Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba
|
Jana
gazeti la Mwananchi lilichapisha habari
katika ukurasa wa kwanza ikisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeomba
kuongezewa muda wa mwezi mmoja kutokana na ugumu wa kazi ya uchambuzi wa maoni
yaliyotolewa na wananchi na asasi mbalimbali. Kama mambo yangekwenda kama
ilivyotarajiwa hapo awali, Tume hiyo iliyoanza kazi Mei 1 mwaka jana, chini ya
Jaji Joseph Warioba ingekamilisha kazi yake Novemba 1, mwaka huu.
Kwa
mujibu wa Sura ya 83 ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Tume hiyo ilitakiwa
kufanya kazi kwa miezi 18. Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji
Augustino Ramadhan alisema juzi kwamba wamepeleka serikalini ombi la kuongezewa
muda wa kufanya kazi kutokana na kukabiliwa na kazi ya ziada ya kuchambua maoni
hayo. Pamoja na Serikali kukiri kupokea ombi hilo, hadi tunakwenda mitamboni
jana ilikuwa haijatoa jibu la kulikubali wala kulikataa.
Sisi
hatuoni sababu yoyote inayoweza kuisukuma Serikali kulikataa ombi hilo, hasa
kutokana na kujitokeza kwa mambo mengi ambayo hayakutarajiwa kabla na wakati wa
mchakato wa Katiba Mpya. Mikutano ya Mabaraza ya Katiba iliyofanyika nchi
nzima, kwa mfano ilizua tafrani kubwa ambapo wajumbe wa mabaraza hayo
waligawanyika kwa misingi ya kisiasa na kiitikadi. Tume hiyo ililazimika
kutumia muda mwingi kujielekeza katika kutoa tafsiri na kufafanua vifungu
katika Rasimu ya Kwanza ya Katiba. Pia Tume ilitumia muda mrefu kuratibu
mijadala ya Rasimu hiyo, kwani wajumbe wengi wa mabaraza hayo walikuwa
wakijadili hoja zilizotokana na misimamo ya vyama vyao badala ya kujadili
rasimu yenyewe.
Hivyo,
Serikali haina budi kukubali ombi hilo la tume haraka iwezekanavyo, pamoja na
ukweli kwamba kuiongezea tume mwezi mmoja kuchambua maoni ya wananchi na asasi
mbalimbali ni kuongeza gharama za mchakato huo. Lakini, wahenga waliposema maji
ukiyavulia nguo ni sharti uyaoge, walipatia kabisa usemi huo, kwani kama
tumeamua kama taifa kupata Katiba Mpya itakayotuvusha miaka 50 mingine ijayo
lazima tubebe gharama hizo za kutuletea demokrasia ya kweli.
Ni
vyema tukatambua kwamba hatua ya tume ya kuomba kuongezewa mwezi mmoja siyo ya
ajabu. Sheria inaipa tume hiyo fursa ya kuongezewa miezi miwili nje ya muda
uliowekwa. Kinachotakiwa sasa ni Serikali kujipanga vizuri na kutekeleza mambo
mbalimbali kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2015. Mambo hayo ni pamoja
na kuandaa, kurekebisha na kupitisha sheria mbalimbali kwa lengo la kuondoa
sheria kandamizi na kuweka sheria zitakazowezesha kuwapo mazingira linganifu ya
ushindani wa kisiasa. Kwa mfano, inahitajika sheria mpya ya Tume Huru ya
Uchaguzi.
Moja
ya mambo muhimu ambayo Serikali inapata kigugumizi kuyatolea uamuzi ni suala la
kufanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa sambamba na Uchaguzi Mkuu wa 2015. Muda
uliobaki kati ya sasa na 2014 (ambao ulipangwa kufanyika) hautoshi kufanya
maandalizi na uchaguzi ulio huru na haki. Uchaguzi huo ni vyema usimamiwe na
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. Hivyo, Tamisemi iliyokuwa ikisimamia chaguzi za
Serikali za Mitaa na kusababisha malalamiko mengi kutoka kwa wananchi itakuwa
imeondolewa mzigo huo mzito. Kufanya uchaguzi huo wakati mmoja na Uchaguzi Mkuu
kutapunguza gharama kwa kiasi kikubwa kama ilivyo katika nchi nyingi barani
Afrika na kwingineko.