JESHI
la Polisi Makao Makuu limeendelea kumshikilia kwa siku 11 bila kumfikisha
mahakamani Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) mjini Bukoba,
Evodius Justinian (30) huku ndugu zake wakizuiliwa kumpa chakula isipokuwa maji
tu.
Justinian
alishikiliwa mjini Bukoba Aprili 2, mwaka huu kisha kusafirishwa hadi jijini
Mwanza na kuhojiwa, kisha Dar es Salaam huku akipewa mateso makali ya
kulazimishwa akubali kuhusika kutengeneza video inayomhusisha na uchochezi
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare.
Awali
ndugu zake na viongozi wa CHADEMA mjini Bukoba walielezwa na polisi kuwa
Justinian anasafirisha kwenda wilayani Igunga, Tabora ambako alidaiwa kuwa
alitenda makosa ya jinai, lakini alifichwa jijini Mwanza.
Wakizungumza
na gazeti hili, mawakili wa mtuhumiwa huyo Nyaronyo Kicheere na Peter Kibatala
walisema kuwa juzi jioni ndugu zake walimpelekea chakula, lakini walipofika
waliambiwa kuwa haruhusiwi chakula isipokuwa maji tu.
“Asubuhi
alipelekewa chai, lakini polisi walidai kuwa ndugu walichelewa na hivyo
kuwazuia. Na walipopeleka chakula cha mchana waliambiwa hayupo kwani alikuwa
amepelekwa hospitali bila kuitaja kwa jina,” alisema Kicheere.
Kicheere
aliongeza kuwa baada ya ndugu kuwapa taarifa hiyo, yeye na wakili mwenzake
Kibatala walilazimika kuondoka mahakamani Kisutu walipokuwa wakimsubiri mteja
wao afikishwe. Mawakili
hao walisema wanakusudua wakati wowote kupeleka maombi Mahakama Kuu kudai
polisi wapeleke mwili wa mtuhumiwa mahakamani (habeas corpus).
Lakini
pia mawakili hao walisema kuwa leo wataendelea kushinda mahakamani muda wote wa
kazi kumsubiri mteja wao. Waliwataka
Watanzania wakiwemo wanasheria na watetezi wa haki za binadamu kuendelea kupiga
kelele dhidi ya Jeshi la Polisi linavyokiuka haki za binadamu.
Akizungumzia
hatua ya mtuhumiwa huyo kutofikishwa mahakamani kama ilivyokuwa imeahidiwa,
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso alisema wakiwa tayari watasema na
kuomba watu wasiingilie kazi yao.
“Tutasema
siku ya kumfikisha, hapa suala la msingi ni polisi tunafanya nini, ni kama wewe
unavyoandika habari, hakuna wa kukuuliza,” alisema Senso.
Alipoelezwa
juu sheria inavyotaka mtuhumiwa kufikishwa mahakamani ndani ya saa 24 baada ya
kukamatwa, Senso alisema pasipo kufafanua kuwa sheria hiyo hiyo inaweza
kutumika vinginevyo. Jumatatu
wiki hii, mbele ya wakili wake Kicheere, mtuhumiwa huyo alieleza unyama
aliofanyiwa na jeshi hilo wakati wote wa mahojiano mkoani Mwanza na jijini
hapa.
Katika
maelezo yake yaliyoshuhudiwa na Ofisa wa Polisi Makao Makuu, Advocate Nyombi,
Justinian alisema kuwa baada ya kutolewa mjini Bukoba kwa siri bila ndugu zake
kujua, alipelekwa jijini Mwanza na kuhojiwa bila kuruhusiwa kuonana na wakili
wake. Alieleza
kuwa wakati wote wa mahojiano hayo alikuwa akilazimishwa kukiri kurekodi video
ya Lwakatare inayoonesha mikakati ya ugaidi.
Alisema
alisafirishwa kwa siri kwa ndege hadi Dar es Salaam, akapelekwa chooni na
kupigwa, kutishiwa na kuteswa kwa nyaya za umeme na kunyimwa fursa ya kupewa
chakula.
“Nimepigwa
na polisi nikiwa Mwanza, nikiwa chooni Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam wakati
naletwa huku, polisi wakaniambia mimi ni mtu hatari sana, niseme nilifanya nini
Igunga. “Nikiwa
Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam niliomba kwenda chooni, waliingia pamoja na
mimi wakanipiga sana, nimeshaandika maelezo kwa kulazimishwa, niliomba kuwa na
wakili wakanikatalia,” alisema.
Aliongeza
kuwa akiwa Dar es Salaam alihojiwa aseme ukweli kuhusu video ya Lwakatare.
Akawajibu kuwa ilifanyiwa uhariri na Ludovick, lakini akapigwa makofi na askari
wakaagiza nyaya za umeme za kutesea.
“Waliposema
kuleta nyaya za umeme, kwa kuhofia mateso ya umeme nikasema hii video ni
yangu,” alisema.
Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment