To Chat with me click here

Thursday, April 10, 2014

VITENDO VYA MAPENZI YA JINSIA MOJA VINAPINGWA SANA KATIKA MATAIFA YA AFRIKA.



Serikali ya Tanzania imefutilia mbali usajili wa shirika moja lisilokuwa la kiserikali kwa sababu ya kuhamasisha mapenzi ya jinsia moja katika jamii.

Shirika hilo kwa jina Sisi Kwa Sisi lilisajiliwa baada ya kudai kuwa malengo yake yalikuwa ni kusaidia jamii.
Tanzania imesema imechukua hatua ya kufutilia mbali usajili wa shirika hilo kwa kukiuka sheria za nchi na kwenda kinyume na malengo ya usajili wake.

Mkurugenzi wa usajili wa mashirika yasiyo ya Kiserikali nchini Tanzania, Maseli Katemba, amesema kuwa shirika hilo la Sisi kwa Sisi limekiuka malengo yake ya awali ya kuwapa elimu na misaada ya kifedha wananchi lakini mambo yakawa tofauti.
"Baada ya kufuatilia tumegundua kuwa sasa wanatilia mkazo kuwasaidia watu wa jinsia moja," alisema Bwana Katemba.

Bwana Katemba amesema kuwa Serikali itaendelea na kuyasaka makundi mengine kama hayo ambayo yanaendesha maswala yaliyo kinyume na sheria za Tanzania.

Je Tanzania tuna sheria ya kupinga mapenzi ya jinsia moja?
 
Source: BBC

KAMA VITA IMEFIKIA HAPA, WAJUMBE WA TUME YA KATIBA WAJIHADHARI!

Tovuti ya tume ya katiba ionekanavyo baada ya kufungiwa na serikali

Serikali isiyo na soni. Imefunga tovuti ya tume ya mabadiliko ya katiba, eti lengo kuu ni kuhakikisha wananchi hawapati rejea na nyaraka mbalimbali ambazo zinaweza kusaidia uelewa na ufahamu wao. Sababu ya serikali ni kuwa, kazi ya tume imekwisha hivyo na tovuto yake haina kazi!!!!!!!!!

Serikali inayoogopa wananchi wake wasiendelee kuelimika, kujielimisha na kufahamu mambo muhimu ya nchi ni serikali ya ajabu sana.

Tovuti ni maktaba za kielektroniki, tume ya katiba ya Kenya hadi leo tovuti yao ipo hewani, tume ya katiba ya Ghana hadi leo inafanya kazi, ya Afrika ya kusini hadi sasa iko hewani baada ya miaka mingi ya kutunga katiba ya taifa hilo mara baada ya Madiba kuingia madarakani.

Hapa Tanzania, serikali iloituma tume kukusanya maoni ya wananchi sasa imekasirika, kwa hiyo inayapiga vita maoni ya wananchi, inaipiga vita tume ya mabadiliko ya katiba.

Serikali nyingi za kiafrika zina rekodi mbaya mno kila inapotokea matakwa yake fulani yamezuiwa na na watu fulani kwa njia halali.

Kwa chuki hizi za waziwazi dhidi ya tume na Wajumbe wa tume ya mabadiliko ya katiba, natoa wito kwa wajumbe hao kuwa makini na nyendo zao na kutojiamini sana.

Ikumbukwe nchi hii watu wamewahi kung'olewa macho na wengine meno na vyombo vya dola viliishia kukamata wendawazimu na kuwapa mashtaka huku wahusika halisi waliotumwa kufanya kazi hizo za kinyama kwa maslahi tusiyoyajua wakitamba mitaani hadi leo.

Nasisitiza kuwa, ikiwa serikali ya kiafrika inafunga hadi tovuti yenye taarifa za maoni ya wananchi iliyokuwa wazi kwa umma, ni muhimu wajumbe wa tume wakajichunga sana. Mimi siiamini sana serikali hii ambayo leo inaweza kukutuma kazi na kesho asubuhi ikakugeuka na kukupiga vita wewe na kazi uliyoifanya.

Haya ni maoni na mtizamo wangu binafsi. Inatosha tu kuheshimu mawazo ya kila mtu.

By Julius Mtatiro, 
Mjumbe wa Bunge la Katiba,
Dodoma
09/04/2014

Friday, April 4, 2014

PROPAGANDA YA KATIBA MPYA: UFISADI WA CCM




HAPO mwanzo, wakati Tanganyika inapata uhuru kulikuwapo na chama cha ukombozi wa Waafrika wa Tanganyika (TANU) ambacho kiliweza kuwaunganisha wananchi! Baadaye, TANU iliungana na ASP kuunda Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kwa falsafa yake kiliamua kuandaa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Katiba ya 1977 iliipa CCM haki ya kipekee ya kushika hatamu za uongozi (kama ilivyokuwa kwenye Ibara ya 10 ya Katiba ya JMT, 1977).

Katiba ya 1965 na ya 1977, TANU kwa upande wa Tanganyika ilijipendelea na haikuruhusu maoni ya wananchi isipokuwa ilichukua mamlaka wa watu na kuyafanya kuwa sehemu ya itikadi ya chama kwa madai ya kuwashirikisha wakulima na wafanyakazi.

Kwa upande wa Zanzibar, baada ya mapinduzi ya Januari 11 na 12, 1964 vyama vyote vya siasa vilipigwa marufuku na ASP iliendesha nchi kwa kutumia mawazo na maoni ya watu 14 (maarufu kama, Baraza la Watu 14 au Baraza la Mapinduzi). Fikra za watu wawili (Nyerere na Karume) zilitawala fikra za wananchi wote wa Tanzania!

Mwaka 1977, kama kawaida ya vyama vinavyopora uhuru, haki na usawa wa wananchi kwa muundo wa chama kushika hatamu, CCM ilijipa haki za kipekee (exclusive rights) za kutawala na kwa kutumia katiba iliyotungwa kukidhi utashi huo iliendelea kufaidi haki za kipekee kwa muda mrefu hata sasa!

Japokuwa CCM ilifanya ufisadi mkubwa kwenye mfumo wa serikali zake (ya muungano na ya mapinduzi), jambo kubwa lililowekwa na CCM kwenye Katiba ya 1977 ni nafasi ya kipekee ya kuongoza mabadiliko!

Mkakati wa kujipa mamlaka ya kipekee katika kufikia mujtamaa wa watu kwa uhuru, haki na usawa ulikuwa ufisadi wa kutisha ambao CCM imeendelea kuutumia hata wakati huu nchi inapotarajia kuandika Katiba Mpya!

Kazi ya kuandika katiba ya wananchi ni kazi ngumu kama kuna mikingamo inayotokana na ufisadi wa kimfumo na wa kimuundo uliyojengwa kwa miaka mingi na chama kinachoongoza kwa propaganda, hila, mizengwe, woga na ukiritimba wa kisiasa!

CCM imejenga mazingira ya kutumia uongo wa kimasilahi na kuwafanya wanachama wake waamini kila chama hicho kinachoamini na kukitetea! Tazama, wakati lilipofanyiwa upitizi Azimio la Arusha, mwenyekiti wa wakati huo, Ali Hassan Mwinyi alisema: Azimio la Arusha, kama tunavyojua, limetangazwa mwaka 1967. Hii leo tuko katika mwaka 1991.

Imepita miaka mingi, zaidi ya 20 tangu kutangazwa kwa Azimio la Arusha. Na katika kipindi cha miaka 20 yametokea mabadiliko mengi duniani na pia katika hali ya maisha yetu (rejea hotuba ya Februari,25, 1992, Diamond Jubilee, Dar es Salaam).

Hotuba ya mzee Ali Hassan Mwinyi, ililenga katika kuonesha mabadiliko yaliyotokea na yanayohitaji mabadiliko katika kufanya upitizi wa marekebisho ya Azimio la Arusha ili kwenda na wakati!

Inashangaza, CCM iliona busara kubadilisha falsafa ya kuendesha Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kwa kubadilisha baadhi ya miiko na maadili ya uongozi wa umma kwa kuzingatia mabadiliko ya wakati. Huku ikisisitizwa kwamba, ‘kila zama na kitabu chake.’

WANAMTANDAO WA CCM WAMEKULA NYAMA YA MTU




VITA ya urais mwaka 2015 ndani ya chama tawala – CCM, inatajwa kuwa ngumu na kutabiriwa kwamba inaweza kukiathiri kutokana na tabia ya uhasama inayojengeka siku hadi siku.

Inatabiriwa kwamba kuna kila dalili za CCM kupasuka vipande vipande kama tabia ya siasa za fitna na kupakana matope zitaachwa ziendelee kuimomonyoa.
Baadhi ya wanasiasa wanajiona kuwa na haki ya kucheza rafu na kuchafua wenzao kwa gharama zozote ili mradi waonekane hawafai kupitishwa na chama hicho kugombea urais wa mwaka 2015.

Mizizi ya siasa chafu za kupakana matope ina kina kirefu ndani ya CCM na haijaanza juzi, bali ni staili iliyotumiwa na kundi maarufu la mtandao lililomwingiza Rais Jakaya Kikwete madarakani mwaka 2005.

Wapo wanasiasa ambao hadi sasa wanaugulia majeraha yaliyosababishwa kwa makusudi na kundi la mtandao mwaka 2005 kwa lengo la kuhakikisha kwamba hawapati nafasi ya kuteuliwa kuwa wagombea wa nafasi ya urais kwenye mchuano huo uliokuwa na wagombea 11.

Walioumizwa na wanaodaiwa kuendelea kuwekewa macho mawili mawili hadi leo ni wale walioonekana kuwa na ushawishi na nafasi pana ambayo kwa njia moja au nyingine iliibua hofu kubwa kwa kundi hilo na mgombea wao kwa kuamini kwamba wangekuwa kikwazo kikubwa kwao kukidhi malengo yao.

Chini ya kundi hilo, tuliona kashfa mbalimbali zikiwaandama wanasiasa waliokuwa na majina makubwa kwa kuibuliwa mambo yasiyo na vichwa wala miguu.

Katika hili CCM imejiwekea ‘laana’ ambayo lazima itakuja kukigharimu chama hicho, kwani uchafu huo ulipokuwa ukifanyika, chama kilifumbia macho na kujifanya kwamba hakioni wakati wanachama wake wakiumizwa na kundi hilo na chama kukaa kimya bila kutoa tamko lolote.

Baadhi ya vyombo vya habari viligeuka kuwa wakala namba moja wa kundi la mtandao kwa kuhakikisha vinapeleka ujumbe hasi kwa wananchi dhidi ya wagombea walioonekana kuwa tishio kwa kundi hilo la mtandao.

Tuliona namna aliyewahi kuwa  Waziri Mkuu na Katibu wa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU, sasa AU), Dk. Salim Ahmed Salim alivyoandamwa kila kona kuanzia maisha yake binafsi  kwa kudaiwa kumdhulumu na kumnyima haki zake mmoja wa watu waliokuwa wasaidizi wake.

Haikuishia hapo Watanzania wakaaminishwa kwamba Dk. Salim, aliyeipatia nchi hii heshima kubwa kimataifa, si Mtanzania na ndugu zake wana vyeo vya juu huko Arabuni huku yeye akidaiwa kuwa mwanachama wa chama cha Hizbul, kilichouunga mkono utawala wa Sultani huko Zanzibar.

Hayakuishia kwa Dk. Salim, kundi hilo linaloonekana kutaka kutumia tena staili hiyo ya kupakana matope kwenye uchaguzi mkuu ujao lilimwandama aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo,  Frederick Sumaye, kwa kumpaka matope katika masuala mbalimbali likiwemo la kujilimbikizia utajiri wa matrilioni hadi kuwapora wanakijiji ardhi huko Mvomero na Kibaigwa.

Hata hivyo, muda na wakati ulibainisha ukweli wa hayo baada ya kundi hilo kupata walichotaka na ghafla  hatukusikia tena ‘uchafu’ wala  ‘wizi’ wa kina Sumaye.

Hofu na tabia za kundi hili zinatajwa kuanza kuchukua kasi tena wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu ujao. Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kuonya kuwa: “Ukila nyama ya mtu huwezi kuacha tabia hiyo, itaendelea.”

MKUU WA MILA AMPA BARAKA MGOMBEA CHADEMA CHALINZE!




WAKATI kampeni za uchaguzi mdogo Chalinze zikikaribia ukingoni kwa wapiga kura kumchagua mbunge wao siku ya Jumapili ijayo, Mkuu wa Mila wa jamii ya Wamasai wa Tanga, Morogoro na Pwani, Chifu Tiku Moreto, amempa baraka za ushindi mgombea wa CHADEMA, Mathayo Torongey, akimtaka atimize wajibu wake kwa kutenda haki kwa wote.

Katika tendo hilo lililofanyika juzi asubuhi, kwa faragha katika makazi ya kiongozi huyo wa kijadi, maeneo ya Kibaha Vijijini, kijijini Gumba, Chifu Moreto, alimfanyia dua ya kimila, kisha kumtakia kila la heri mgombea huyo, ambapo alimpatia kitu mfano wa kalamu kama ishara ya uongozi unaosimamia haki.

Kabla ya tendo hilo la kimila, kiongozi huyo wa kimila alitoa nasaha zake kwa msafara wa viongozi wa CHADEMA waliofika kijijini hapo, wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Said Issa Mohamed, ambapo Chifu Moreto alisema pia anamtakia baraka za Mungu, Torongey.

“Mimi kama kiongozi wa kimila, wote mnaogombea ni wa kwangu…yule mwenzako wa CCM naye alikuja hapa…natambua kuwa wewe ni Mmasai mwenzangu, lakini mimi kama kiongozi sina CHADEMA wala CCM, wote ninyi ni wa kwangu. Sina cha chama tawala wala upinzani. Nakutakia mafanikio mema katika uchaguzi huu.

“Ni kweli kuwa CCM imekuwa na udhaifu mwingi, ona hata hapa kwangu wanataka kupauza. Ni kwa sababu tu mimi ningali hai hapa, lakini nasema kuwa mimi kama kiongozi wa mila sina cha chama tawala wala upinzani,” alisema Chifu Moreto kupitia kwa mtafsiri wake.

CHADEMA wazungumza

Mapema akitoa nasaha za msafara wao kwa niaba ya Makamu Mwenyekiti, Mohamed, mmoja wa makamanda wa chama hicho waliofika kwa chifu huyo,  Alphonce Mawazo, alisema kuwa migogoro ya wakulima na wafugaji imekuwa ikisababishwa na uongozi mbovu, unaoweka sera zinazosababisha makundi hayo mawili kukosa haki zao za msingi.

Alisema kuwa katika maeneo mengi, wafugaji wamekuwa kama wakimbizi kwenye maeneo yao, hivyo kujikuta wakigombania ardhi ya malisho ya mifugo yao na wakulima ambao nao wanahitaji maeneo hayo kwa ajili ya kilimo.

Baba yetu chifu…mimi natoka jamii ya wafugaji kama ninyi…ingawa sisi Usukumani tunafuga na kulima pia. Sisi watu wa jamii ya wafugaji mifugo yetu ndiyo benki yetu, mifugo yetu ndiyo M-Pesa zetu, mifugo yetu ndiyo inatupatia wake, mifugo yetu ndiyo kila kitu, sasa kwa sera za CCM, chama kilichoko madarakani sasa, wafugaji miaka michache ijayo tutakosa pa kukimbilia.

“Wakati ule wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, serikali ilijali watu wake, wafugaji tuliletewa mabwana mifugo, wakulima tuliletewa mabwana shamba, leo hakuna tena mambo hayo…badala yake sera wanazotuletea ni kupunguza mifugo, sasa wanataka kuvunja kabisa benki zetu, wachukue hata kilichobaki.

“Kabla ya sera hizi mbovu walianza kwa kupora ardhi…eti leo hii serikali yetu haiwezi kutenga maeneo kwa ajili ya wakulima na wafugaji, lakini inao uwezo wa kupora ardhi kwa ajili ya kumpatia mwekezaji aliyetoka China au Marekani maelfu ya ekari, huku watu wake wakitaabika kwa kukosa ardhi ya kilimo au kufugia, baba yetu nchi hii imekuwa ya hovyo, serikali haijali watu wake tena,” alisema Mawazo.

Naye mgombea Torongey alimshukuru kiongozi wake wa kimila kwa baraka na heri alizomtakia kwenye uchaguzi, akikubali maagizo aliyopewa ya kuwatumikia wananchi wote kwa haki, bila kuwabagua.

JAJI WARIOBA AVUNJA UKIMYA!


Mwenyekiti wa Tume ya mabadiliko ya katiba Jaji Warioba.

SIKU moja baada ya Ikulu ya Rais Jakaya Kikwete kutoa taarifa ya kejeli na kumsuta Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, mwenyekiti huyo naye ameibuka kujibu mapigo.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Jaji Warioba alisema ameiona taarifa ya serikali kuhusu Tume ya Mabadiliko ya Katiba, lakini ameshangazwa na maudhui na lugha iliyotumiwa na Ikulu dhidi yake.

Majibu ya Jaji Warioba kwa Ikulu ya Rais Kikwete, yalitokana na taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ambayo ilimwita Jaji Warioba  mnafiki kwa kujifanya hajui ukomo wa tume yake.

Ikulu ilitoa taarifa hiyo baada ya gazeti moja juzi kumkariri Jaji Warioba akidai kuwa tume yake ilifukuzwa kazi na kwamba haikupewa muda wa kuandaa na kuwasilisha nyaraka za kukabidhi ofisi na madaraka na kwamba wajumbe wa tume hiyo waliporwa magari ambayo yamewekwa Ikulu.

Akitoa ufafanuzi wa taarifa ya Ikulu ya juzi, katika taarifa hiyo, Warioba alifafanua hivi:

“Kwanza, tume iliwaheshimu sana waheshimiwa marais wetu. Mafanikio ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba yametokana na jinsi Mheshimiwa Rais wa Jamhuri na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar  walivyoiunga mkono na kuisaidia tume. Milango yao ilikuwa wazi wakati wote. Wakati wowote mimi kama mwenyekiti nilipoomba kuonana nao nilipata nafasi haraka na tume ilipoomba chochote, pamoja na kuongezewa muda hawakusita. Na wakati wote hawakutoa shinikizo la aina yoyote.  Makatibu wakuu viongozi nao waliisaidia tume kwa kiwango hicho. Heshima yangu na wenzangu kwa waheshimiwa marais na makatibu wakuu viongozi ni kubwa.

“Pili, tume ilikuwa haijamaliza kazi yake wakati inakabidhi ripoti kwa Mheshimiwa Rais. Tume iliendelea na kazi ya kuandaa Randama ya Rasimu, Bango Kitita la Rasimu na maelezo niliyotoa kwenye Bunge Maalumu. Serikali ilijua tulikuwa tunafanya kazi hiyo na nyaraka hizo zilikabidhiwa bungeni siku ya kuwasilisha Rasimu.

Tatu, wajumbe wa tume hawajatoa madai ya kulipwa shilingi milioni mia mbili. Hakuna mjumbe yeyote aliyetoa dai kama hilo na serikali inajua,” alisema Jaji Warioba.

Alisema alichozungumza ni muda wa kuandaa makabidhiano na kuandaa safari ya wajumbe kurudi makwao. Alisema aliwasilisha rasimu Machi 18, 2014, tume ilivunjwa Machi 19, 2014 wakati wajumbe wako Dodoma.