To Chat with me click here

Thursday, March 14, 2013

KIBANDA AANZA KUSIMAMA


Tanzania Editors Forum Absalom Kibanda.
MHARIRI Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006), Absalom Kibanda, ameanza mazoezi ya kusimama. Kibanda amelazwa katika Hospitali ya Millpark iliyoko Johannesbaurg, Afrika Kusini baada ya kuteswa la kujeruhiwa vibaya wiki iliyopita.

Taarifa ya Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena, Dar es Salaam jana, ilisema kwa ujumla afya ya Kbanda inaendelea kuimarika na madaktari na wauguzi katika hosipitali hiyo wameendelea kumuhudumia kwa karibu.

“Nafuu aliyoipata imemwezesha kuanza mazoezi ya kusimama na kutembea ndani ya chumba alimolazwa. Madaktari wanaomtibu wamesema wanafanya hivyo kuwezesha mwili wake kupata nguvu na kuujengea uwezo wa kujitegemea,” ilisema taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa Meena, baada ya siku mbili au tatu kadri hali halisi itakavyokuwa, madaktari wanatarajia kuanza mazoezi ya kumtembeza nje ya chumba chake katika jitihada hizohizo za kuuwezesha mwili wake kupata nguvu.

Wakati huo huo, Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mtwara (MTPC) imesema imepokea kwa masikitiko taarifa za kuvamiwa, kupigwa na kuteswa kwa Kibanda.

Katika taarifa yake jana, MTPC ilisema inampa pole Kibanda kwa tukio hilo na inamuombea kwa Mungu apone haraka majeraha aliyoyapata arejee kazini kuendelea na shughuli za upashanaji habari.

“Klabu unaungana na wadau wengine wa habari nchini kulaani vikali tukio hilo na mengine yanayohusisha utesaji wa wanahabari na inalitaka jeshi la polisi kuharakisha uchunguzi wahuska wakamatwe na wafikishwe mbele ya vyombo vya husika sheria ichukue mkondo wake.

“Sisi wanahabari wa Mtwara tunalichukulia tukio hilo kama njama za watu wachache za kutaka kufifisha taaluma na uhuru wa habari nchini kwa kubana wigo wa upashanaji habari za kweli na zenye maslahi kwa Watanzania,” ilisema taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment