwakatare na kuhusishwa na matendo hayo ya utekaji na kushambulia
watu, kumedhihirisha kuwapo kwa njama chafu zenye lengo la kukichafua chama
hicho mbele ya jamii.
Dk. Slaa alisema njama hizo
zinaratibiwa na kigogo mmoja serikalini ambaye analitumia Jeshi la Polisi na
vyombo vingine vya dola kuidhoofisha CHADEMA.
“Ikiwa ni kweli wanamshikilia kutokana
na hiyo video, ni furaha kwetu, kwa sababu ukombozi wa nchi umekaribia,”
alisema bila kufafanua.
Hata hivyo Dk. Slaa alisema
ameshangazwa na uharaka wa polisi wa kumkamata Lwakatare siku moja tu baada ya
video hiyo kuwekwa mtandaoni, na kuacha hata kumhoji mmoja wa mawaziri
aliyetajwa na baadhi ya magazeti jana akihusishwa kutekwa na kuteswa kwa
Kibanda.
“Waziri hajakamatwa wala kuhojiwa,
alitekwa Ulimboka akamtaja ofisa wa Ikulu, lakini hajakamatwa wala kuitishwa
gwaride la utambulisho. “Aliuawa kinyama Mwangosi (Daudi Mwangosi), katikati ya
kundi la maofisa wa polisi na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, lakini
hakuna aliyechukuliwa hatua. Lakini kwa video ambayo haijulikani asili yake,
polisi wameharakisha kumkamata na kumpekua nyumbani kwake, kulikoni?” alihoji Dk.
Slaa.
Alisema ni wazi kwamba sasa lazima
Watanzania wafumbue macho na wajue ukweli ulivyo na namna polisi wanavyotumika
kuiangamiza CHADEMA, lakini akadai kuwa ukweli utajulikana muda si mrefu. Wakili
wa Lwakatare, Nyaronyo Kicheere, akizungumza, alisema mteja wake majira ya saa
10 alikwenda kupekuliwa nyumbani kwake Kimara.
“Kwa sasa tumeshafika nyumbani kwa
Lwakatare Kimara King’ong’o na maofisa wapatao saba wanaendelea na upekuzi
katika nyumba yake,” alisema mwanasheria huyo.
No comments:
Post a Comment