WANASHERIA wameunga mkono msimamo wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na wale wa NCCR- Mageuzi kupinga
hatua ya Ofisi ya Bunge kuliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata wabunge wake ili
wakahojiwe.
Wakizungumza na Tanzania Daima, mwanasheria
mashuhuri hapa nchini na wakili wa kujitegemea, Mathew Kakamba, alisema ni
kinyume cha sheria na ni matumizi mabaya ya madaraka kwa Ofisi ya Bunge kutumia
polisi kuwakamata wabunge katika masuala yanayolihusu Bunge.
Wanasheria hao walitoa maoni yao kuhusiana
na mvutano mkubwa wa kisheria uliozuka baina ya CHADEMA na Ofisi ya Bunge
ambayo imeagiza kukamatwa kwa wabunge kadhaa wa upinzani ili wakahojiwe na
Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge, ambayo CHADEMA wanadai kuwa haipo.
Wakili Kakamba katika maoni yake
alisema ni makosa kisheria kutumia nguvu za mhimili mwingine katika kuendesha
masuala yanayohusu mhimili wa pili.
“Kuna mgogoro unaojulikana kwa
Watanzania karibu wote kuhusiana na vurugu zilizotokea katika mkutano wa Bunge
lililokwisha, na kuvunjwa kwa kamati za kudumu za Bunge.
“Pamoja na kuvunjwa kwa kamati hizo,
bado kama sikosei, wajumbe wake hawajateuliwa na kwa maana hiyo, kisheria
utendaji wake haujaanza. Kwa lugha nyingine, haziwezi kuitwa kamati rasmi kwa
sababu hazina wajumbe,” alisema Wakili Kakamba.
Kauli ya Wakili Kakamba imeungwa mkono
na wakili mwingine, Aloyce Komba, ambaye amekiita kitendo cha Ofisi ya
Bunge kutumia polisi kuwakamata wabunge wao wa upinzani kuwa ni udhalilishaji
mkubwa na uvunjaji wa haki za binadamu.
Komba anayetoka Kampuni ya Uwakili ya
Haki Kwanza, alisema Bunge ni chombo kinachojitegemea na linazo sheria na
kanuni zinazopaswa kutumika kumlazimisha mbunge kutimiza agizo la wito.
“Masuala yote ya Bunge yanatakiwa
kuendeshwa kibunge bila kutegemea vyombo vingine vya nje, labda tu ikiwa kuna
mwingiliano kutoka katika mhimili mwingine. “Si sahihi kwa spika kutumia polisi
kuwakamata wabunge wakati wanazo kanuni na taratibu nzuri tu, na sidhani kama
ni utaratibu mzuri na unaolenga kudumisha demokrasia.
“Mbunge akishindwa kufika, kwani hakuna
sheria nyingine hata za kuzuiwa kuhudhuria vikao kadhaa vya Bunge, hadi leo
wanataka kutumia polisi kuwakamata?” alihoji Komba.
Akizungumzia uhalali wa kamati hizo,
Komba ambaye ni mtaalamu wa sheria katika mambo ya utawala, alisema kimsingi
hazipo, kwa sababu tangu kuvunjwa kwake na kuundwa nyingine, bado spika
hajateua wajumbe wa kamati mpya.
“Hajateua wajumbe wa kamati hizo, na ni
sawa kabisa kuwa hazipo. Sasa wanaitwa kuhojiwa na kamati gani? Mtazamo wa
kisheria ni kwamba hazipo.
Alikwenda mbali zaidi na kuilaumu Ofisi
ya Bunge kwa madai ya kuvunja haki za msingi kwa sababu aliyetendewa kosa ni
spika (kiti), anayelalamika ni spika, mteuzi wa kamati ni spika na ushahidi mwingi
utatoka kwa spika, hivyo kupingana kabisa na haki za sheria ambazo mlalamikaji
hapaswi tena kuwa mwendesha mashitaka.
Hata hivyo, mawakili hao walikubaliana
na kuwataka wabunge wote waliopata barua za wito kutoka Ofisi ya Bunge kuitikia
na si kukaidi. “Pamoja na kasoro hizo, kama wameitwa na Ofisi ya Bunge,
wanatakiwa kwenda na si kugoma. Huko ndiko mahali pekee wanakotakiwa kuwakosoa
hao wakubwa, na hata wanao uwezo wa kukataa kuzungumza hata kama kamati yenyewe
ingekuwa hai kisheria,” walisema wanasheria hao.
CHADEMA wagoma
Juzi Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk.
Willibrod Slaa alimwagiza Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni kuiandikia
barua Ofisi ya Bunge ya kukataa wabunge wake kukamatwa na polisi ama kuhojiwa
na kamati waliyodai ni hewa, kwa kuwa zilizokuwapo zilivunjwa na Spika Anne
Makinda katika kikao kilichoisha mwezi uliopita.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana,
Dk. Slaa alisema kisheria, kanuni na taratibu za Bunge, kamati ambazo
zimeshavunjwa haziwezi kufanya kazi yoyote kwa kuwa ni batili mpaka hapo
zitakapoundwa kamati nyingine.
Alilitaka Bunge kurejea kanuni za
kudumu za Bunge namba 113 (7), inayozungumzia ukomo wa uhai wa kamati za Bunge,
uhai wake unaishia Mkutano wa Kumi wa Bunge ambapo inakuwa ni nusu ya kwanza ya
uhai wa Bunge lenyewe.
Dk. Slaa alisema kutokana na kifungu
hicho, inaonesha dhahiri kwamba Spika Anne Makinda na wasaidizi wake wana
matumizi mabaya ya sheria, kutoifahamu vizuri ama kulewa madaraka, hali ambayo
CHADEMA haitakubaliana nao.
Hivyo alisema Kamati ya Haki, Kinga na
Maadili ya Bunge ambayo ilikuwa chini ya Mbunge wa Mlalo, Brigedia mstaafu
Hassan Ngwilizi (CCM), haitawahoji wabunge wake kwa kuwa imekwisha kumaliza
kazi yake tangu Februari 8, mwaka huu.
Msimamo wa CHADEMA unakuja zikiwa ni
siku mbili tangu Ofisi ya Bunge kupitia Katibu Mkuu, Dk. Thomas Kashililah,
itumie Jeshi la Polisi kuwataarifu baadhi ya wabunge wa chama hicho kuwa
wanahitajika jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano na kamati hiyo.
Katibu Mkuu huyo alisema kama wabunge
wa CHADEMA wanaitiwa kuhusu vurugu zilizotokea bungeni Februari 4, mwaka huu,
tayari zimeshatolewa hukumu yake kwa kuwataja wahusika kuwa ni Tundu Lissu
(Singida Mashariki), John Mnyika (Ubungo), Paulina Gekul (Viti Maalumu) na
Joshua Nassari ( Arumeru Mashariki).
Alisema katika hukumu hiyo ambayo
ilisomwa na Spika Makinda ilikuwa ya upande mmoja wa kamati yenyewe iliyokaliwa
na wabunge wa CCM ambao waliwaona wabunge wa CHADEMA pekee ndio waliofanya
vurugu huku ikishindwa kuwaita wahusika kwa mahojiano.
Aidha, alisema hata kama kamati ya
Brigedia Ngwilizi ingekuwa hai, wabunge wake wasingeitii, kwa kuwa tayari
imekwisha kuwahukumu.
Hata hivyo Dk. Slaa alitumia nafasi
hiyo kumtaka Spika Makinda kwenda kozi kwa ajili ya kujifunza sheria za
kuongoza Bunge kutokana na kushindwa kwake katika kipindi chote alichokalia
kiti hicho.
“Nasikia Spika Makinda huwa anasema
kuwa niwafundishe wabunge wangu sheria, kanuni na taratibu za Bunge kwa
kuwa nazifahamu vizuri, kwani yeye na wanasheria wake wanafanya nini? Kupoka
kwake sheria na taratibu za bungeni ndizo zinazosababisha vurugu?” alihoji Dk.
Slaa na kuongeza:
“Nataka nimwambie kwamba wakati nipo
bungeni, maspika waliokuwa wakiongoza Bunge akiwamo Samuel Sitta walikuwa
wakijua kuongoza, kwa kufuata sheria na kanuni zake na ndiyo maana hakuna
vurugu zilizokuwa zikitokea na si yeye.”
Aidha, alisema maspika hao walikuwa
wanajua kwamba mabunge yote ya Afrika na yale ambayo Tanzania inaiga kutoka
kwao yana sheria na taratibu zinazowaruhusu kushangilia hata kuzomea kwa kutaja
chama chao na si hivi ambavyo Spika Makinda anavyofanya.
Lissu anena
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Lissu
alisema kwa mujibu wa sheria na kanuni za Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya
Bunge, zinamtaka Katibu Mkuu wa Bunge Dk. Kashililah kuandika barua hizo kwa
niaba ya Spika Makinda lakini hakufanya hivyo.
Lakini pia Lissua alisema hata barua ya
polisi (police message) waliyopewa si taarifa tosha ya kujipeleka wao kuhojiwa
bali walipaswa kupelekewa taarifa ya kuitwa kwa ajili ya mahojiano na Bunge.
Kutokana na maelezo hayo Lissu alisema
hakuna jambo lililofuatwa kisheria, hivyo hakuna watakayemwona, na alidai kuwa
tayari hukumu yao ilishatolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Brigedia Ngwilizi
Februari 8, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment