To Chat with me click here

Wednesday, March 13, 2013

UHURU KENYATTA: HUU NI UKOMAVU WA KWELI KWA DEMOKRASIA



Nairobi, Kenya. Rais Mteule wa Kenya, Uhuru Kenyatta ameahidi kwamba muungano wa Jubilee utahakikisha unabadilisha maisha ya Wakenya na kuomba ushirikiano kwa watu wa kada zote ili waweze kutimiza ahadi walizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi.

Kenyatta ambaye amechaguliwa kuwa Rais wa nne wa Kenya alisema kwamba atahakikisha anatembelea maeneo yote ya nchi na kuhakikisha ahadi ya muungano wa Jubilee ya kuongeza ajira na kuwawezesha wananchi inatekelezwa bila kujali kabila, dini au rangi.

Aliyaeleza hayo wakati wa ibada ya Jumapili huko Gatundu juzi, ambapo pamoja na kusali alipokea wageni waliokwenda kumpongeza katika makazi ya familia huko huko Gatundu.

Wakati akielekea kanisani, Kenyatta aliweka vituo kadhaa kwenye maeneo ya Juja, Kimonyo na Gatundu ambapo alisalimiana na mamia ya wafuasi wake waliokuwa wamejipanga barabarani huku wakimshangilia.

Akizungumzia ushindi wake, Kenyatta alisema hiyo ni ishara ya wazi kwamba ni ushindi kwa demokrasia na amani. Baada ya kutangazwa mshindi katika uchaguzi uliofanywa Jumatatu wiki iliyopita, kwa kupata asilimia 50.07, Kenyatta alisema wapiga kura walizingatia sheria na kuahidi kushirikiana na wapinzani wake.
 
Hata hivyo, mpinzani wake mkuu, Raila Odinga, aliahidi kupinga ushindi wa Kenyatta mahakamani.

Aidha Kenyatta , anakabiliwa na kesi ya uhalifu dhidi ya ubinadamu katika mahakama ya ICC, akidaiwa kuhusika na ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.

Kenyatta anatuhumiwa kwa kuchochea ghasia baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 ambapo zaidi ya watu 1000 waliuawa na wengine zaidi ya 600,000 kuachwa bila makao.

Siku ya Jumamosi, tume ya uchaguzi ilimtangaza Kenyatta kama mshindi wa uchaguzi huo, baada ya kushinda zaidi ya asilimia 50 kwa njia ya wazi na huru.
Tume hiyo ilisema kuwa wapiga kura zaidi ya walijitokeza kwa wingi sana asilimia 86, idadi kubwa zaidi ya wapiga kura kuwahi kushuhudiwa. Ulikuwa uchaguzi wenye ushindani mkubwa kuwahi kushudiwa.
 
Baada ya matokeo kutangazwa, Kenyatta aliwaambia wafuasi wake kuwa atawahudumia Wakenya wote, bila ya upendeleo. Baada ya ushindi wake, Uhuru aliwaambia Wakenya kuwa kinachosherehekewa ni ushindi wa demokrasia, amani na umoja. 

Aliongeza kuwa wapiga kura walionyesha kukomaa kisiasa kwa kiwango ambacho hakikutarajiwa na kuwataka walioshindwa kushirikiana nao. Hata hivyo kwa upande wake, Odinga, alisema tume ya uchaguzi iliwakosea wakenya. Ametangaza kuwa atapinga matokeo hayo katika mahakama ya juu zaidi.

No comments:

Post a Comment