To Chat with me click here

Friday, May 16, 2014

UFISADI BIL. 200 BOT: VIGOGO WAUNDA ZENGWE KUKWEPA!

Mengi, Mkono wazushiwa kumchafua Muhongo; Dk. Slaa asema ni baada ya Bunge kugeuka kichaka


MKAKATI wa kuwanasua vigogo wa serikali wanaotuhumiwa kuhusika katika kashfa nzito ya ufisadi wa dola za Marekani milioni 122 (sawa na sh bilioni 200) katika akaunti ya Baraza la Usuluhishi la Migogoro ya Kibiashara (Escrow) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), umeanza kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Waraka ambao umeandikwa na mtu anayejitambulisha kama mhasibu wa Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco), unawataja Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi na Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono, kuwa ndio wanaeneza tuhuma hizo kwa lengo la kuwachafua Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliachim Maswi.

Huu ni mnyukano unaotokana na tuhuma za Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), kuhusu vigogo sita wa serikali wakiwemo mawaziri kadhaa aliodai wamehusika na ufisadi wa fedha hizo zilizokuwa zimewekwa katika akaunti ya Escrow.

Kafulila aliwataja Waziri Muhongo na Katibu Mkuu wake, Maswi, Waziri wa Fedha Saada Mkuya, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Benno Ndullu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Mhandisi Felchesmi Mramba.

Alisema kuwa ufisadi huo ni lazima mbivu na mbichi zifahamike, na kwamba haungi mkono uamuzi wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wa kuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza suala hili kwa kuwa linagusa mamlaka kubwa katika dola, badala yake iundwe Kamati Teule ya Bunge.

Katika kile kinachoonekana kama mkakati wa kuhamisha hoja ya msingi, jana ulisambazwa waraka kwenye mitandao ya kijamii ukiwa umeandikwa kwa utaalamu wa hali ya juu ukisomeka “Sakata la IPTL mchezo wa wanasheria na wafanyabiashara”.

Mwandishi wa waraka huo anasema; “Mimi ni Mtanzania mwajiriwa wa Tanesco, kwa muda mrefu nimekuwa nikilifuatilia suala la IPTL linavyokwenda na linavyojadiliwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo bungeni.

“Naomba niwaeleze kwamba suala hili naona wengi hawalielewi, bali wanaongea kwa jazba na ushabiki kwa kitu wasichokijua kabisa na huenda labda wanatumiwa na watu wenye maslahi na Shirika letu la Tanesco,” alisema.
Alifafanua kuwa suala la Tanesco, IPTL na akaunti ya Escrow ni la kisheria zaidi na si suala la kisiasa, na kwamba tusipokuwa makini tutajikuta tunaingia katika masuala yasiyokuwa ya msingi na tukajuta baadaye.

“Mimi kama Mhasibu wa Tanesco, nakumbuka Escrow ilifunguliwa tarehe 5 July, 2006 wakati mkataba wa IPTL na Tanesco uliingiwa mwaka 1995 na lengo lake lilikuwa ni kuweka fedha za Capacity charges ambazo zilikuwa na mgogoro kutokana na Tanesco kupinga gharama hizo, lakini wakati huo huo walikuwa wakitumia umeme wa IPTL.


“Hata hivyo, IPTL tangu kuazishwa kwake ilianza kuingia kwenye mgogoro kutokana na wanahisa wenyewe kutokuelewana, sababu kubwa ikiwa ni kutokuaminiana hasa katika suala la mapato.”

Aliongeza; “Kampuni ya Merchmar iliyokuwa inamilikiwa na mwekezaji ambaye ni Rais wa Malaysia aliyekuwa na hisa asilimia 70 wakati mzawa Kampuni ya VIP Engineering aliyekuwa akimiliki hisa asilimia 30, kutokana na mgogoro huo wa kutokuelewana kwa wanahisa, Serikali ilimteua RITA mwaka 2011 kufilisi na kuuza mali zote za IPTL na baadaye kulipa madeni yanayodaiwa kampuni hiyo ya IPTL.

“Kwamba, hata hivyo bila serikali kushirikishwa huku IPTL ikielewa fika kwamba iko chini ya mfilisi, waliamua kuuza baadhi ya hisa zake kwa Benki ya Standard Chartered ya Hongkong.

