SAKATA la Mkurugenzi wa Ulinzi na
Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare na
Ludovick Rwezaula kushtakiwa kwa makosa ya ugaidi, limeibua mvutano mkali
bungeni huku wabunge wakishambuliana kwa maneno makali.
Mvutano huo uliibuka jana wakati wa
kujadili hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2013/2014
ambapo Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM) alichafua hewa wakati
akichangia na kudai kuwa aliyerekodi video ya Lwakatare yupo tayari kuja
kutoa ushahidi.
Mwigulu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu
wa CCM (Bara) aliliambia Bunge kuwa CHADEMA wasihangaike kujitetea kwa swala la
Lwakatare kwani ushahidi wote kuhusu video hiyo upo na kwamba yuko tayari
kuutoa bungeni, duniani na mbinguni.
“Nataka nitoe ufafanuzi kuhusu suala la
ugaidi ambalo Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amezungumza kwenye hotuba
yake hapa bungeni jana. Aliyerekodi mkanda yupo na mimi niko tayari kuhojiwa
popote hata mbinguni,” alisema Mwigulu na kuibua nderemo kutoka kwa wabunge wa
CCM.
Mwigulu alionyesha karatasi aliyodai
kuwa ilitumiwa na Lwakatare kupanga kile alichodai kuwa ni mkakati wa mauaji
akisema huo ndiyo mkakati wa CHADEMA kupanga mauaji na kwamba viongozi wakuu wa
chama hicho wanapaswa kushtakiwa.
Bila kujali kwamba suala hilo liko
mahakamani wala ni kinyume cha kanuni za Bunge kumtaja mbunge mwingine kwa jina
akimtuhumu, Mwigulu alisema anaishangaa CHADEMA kumtaka yeye aunganishwe kwenye
kesi kwa kuwa na mawasiliano na mmoja wa watuhumiwa wakati hata wao wana
mawasiliano na Lwakatare.
“Alisema Mbowe hapa jana kuwa mimi
napaswa kushtakiwa kwa ugaidi, ingawa simuoni hapa ndani labda tayari
amekwishakamatwa na polisi, lakini nataka kusema kuwa watu hawa ni waongo na
wanafiki. Wanapanga mauaji halafu wanakuja hapa kuwahadaa wananchi kuwa
wanapinga ugaidi,” alidai.
Hatua hiyo ya Mwigulu kumtaja Mbowe kwa
jina na chama chake kuwa ni magaidi, iliwashtua baadhi ya wabunge wakishangaa
kuona Spika wa Bunge, Anne Makinda akishindwa kutumia kanuni kumbana na kumtaka
afute kauli ana atoe uthibitisho.
Baada ya kuona Makinda anakuwa na
kigugumizi, baadhi ya wabunge wa CHADEMA, Joseph Selasini (Rombo), Mustafa
Akunaay (Mbulu), Pauline Gekul (Viti Maalumu) walijaribu kusimama kuomba
mwongozo lakini walikataliwa.
Spika Makinda ambaye alionekana
kukitetea chama chake cha CCM alitumia mafumbo kuwajibu wabunge wa CHADEMA
akiwataka kuacha tabia ya mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu.
“Jana Kiongozi wa Kambi ya Upinzani,
Freeman Mbowe alizungumzia suala la ugaidi na kesi iliyopo mahakamani, hakuzuiliwa.
Leo mnamzuia Mwigulu. Kama ni kanuni ziwe kwa wote si mkuki kwa nguruwe halafu
kwa wengine...,” alisema.
Baada ya Mwigulu kuchangia ndipo Mbunge
wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA) alipata nafasi ya kuchangia hotuba
ya Waziri Mkuu na kuzungumzia maeneo matatu ya elimu, usalama wa nchi na katiba
mpya.
Katika suala la usalama, Lissu
alijielekeza moja kwa moja kupangua makombora ya Mwigulu bila kumtaja kwa jina,
akisema Jeshi la Polisi limekuwa na mawasiliano na baadhi ya watu ndani ya
Bunge kufanya vitendo vya kigaidi na kuwapakazia watu wengine.
“Kwa muda mrefu Jeshi la Polisi
limekuwa likituhumiwa kufanya vitendo vya uhalifu na kushirikiana na watu humu
ndani kupanga vitendo vya kigaidi na kuwasingizia watu wasio na hatia. Hii
haikubaliki,” alisema Lissu.
Lissu alisema kuwa mmoja wa watuhumiwa
wa ugaidi wanaoendelea kushikiliwa mahabusu amekuwa akifanya mawasiliano
ya simu na mmoja kati ya wabunge kupanga njama za ugaidi na kuwabambikia watu
wasio na hatia.
Alienda mbali kwa kusema kuwa kiongozi
huyo ambaye yumo ndani ya Bunge, alituma pesa kwa njia ya simu kwa mmoja wa
watuhumiwa hao wa ugaidi kwa ajili ya kupanga ugaidi.
Wakati akiendelea na hotuba yake,
Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah (CCM) aliomba mwongozo wa Spika kuhoji
kama Lissu ana ushahidi wa mambo anayosema. Alipotakiwa na Spika kujibu
swali hilo, Lissu alisema mawasiliano ya kwanza kati ya kiongozi huyo na
mtuhumiwa mmoja wa ugaidi, yalifanyika Januari 24 mwaka jana.
“Mawasiliano ya pili yalifanyika
Desemba mwaka jana ambapo kiongozi huyo alituma pesa kwa mtuhumiwa huyo.
Mheshimiwa Spika tuna ushahidi wa kutosha kuhusu hilo,” alisema Lissu.
Hata hivyo, hatua ya Spika kukatiza
hotuba ya Lissu na kumpatia nafasi Abdallah kuomba mwongozo ililalamikiwa na
wabunge wa upinzani ambapo wengine walikuwa wakizomea na kudai kuwa anapendelea.
Lissu aliendelea na mchango wake akisema “sheria ya ugaidi inasema anayetoa
fedha kufadhili ugaidi naye ni gaidi, akamatwe, afungwe.”
Mbali ya kuzungumzia suala hilo la
ugaidi, Lissu alisisitiza kauli ya Mbowe juzi kuwa CHADEMA haitashiriki kwenye
mchakato wa katiba kama kasoro zilizoainishwa hazitarekebishwa. Alisema CHADEMA
ikijitoa haitabaki kimya, bali itazunguka nchi nzima kuwataka wananchi
kutoipigia kura ya ndiyo.
Lissu alisema Kenya na Zimbabwe
zilishamwaga damu kutokana na katiba na kuitahadharisha serikali kuwa makini na
mchakato huo. Pia alijadili suala la elimu akisema kuwa sasa ni wakati wa
kuwajibishana na sio kutafuta mchawi.
“Waziri Mkuu amesema kwenye hotuba yake
juzi kwamba tusitafute mchawi wala sio wakati wa kulaumiana. Mimi nakubali
kwamba huo si wakati wa kulaumiana bali wa kuwajibishana,” alisema Lissu.
Alionesha ripoti ya serikali ya mwaka
2010 iliyochunguza chanzo cha kufeli kwa matokeo ya kidato cha nne, lakini
haijafanyiwa kazi wala haijatangazwa hadharani. “Ripoti hii Waziri Mkuu
anaijua, hajaifanyia kazi, leo ameunda tume nyingine. CHADEMA tunasema Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi afukuzwe, Waziri Mkuu afukuzwe, wameshindwa
kazi,” alisema.
Alisema kama rais hataki kumwajibisha,
Bunge lipige kura ya kutokuwa na imani naye. Baada ya Lissu kumaliza kujadili
hoja hiyo, Spika Makinda aliitaka Kamati ya Kanuni kukutana kwa dharura
kujadili ukiukwaji huo wa kanuni mpya walizojiwekea, na hivyo kufikia hatua ya
wabunge kujadili jambo lililoko mahakamani.
No comments:
Post a Comment