Naibu Katibu Mkuu Chadema - Mhe. Zitto Kabwe |
TUME ya Uchaguzi nchini (NEC)
inadaiwa kuingia katika mchakato wa mwisho wa kuzipa zabuni ya kuandaa vifaa
vya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 kampuni za M/S Jazzmatrix Cooperation na M/S Invu
IT Solution zinazodaiwa kuwa na rekodi mbaya ya utendaji.
Tanzania Daima limedokezwa kuwa
mkakati huo unahusishwa na njama za kutaka kukibeba Chama Cha Mapinduzi
(CCM) katika uchaguzi huo kwa kuchakachua matokeo ya kukibakiza madarakani.
Kampuni hizo ambazo
katika zabuni ya Tume ya Uchaguzi zimetajwa kushirikiana na Kampuni ya
Kitanzania ya M/S SCI Tanzania Limited, mbali ya kutojulikana zinapotoka, pia
ndizo zimekuwa na gharama kubwa kuliko kampuni nyingine zilizoomba kazi hiyo.
Kiwango ambacho kampuni hizo
zilitaja na kukubaliwa na NEC kwa ajili ya kuandaa vifaa vya kielektroniki vya
kusajili wapiga kura (Biometric Voters Registration) ni zaidi ya euro milioni
60, sawa na sh bilioni 126.3, wakati kampuni zinazofuata zikihitaji kuanzia
euro milioni 40.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, ni mmoja wa viongozi
waliofichua mkakati huo, akidai unafanywa na serikali ya CCM ili kuhakikisha
wanajiandaa kudhibiti kila eneo ili waweze kubaki madarakani.
Alisema lengo ni kuhakikisha
mchakato wa vitambulisho vya kupigia kura vya kielektroniki vina kuwa na faida
kwa CCM na kukiingizia fedha chama hicho za kutumia kwenye uchaguzi huo kupitia
mfumo huo dhaifu wa vitambulisho hivyo.
Zitto alisema kutokana na hali
hiyo, amemwandikia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) barua ya kutaka ukaguzi
wa zabuni hiyo ufanyike kwa kushirikisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru) na vyombo vingine vya usalama kwa ajili ya kujiridhisha.
“Wenzetu CCM wanafanya mikakati
ya kujiandaa na Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kuhakikisha wanapata fedha za kutosha na hata mazingira
mabaya ya vifaa vitakavyotumika katika upigaji kura na sasa wameshaingia hata
katika Tume ya Uchaguzi kwa ajili ya kutengeneza mazingira,” alisema Zitto.
Aliongeza kuwa kiasi
kilichotolewa ni kodi ya Watanzania na kwamba ni vema taifa likajiridhisha kuwa
matatizo yaliyotokea Kenya na Ghana hayatajirudia Tanzania, hasa wakati wa
upigaji kura.
Gazeti hili limeona barua
hiyo ya Zitto kwenda kwa CAG, ya Novemba 7, 2013, yenye kichwa cha habari;
‘Zabuni ya Biometric Voters Registration (BRV KITS) No.
IE/018/2012-13/HQ/G/19 yenye thamani ya sh bilioni 126.3.’
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa
Kigoma Kaskazini anasema kuwa
NEC imekuwa katika mchakato wa zabuni tajwa hapo juu.
“Zabuni hiyo sasa imeanza
kuleta malalamiko miongoni mwa wananchi kutokana na kinachosemekana kuwa
kampuni iliyopewa zabuni hiyo haina uwezo kiteknolojia, pia bei zao ni kubwa.
“Katika mafunzo ya hivi
karibuni ya SADCOPAC jijini Nairobi tuliazimia kuwa ni vema kwenye zabuni nyeti
kama za namna hii, SAIs wawe na uwezo wa kufanya ukaguzi kabla ya zabuni
kutolewa na kuanza kutekelezwa,” alisema.
Kwa mujibu wa nyaraka za
NEC ambazo Tanzania Daima linazo, kampuni zilizopewa tenda ya pamoja yenye
kugharimu kiasi cha dola 78, 987,636.00, sawa na sh 126,291,375,455 ni M/S
Jazzmatrix Cooperation na M/S Invu IT Solution ambazo hazijulikani nchi
zinapotoka zikiwa zinashirikiana na M/S SCI Tanzania Limited.
Katika nyaraka hizo
kampuni zilizokosa tenda na ambazo zimelalamika kwa Mkurugenzi wa NEC
namna mchakato wa kutoa zabuni hiyo ulivyoendeshwa zimeainishwa kuwa ni M/S
Zetes SA ya nchini Ubalgiji, M/S IRIS Corporation Technology ya Malaysia,
M/S Lithotech Exports ya Afrika Kusini, M/S Safran Morpho ya Ufaransa na
M/S Avante International Technology, Inc ya Marerkani.
Kampuni hizo zinahoji
njia na sababu zilizowafanya wakose tenda hiyo licha ya kuwa na uzoefu, vifaa
bora pamoja na kuwa na kiwango kidogo cha gharama tofauti na kampuni iliyopewa
kazi.
Katika moja ya malalamiko
yao, Kampuni ya M/S Morpho, inalalamika kutofahamishwa namna walivyokosa vigezo
vya kupata kazi hiyo licha ya kuwa na sifa za kimataifa za kufanya kazi huku
ikiwa imetoa bei nafuu kuliko kampuni iliyopata kazi.
“Tulikuwa miongoni mwa
washindani muhimu kwa kuwa kiwango chetu kilikuwa ni sh bilioni 97.8 ambazo ni
sawa na euro 44,939,912 + sh 3,843,736,140.
“Ujuzi, vigezo na uzoefu wetu
havilingani, duniani kote tumefanya kazi katika maeneo mengine kwa ufanisi na
tunashindwa kuelewa kivipi walishinda hao ambao wamepata kazi kwa kiwango cha
zaidi ya sh bilioni 27.8 ikilinganishwa na yetu,” ilisomeka sehemu ya barua.
Alipotafutwa Mkurugenzi
wa NEC, Julius Mallaba, alisema hawezi kuliongelea suala hilo katika simu na
kuomba mwandishi awasiliane na Kaimu Mkurugenzi wa NEC, Dk. Sist Cariah, ambaye
alisema mchakato wa kupata kampuni ulifuatwa kisheria.
Dk. Cariah alisema si kweli
kwamba kampuni iliyopewa kazi haina uwezo bali malalamiko yanatoka kwa watu
walioshindwa kupata kazi hiyo.
Alipoulizwa juu ya uzoefu wa
kampuni hiyo na wapi ilifanya kazi, Dk. Cariah alisema kwa maelezo waliyonayo
ni kwamba kampuni hiyo ina uzoefu wa miaka 35 wa kufanya kazi, huku akishindwa
kuainisha sehemu ilizowahi kufanya kazi.
Kuhusu wapi zimetoka kampuni
hizo, Dk. Cariah alisema suala la kutoainishwa kimaandishi ni makosa ya kawaida,
huku akitaja kuwa zinatoka katika nchi ya India na Australia.
Kuhusu gharama, Dk. Cariah
alisema licha ya makampuni mengine kutaja gharama za chini, zingeweza kuwa na
gharama kubwa zaidi wakati wa kukamilisha kazi hiyo kutokana na kuwa na gharama
zilizojificha.
No comments:
Post a Comment