“Wakati hayo yakiendelea, ghafla benki hiyo ya Standard Chartered ilifungua kesi tarehe 7 May, 2002 dhidi ya Serikali ya Tanzania bila kesi hiyo kusajiliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania.

“Kutokana na kesi hiyo kushindwa kusajiliwa Tanzania, Benki ya Standard Chatered ya Hongkong hawana mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo. Tarehe 5, Septemba 2013, hukumu ilitolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania ya kuiondoa IPTL chini ya ufilisi wa RITA.”

Waraka huo unaongeza kuwa IPTL imenunuliwa na mwekezaji mwingine ambaye ni Pan Africa Power Solution (PAP) ambaye ndiye mmiliki halali wa IPTL, na kwamba amenunua hisa zote za Merchmar asilimia 70 na 30 za VIP.
Hukumu hiyo ilitolewa na mhimili mwingine wa dola ambao ni mahakama chini ya Jaji Utamwa ambaye aliamuru mali zote za IPTL zilikabidhiwe kwa PAP.

“Vile vile katika hukumu hiyo iliamuriwa fedha zilizokuwa katika akaunti ya Escrow nazo zitolewe na walipwe haki yao IPTL. Baada ya hukumu hiyo, wizara iliandika barua ya kuomba mwongozo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali juu ya uamuzi huo, na jibu ni kwamba wizara, BoT na Tanesco walitakiwa kutii uamuzi wa mahakama na kwa vile hakuna aliye juu ya sheria,” ulisomeka waraka huo.

Pamoja na mengi yaliyotajwa mle, anatuhumiwa mwanasheria wa Tanesco, Nimrod Mkono kuwa amekuwa akitumia fedha nyingi, lakini hadi sasa Tanesco haijawahi kushinda kesi hiyo ambapo tangu mwaka 2008, alikuwa akitumia sh bilioni 10 kila mwaka na hadi kufikia mwaka 2013 alikuwa ametumia sh bilioni 52. Serikali imekwishamlipa sh bilioni 35 na zilizobaki zimelipwa na Tanesco.

“Sasa mgogoro unaoanza ni pale alipokuja Waziri Muhongo na Katibu Mkuu, Maswi ambao pamoja na kwamba wanatoka mkoa mmoja wa Mara, lakini walimpinga waziwazi bila kuficha kwamba hawapo tayari kuona akiendelea kutafuna fedha za Tanesco namna hiyo na kusisitiza kutompatia kazi hiyo tena.
“Kama watu wanaweza kufanya tathmini ya haraka au uchunguzi wa kawaida tangu mwanasheria huyu asimamishwe kufanya kazi na Tanesco, mambo mengi yamekuwa yakizushwa pasipo na maana wala msingi wowote, mbona Mkono wakati anatafuna fedha za Tanesco suala la IPTL lilikuwa kimya,” unahoji waraka huo.

Unaongeza kuwa nguvu ya suala la IPTL na kumpinga Prof. Muhongo imezidi kuongezeka pale Mengi anapodai amenyimwa kuwekeza kwenye gesi.

“Hivi nani amemnyima Mengi kuwekeza kwenye gesi? Aende akachukue fomu ya kuwekeza, mbona haendi? Yeye anachotaka ni kuwa dalali ashike vitalu halafu akatafute wawekezaji ili afaidike yeye na mke wake Jaquiline, lakini Muhongo anakataa hilo, anataka dalali wa kuwaleta wawekezaji liwe Shirika la Taifa la Mafuta (TPDC),” aliandika.

Mwandishi anaongeza kuwa; “nimemtaja Mengi kwa kuwa sisi wafanyakazi wa Tanesco tunaelewa kwamba hao wote wameungana dhidi ya Prof. Muhongo kwa kuwa wanamuona amewanyima ulaji na kuanza kupambana naye kupitia wabunge na vyombo vya habari.”

Akizungumza kwa njia ya simu kuhusu tuhuma hizo, Mkono alisema hashangazwi na ujumbe huo unaoweza kuwa umetumwa na mahasimu wake kisiasa na kibiashara.

“Kuna baadhi ya wakubwa pale Wizara ya Nishati hawapendi ukweli… mwaka jana nilihoji kuhusu malipo ya fidia kwa wananchi wa Buhemba kutokana na athari walizopata kufuatia uwekezaji feki wa Kampuni ya Meremeta.

