Dar es Salaam.
Serikali
imepoteza zaidi ya Sh362.9 bilioni kutokana na baadhi ya kashfa kubwa za
ufisadi na operesheni mbalimbali zilizoligharimu taifa tangu uhuru.
Uchunguzi
wa gazeti hili umebaini taifa kukumbwa na kashfa mbalimbali za upotevu wa fedha
au kuanzisha mipango ambayo utekelezaji wake ulisababisha maumivu kwa wananchi
na hakuna awamu ya uongozi wa Serikali iliyokwepa hali hiyo.
Kuanzia
awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere aliyeiongoza nchi toka mwaka 1961
ilipopata uhuru hadi 1986, Rais Ali Hassan Mwinyi (1986-1995), Rais Benjamin
Mkapa (1995-2005) na Rais Jakaya Kikwete (2005-hadi sasa), kumeibuka kashfa
mbalimbali, saba zikiwa kubwa na kulitikisa taifa.
Kashfa
na operesheni saba kubwa zilizotikisa taifa ni pamoja na Operesheni Uhujumu
Uchumi, ufisadi katika Mfuko wa Kuwezesha Uagizaji Bidhaa kutoka Nje ya Nchi
(Commodity Import Support – CIS) na Kashfa ya Rada.
Nyingine
ni ufisadi Akaunti ya EPA, kashfa ya Richmond, Operesheni Tokomeza Ujangili na
ile ya uchotaji mabilioni katika akaunti ya Escrow.
Operesheni
Uhujumu Uchumi
Mwaka
1984 Serikali ilianzisha Operesheni Uhujumu Uchumi, iliyoongozwa na Waziri Mkuu
wa wakati huo, Edward Sokoine ili kutaifisha mali ambazo baadhi ya watu walidaiwa
kujipatia kwa njia isiyo halali.
Operesheni
hiyo ilishuhudia baadhi ya watuhumiwa wakimwaga fedha mitaani na majalalani,
huku wengine wakitupa mali kuhofia kutiwa kwenye mkono wa sheria.
Hata
hivyo, katika operesheni hiyo baadhi ya watendaji wa Serikali ambao hawakuwa
waaminifu, waliitumia nafasi hiyo vibaya kutaifisha mali za baadhi ya watu,
ambao hawakuwa wahujumu uchumi.
Zoezi
hilo lilisababisha wananchi kadhaa hasa vijijini kuwekwa ndani na wengine
kuachwa maskini baada ya kunyang’anywa mali zao ikiwamo mifugo na mashine za
kusaga nafaka, kwa kudaiwa kuwa walizipata kwa njia isiyo halali.
Mfuko
wa Commodity Import Support (CIS)
Miaka
24 baadaye yaani mwaka 2008, liliibuka sakata jingine lililokuwa na harufu
kubwa ya ufisadi wa mabilioni katika Mfuko wa Kuwezesha Uagizaji Bidhaa kutoka
Nje ya Nchi (Commodity Import Support – CIS).
Sakata
hilo liliwahusisha baadhi ya wanasiasa, wafanyabiashara maarufu nchini na
wizara kadhaa za Serikali ya Muungano na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ). Kupitia
mfuko huo, vigogo hao walichota zaidi ya Sh200 bilioni kwa kivuli cha uagizaji
bidhaa kutoka nje ya nchi.
Mfuko
huo wa CIS, ulianzishwa katika miaka ya 1980, ambapo baadhi ya nchi wafadhili
ikiwamo Japan, zililenga kuipatia Tanzania fedha za kigeni za kununulia malighafi,
vyombo vya usafiri wa barabara, vifaa vya kilimo, ujenzi na vingine mbalimbali.
Mpango huo ulioanzishwa na Serikali uliendelea hadi mwanzoni mwa miaka 2000,
ambapo nchi hizo wahisani ikiwamo Japan, Uingereza, Uholanzi, Saudi Arabia,
Norway, Uswisi, Ubelgiji, Sweden na Denmark zilikuwa zikiipatia Serikali fedha
za kigeni ili kuimarisha sekta za biashara.
Wizara
zilizotajwa katika orodha ya wadeni wa CIS ni pamoja na iliyokuwa ya
Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya Kazi, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maji na
Wizara ya Mambo ya Ndani kwa Tanzania Bara, wakati Zanzibar zinatajwa Wizara ya
Mawasiliano na Uchukuzi na Wizara ya Maji.
Rada
Mwaka
2011 Serikali ilikumbwa na jinamizi la ufisadi kwa mara nyingine. Safari hii
uliibuka ufisadi wa mabilioni ya shilingi kupitia ununuzi wa rada kuukuu kutoka
Kampuni ya BAE Systems ya Uingereza. Ununuzi wa rada hiyo unatajwa kutofuata
taratibu sahihi, uliligharimu taifa Sh29.5 bilioni, wakati gharama halisi
ilikuwa Sh21 bilioni.
Serikali
ya Uingereza iliamua kurudisha fedha hizo kama chenji, huku ikisisitiza kuwa
watuhumiwa wote wa hapa nchini waliohusika na ununuzi wa rada hiyo mtumba,
washitakiwe Tanzania au Uingereza kutokana na kubainika dosari kwenye ununuzi
huo.
Wakati
Uingereza ikitaka watuhumiwa hao wafikishwe mahakamani, mtandao wa Wikileaks
unaosifika kwa kufichua siri za ndani ya mataifa mbalimbali duniani, ulibaini
kuwepo kwa harakati nchini za kutowafikisha mahakamani wahusika wa ufisadi huo.
EPA
Mwaka
2008 iliibuka kashfa nyingine ya wizi wa mabilioni katika Akaunti ya Malipo ya
Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu (BoT), ambapo vigogo kadhaa walitumia
mbinu chafu kuchota zaidi ya Sh133 bilioni katika akaunti hiyo.
Katika
wizi huo ulioitikisa nchi, wahusika walitajwa kutumia vivuli vya siasa katika
kupitisha nyaraka bila kufanyiwa uhakiki wa nyaraka hizo.