To Chat with me click here

Monday, October 7, 2013

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI




Ofisi ya Rais, Ikulu, imeanza mawasiliano na viongozi wa vyama vya siasa nchini vyenye hoja kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uliopitishwa karibuni na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nia ya kuandaa mkutano kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na viongozi wa vyama hivyo.

Mawasiliano hayo yameanza leo, Jumatatu, Oktoba 7, 2013, kufuatia maelekezo ya Rais Kikwete kwa Ofisi ya Katibu wa Rais.

Kufuatia matukio yaliyotokea Bungeni wakati wa kujadiliwa na kupitishwa kwa Muswada huo mwezi uliopita, na maneno na kauli mbali mbali ambazo zimetolewa na wabunge wa vyama vya upinzani na wadau wengine kufuatia kupitishwa kwa Muswada huo na Bunge, Rais Kikwete katika hotuba yake kwa wananchi Ijumaa iliyopita, Oktoba 4, 2013, alisema kuwa hoja na kauli za wanaopinga Muswada huo zinazungumzika kwa nia njema ya kutafuta mwafaka katika mchakato wa kutafuta Katiba Mpya.

Kwa mujibu wa maandalizi hayo, Ofisi ya Rais, Ikulu inaangalia uwezekano wa kuitisha mkutano huo Jumapili ya Oktoba 13 ama Jumanne ya Oktoba 15, mwaka huu.



Leo, Jumatatu, Oktoba 7, 2013, zimetungwa habari, zikaingizwa kwenye Mitandao ya Kijamii na kusambazwa sana zikidai kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametia saini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambao ulipitishwa na Bunge katika Kikao chake cha mwezi uliopita.

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu inapenda kufafanua kama ifuatavyo:

a) Kwanza, Ofisi ya Rais, Ikulu haijapokea Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Inawezekana Muswada huo umekwishakutumwa kutoka Bungeni lakini haujamfikia Mheshimiwa Rais. Hivyo, kama haujamfikia, Mhe. Rais hawezi akawa ameutia saini

b) Pili, Muswada huo ukimfikia Mheshimiwa Rais, inatarajiwa kuwa atautia saini kwa sababu Muswada huo umepitia katika mchakato sahihi na halali wa Kikatiba kwa maana ya kufikishwa Bungeni na Serikali, Kujadiliwa na hatimaye kupitishwa na Bunge.

c) Tatu, kama yapo marekebisho ambayo yanaonekana yanafaa kufanywa katika Sheria hiyo, basi yatafanywa na Bunge baada ya Mhe. Rais kuwa ametimiza matakwa ya Kikatiba ya kutia saini Muswada ambao umepitishwa na Bunge kwa kufuatia mchakato sahihi na halali wa Kikatiba.

d) Nne, na wala hii haitakuwa mara ya kwanza kwa Sheria kupitishwa na Bunge, ikatiwa saini na Mhe. Rais na baadaye kufanyiwa marekebisho na Bunge baada ya kuonekana umuhimu wa kufanya marekebisho hayo. Mwishoni mwa mwaka 2012, Sheria ya Marekebisho ya Katiba ilipitia njia hiyo.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.

7 Oktoba, 2013

No comments:

Post a Comment