“Nikasema kwanini fedha zao zilielekezwa kufidia Kiwira, lakini wananchi wangu wanyimwe, hapo likawa kosa, nikaibua vidonda vya wakubwa na chuki zikaanza. Mfano mtu anasema nimefilisi BoT au Tanesco, kwanza namshangaa, je mimi nilienda BoT au Tanesco kuiba?”  alihoji.

Alisema kampuni yake ya uwakili ni ya kimataifa, na amekuwa akifanya kazi na taasisi hizo kwa maadili makubwa, tena akishirikiana na mawakili wengine toka nchi za India na Marekani.

“Na kesi zote tumekuwa tukishinda kwa kulisadia taifa, leo ukifika wakati wa kutakiwa kulipwa gharama zetu ndio mambo yanazushwa… kama nimeiba au kufilisi waende polisi au kwa vyombo husika si kwa kunitukana.

“Sijawahi kumlazimisha mtu au kampuni kufanya kazi ya kutetea taasisi yake, bali wanakuja wenyewe wakijua uwezo wangu katika taaluma hii, iweje waanze kuhoji gharama baada ya kumaliza kazi?” alisema.

Alisema kuwa hashangai kuona haya kwa sababu ndani ya wizara hiyo kuna watendaji aliowaita wababe na wasiopenda kuona Watanzania wengine wakishiriki katika shughuli za uchumi.

Hata hivyo, Mengi hakupatikana kujibu tuhuma hizo na hivyo juhudi za kumtafuta zinaendelea.

Dk. Slaa alivaa Bunge
Akizungumza na gazeti hili kuhusu waraka huo, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema tatizo hilo limetokana na Bunge kugeuka kichaka cha kuficha uozo kwa kukataa pendekezo la kuundwa Kamati Teule kuchunguza tuhuma hizo.

“Tusingefika hapa kwa Bunge kugeuka kichaka cha kuficha uozo kama sio Spika wa Bunge, Anne Makinda kulinda mafisadi na kukataa kuunda kamati teule. Tatizo hili lilianzia kwa Spika aliyepita, Samuel Sitta wakati wa sakata la EPA.

“Sasa ili kujisafisha katika tuhuma hizi, serikali inapaswa kutoa taarifa bungeni kueleza ni lini uchunguzi huo utakamilika na taarifa hiyo itawasiliwashwa lini bungeni,” alisema.

Dk. Slaa aliwataka wananchi wasigeuzwe kuwa mazezeta katika suala hilo na badala yake wanapaswa kupiga kelele ili serikali iseme ukweli na kuchukua hatua.

Alisema kuwa itakuwa ni jambo la ajabu Serikali ya Uingereza ambayo imesaini mpango wa kuisaidia Tanzania euro milioni 71 (sawa na sh bilioni 177) katika miradi ya umeme, inafuatilia kwa umakini tuhuma hizo wakati Watanzania wako kimya.

“Kama serikali inataka kujisafisha katika ufisadi huu, basi Rais Jakaya Kikwete hana budi kufanya kama alivyofanya kwenye sakata la EPA kwa kutafuta mkaguzi kutoka nje ili ukweli ujulikane kwa sababu hapa ndani kwa sasa hakuna anayemwamini mwingine.

“Katika hili wala tusidanganyane, serikali ni mtuhumiwa. Hivyo kusema kwamba inatumia taasisi zake za CAG na Takukuru kujichunguza hapo tayari tumepigwa chenga la macho,” alisema.

Pia alimtaka Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kuacha propaganda kwenye majukwaa ya kisiasa za kudai kwamba UKAWA hawana huruma na Watanzania, badala yake amemtaka asaidie kuishauri Serikali ya Kikwete isipoteze fedha za Uingereza.

“Hizi fedha za Uingereza euro milioni 71 wanazotaka kuzizuia endapo tuhuma hizi za ufisadi zisipowekwa wazi, ni fedha nyingi sana, zingesaidia kwenye masuala mengi ya kijamii kama nishati, elimu, afya na maji. Sasa badala ya Kinana kuona umuhimu huo, anaendeleza propaganda dhidi ya UKAWA,” alisema.

Chanzo: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment