To Chat with me click here

Thursday, May 24, 2012

JE WAIJUA TANZANIA YA KESHO?

Miaka michache iliyopita tumekuwa tukishuhudia jinsi Bunge letu tukufu lilivyokuwa likihoji na kutaka kujua juu ya mikataba mibovu ambayo baadhi ya viongozi wetu wa Serikali wamekuwa wakiingia na mashirika, makapuni ya kigeni ambayo kwa mtazamo, uchambuzi na uchunguzi ambao umekuwa ukifanya na kamati, taasisi, wanaharakati na vyombo mbalimbali vikiwemo vyombo vya dola, kama vile taasisi za kuzuia na kupamba na rushwa, ripoti mbalimbali za mkaguzi mkuu wa serikali na vingine vingi, vyote kwa pamoja vimethibitisha kuwa, mikataba hiyo haina manufaa kwa wananchi wa Taifa hili, hususani walalahoi, huku ikibaki kunufaisha watendaji hao wakuu wa Serikali (Walala Kheri) na mashirika au makampuni hayo ambayo wamekuwa wakiingia nayo mikataba hiyo ya kuiifirisi nchi na Watanzania kwa ujumla wao. 

Baadhi ya mikataba kama ile ya Richmond, Kagoda, EPA, mkataba wa TRC na mingine mingi ambayo umma tumepata kuiisikia, yote imekuwa ikikwamisha kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa nchi na kuongeza kasi ya kukua kwa umasikini miongoni mwa Watanzania na kuongeza hali ngumu ya kimaisha hususani kwa wananchi wa Vijijini. Mbali na hayo tumeona na kupata kusikia juu ya uuzwaji wa mali za umma kama vile maeneo ya wazi, viwanja vya michezo na viwanja kama kile cha KIUTA na vinginevyo. Hayo vyote hufanyika kwa ajili ya manufaa ya wachache na familia zao. 

Pia Sera ya ubinafsishaji hutumika vibaya kwa ajili ya kutimiza azma hizo za kupokonya mali za Taifa kwa ajili ya kujinufaisha wenyewe. Tumesikia na kushuhudia jinsi baadhi ya wananchi wa maeneo mengi yanayochimbwa madini kulalamika kila kukicha jinsi wanavyonyanyasika kutokana na ubinafsishaji huo. Sera hiyo si mbaya na kama ikitumiwa vyema, huweza kuliletea Taifa hili maendeleo makubwa na ya kasi mno, lakini kutokana na ubinafsi wa viongozi wetu, wamekuwa wakiitumia vibaya kwa kujichumia wao wenyewe. Je kwa mwenendo huu Tanzania ambayo Mungu ameijalia karibu kila kitu mfano; Maziwa, Mito, Mbuga, Madini, Ardhi, Amani na mengi mengine itabaki kuwa kama ilivyo sasa kwa ajili ya vizazi vijavyo? Bila shaka jibu ni hapana, wakati unakuja ambapo Tanzania yetu itabaki kuwa mapango matupu na hapatakuwa tena na chochote ambacho vizazi vijavyo vitaweza kujivunia kama ilivyo kwa kizazi hiki au kama isifikavyo nje ya mipaka yake kwa sasa. 

Wataalamu na washauri wengi wa uchumi, wamekuwa wakitoa ushauri mbalimbali kwa serikali na watendaji wake kwa ujumla, juu ya ni namna gani rasilimali zetu zinafaa kutumika ili kuongeza mapato ya Taifa na hatimaye kuinua uchumi wa Taifa, lakini cha kusikitisha ni kuwa, viongozi hao na watendaji wakuu wa serikali wamekuwa wakipuuza ushauri huu na kuendeleza matendo yao ya KIFISADI. Jambo hili limezidi kurudisha nyuma maendeleo ya Mtanzania mmoja moja na Taifa kwa ujumla. 

Kulindana na kutochukuliwa hatua kwa viongozi au watendaji ambao wamekuwa wakithibitika kufanya vitendo hivyo vya hujuma na ubadhilifu kumekuwa ni jambo la kawaida kabisa, hivyo kuwafanya wananchi wengi kukosa imani na serikali yao pia na viongozi waliopo madarakani. Hili huweza kuliletea taifa madhara makubwa, hususani pale ambapo wananchi wataamua kulazimisha mabadiliko ya uongozi au utendaji kwa kutumia NGUVU YA UMMA ambayo ndiyo silaha pekee wananchi waliyobakia nayo, katika kutetea na kilinda mali za nchi yao. Kama hili likitokea tunaweza kujikuta (Watanzania) tunapoteza ili sifa ya AMANI na UTULIVYO ambayo tumekuwa nayo kwa miaka mingi sasa tangu uhuru wetu. Mbali na hilo tunaweza kusababisha kuzuka kwa wimbi kubwa la ukimbizi kwa nchi za jirani hata zaidi ya ilivyokuwa wakati ule ambapo tuliitia dosari sifa yetu ya amani pale tulipozalisha wakimbizi baada ya machafuko yale yaliyotokea kule Zanzibar wakatifulani kama mnakumbuka. Pia tutaongeza umaskini na kuyumbisha kabisa ukuaji wa uchumi ambao kwa sasa unakua kwa kusuasua kutokana na matatizo lukuki yanayolisonga Taifa letu. 

Hivyo basi, sisi wapenda maendeleo tungependa kuiasa serikali pamoja na watendaji wake wote kuwa, wakati umefika sasa kwa wao kubalisha namna ya utawala wao wa kidhalimu na kuwajibika zaidi kwa watanzania na si kwa ajili yao wenyewe. Vilevile ni vyema kuhakikisha wanalinda na kuzitekeleza sheria za nchi, ili kuepusha migongano na migogoro ambayo huweza kusababisha vurugu na machafuko ya amani yatokanayo na kutotiiwa kwa utawala wa sheria. Wale wote wanaothibitika kuvunja au kuhujumu uchumi wanapaswa kufikishwa katika vyombo vya sheria na kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake, ili kuwapa imani tena wananchi. Unyonyaji na kutumia mabavu hata pale pasipo hitaji nguvu za kiasi hicho, paepukwe na badala yake majadiliano zaidi yatumike ili kufikia muafaka. Uhuru wa kila mtu, vyama vya siasa na vyombo mbalimbali vya dola uheshimiwe, na nchi iendeshwe kwa demokrasia zaidi huku tukizingatia haki na sheria. 

Mwisho kabisa, uhuru wa kujadili na kutoa mawazo juu ya utengenezwaji wa katiba mpya kwa kila mtanzania usiingiliwe kwani ni haki ya kila mmoja kikatiba. Mchakato wa kutengeza katiba uwekwe wazi na usiharakishwe ili kukipa chama, watu au kikundi fulani manufaa kutokana na zoezi zima la kutengeneza katiba mpya. Katiba kimsingi ni sheria mama ambayo hutoa tashwira na mustakabali mzima wa maendeleo ya nchi na maisha ya wananchi kwa ujumla, hivyo mchakato usifanywe kiujanja janja kwa ajili ya kujinufaisha kwa watu wachache pekee, ila pawe na dhamira ya dhati ya kuleta mabadiliko ya Kitaifa na maendeleo kwa Jamii nzima.

Elimu juu ya zoezi zima la kutengeneza katiba, itolewe kwa kina ili kila mtanzania apate kuelewa kiundani ni nini anachopaswa kufanya (Kama vile afanyavyo, Pro. Issa Shivji, kupitia vipindi vyake vya Television - ITV). Hili litasaidia kupunguza au kuondoa kabisa minong'ono na manunguniko ya baadaye kuwa Katiba haiakisi malengo na maendeleo kwa manufaa ya watanzania wote.  Hivyo ni muhimu kuendela kuelimisha wananchi wote katika nyanja zote.


MUNGU IBARIKI TANZANIA.
    
    

No comments:

Post a Comment