To Chat with me click here

Monday, September 30, 2013

SHAMBULIO LA WESTGATE LADHIHIRISHA MAPUNGUFU MAKUBWA KATIKA USALAMA


Askari wa Kenya wakielekea katika maduka ya WestGate


Wakati vitisho vikirudiwa na dhihaka kutoka kwa al-Shabaab vilivyotokea siku chache zilizopita, Watu wa Kenya bado wanatafuta majibu ya ni kwa namna gani uzingiraji uliosababisha umwagaji wa damu ulivyotokea katika kituo cha biashara ya maduka ya matajiri huko Westgate Nairobi.

Kwa sasa, taarifa zilizo nyingi za uzingiraji zimeeleweka: Jumamosi iliyopita kundi la watu wenye silaha la al-Shabaab walivamia kituo kikubwa cha maduka, waliwaua kikatili wanunuzi na kurusha maguruneti kwenye mkusanyiko wa raia wasio na hatia. Hali hiyo iliyodumu kwa siku nne, watu hao wenye silaha waliawaua watu wapatao 67 na kushikilia idadi isiyojulikana ya mateka hadi vikosi vya usalama vya Kenya vilipopata udhibiti wa hali hiyo Jumanne. 

Lakini baada ya tukio hilo, maswali mengi yalibakia bila majibu: Nini kilichotokea kwa mateka waliobakia? Washambuliaji waliwezaje kuingia katika kituo cha maduka na kushikilia kwa muda mrefu? Nani kiongozi katika shambulio hilo na wapi aliko sasa?

Je, vikosi vya usalama na vya upelelezi vilipata tahadhari kabla kuhusu shambulio, na vingeweza kuliepusha? 

"Shambulio la kigaidi halikutokea pasipo mpango," alisema mchambuzi wa masuala ya usalama Raymond Kipkorir Cheruiyot, kanali mstaafu wa vikosi vya jeshi la Kenya na mmiliki shirika wa kampuni ya Multi Security Consultants Limited huko Nairobi.

"Magaidi walitekeleza shambulio wakati wakala wa usalama wakiwa kwenye kujiridhisha," aliiambia Sabahi. "Maduka ya biashara ya matajiri ya Westgate yalikuwa kwenye jengo lenye hadhi kubwa,ambalo lililpaswa kuwa chini ya uchunguzi imara wa usalama kwa saa 24 na kulindwa na polisi wenye silaha. Kwa njia hiyo, mpango wa shambulio hilo ungeweza kugundulika na kuepushwa."


Cheruiyot alikosoa mwitikio usioungana wa serikali ya Kenya wa kile kinachoelezwa kama shambulio lenye utata ambalo "timu yenye ufa ya magaidi" walipanga kwa uangalifu na kulitekeleza.

Mamlaka zinapaswa kuweka lengo lenye thamani kubwa kama hiyo chini ya uchunguzi wa kudumu, kupitia tena mipangilio na taratibu za usalama zilizopo, na kufuatilia wenyeji wanaowaonea huruma pamoja na au kuunga mikono ugaidi, alisema.

"Ndiyo, muda wamwitikio wa timu ya usalama ulikuwa mzuri, lakini utendaji wao ungeweza kuwa mzuri zaidi, kama walivyotenda kwenye tahadhari ya upelelezi ya nje kwamba maduka ya biashara ya matajiri ya Westgate yalikuwa rahisi kulengwa na magaidi," Cheruiyot alisema.

Tahadhari ya hapo kabla ya ugaidi

Mwezi Agosti, maofisa usalama walitoa tahadhari ya ugaidi kwa Kenya, wakisema walipokea ripoti ya upelelezi kwamba al-Shabaab wapatao watano waliingia Mombasa kutokea Somalia na wangeweza kupanga shambulio kuingiliana na kumbukumbu ya kwanza ya ulamaa wa dini mwenye siasa kali kuuawa kwa Aboud Rogo Mohammed.

"Tahadhari ya usalama huko Mombasa au Kisumu inapaswa kuhusika na nchi nzima," alisema Meja mstaafu wa jeshi Bishar Hajji Abdullahi. "Ni ushahidi kuwa kuna mtu aliyefanya uzembe."

"Baada ya tukio hili, wale wanaojijua kuwa walihusika wanapaswa kuachia ngazi, au rais [anapaswa] kuwafukuza kazi," Abdullahi aliiambia Sabahi.

Vikosi vya Usalama vya Kenya na vikosi vinavyofungamana navyo vimefanya kazi nzuri ya kuwaondoa al-Shabaab ndani ya Somalia, lakini huduma za usalama wa Kenya zilipaswa kuzindua msako wa wanamgambo washukiwa katika ardhi ya nyumbani mara walipopata taarifa za kiintelijensia, alisema.

David Ochami, mwandishi wa habari anayeishi Mombasa anayeripoti habari za vikundi vya wanamgambo vya Mashariki ya Kati na Pembe ya Afrika, alisema kulikuwa na dalili za uwezekano wa shambulizi katika wiki zilizotangulia uzingiraji wa Westgate.

Al-Shabaab na wanaowaunga mkono wamekuwa wakisikika sana katika vyombo vya habari vya kijamii katika wiki chache kabla ya shambulizi, kwa mfano, ujumbe wao mbalimbali ungeweza kutoa ishara za kuzuia shambulizi, alisema. 

"Baadhi ya habari zilizotumwa zinaweza kugeuka kuwa mzaha wa kupandikiza hofu au msimamo, lakini zinapaswa kutambuliwa na kuzingatiwa kwa makini," Ochami aliiambia Sabahi.

Hata wakati wa uzingiraji katika maduka, al-Shabaab mara nyingi waliweka ujumbe kuhusu jambo hilo kwenye Twitter, Ochami alisema, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia jinsi magaidi wanavyotumia mitandao ya kijamii wanapopanga na kutekeleza mashambulizi hayo. 

Licha ya kuwa na angalau na mitandao ya Twitter iliyofungwa mwaka huu, ikiwemo mitatu katika tukio la shambulizi la Westgate, al-Shabaab bado inatumia mitandao ya kijamii kutishia na kuwadhihaki maadui zake. 

Katika mfululizo wa kuandika katika Twitter Alhamisi, al-Shabaab waliikosoa serikali ya Kenya kwa taarifa zinazopingana wazi inazozitoa kufuatia shambulizi hilo. 

"Serikali ya Kenya bado iko kwenye machafuko na hadi baada ya miezi kadhaa ndipo itakapotambua hasa kitu gani kilitokea Westgate," al-Shabaab ilisema. "Mkanganyiko wa habari za matukio yao ni dalili halisi kwamba serikali ya Kenya inaanza kupata machungu ya ukosefu mkubwa wa mawazo." 

Wanamgambo waliendelea kujigamba kwa "kitendo chao cha kupumbaza" katika Westgate, wakiwaacha Wakenya wakishangazwa kabisa kwa zaidi ya saa 100".

Al-Shabaab walirudia vitisho vyao kwa Wakenya wakisema, "…msikate tamaa majamaa, hiyo ilikuwa ni sehemu ya kwanza ya Sheria 1".

Dokezo la tahadhari la shambulizi la Westgate lilikuwa linakuja

Wakati huo, mbunge wa Kenya Mike Sonko alitokea katika vichwa vya habari wiki hii kwa kudai kwamba kabla ya shambulizi hilo alipokea taarifa kwamba magaidi walikuwa wanapanga kuvamia eneo la maduka Westgate na maeneo mengine ya Nairobi.

Alisema alipeleka taarifa hizo kwa viongozi, lakini hawakuichukulia kwa uzito.
Kwa mujibu wa Sonko, anayewakilisha jimbo la Westlands ambako ndiko iliko Westgate, wanawake wawili walimfuata kiasi cha miezi mitatu iliyopita wakiwa na taarifa kwamba wanamgambo wa al-Shabaab wamepanga nyumba huko kitongoji cha Parklands na Nairobi na walikuwa wanapanga mashambulizi kama hayo.

"Walinieleza mashambulizi yanalenga Westgate, Village Market, Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kenyatta na bunge," aliiambia Sabahi. "Niliwasisitiza kwenda kutoa taarifa polisi na kwa maofisa upelelezi ili uchunguzi zaidi uweze kufanyika." 

Idara ya Upelelezi ya Usalama wa Taifa na vyombo vingine vya usalama vilishindwa kuchukua hatua mara moja, Sonko alisema. Alieleza habari hizi kwenye Seneti tarehe 24 Septemba, siku ambayo mapambano huko Westgate .
Mbunge mwenzake Asman Kamama, ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Utawala na Usalama wa Taifa ya Bunge la Taifa, alisema shambulizi la eneo la maduka lilionyesha mianyo katika ukusanyaji wa upelelezi. 

"Jinsi mashambulizi yalivyofanyika, yaliratibiwa vizuri, ikimaanisha ni kitu kilichopangwa vizuri na kutekelezwa," Kamama, mbunge wa Chama cha United Republican anayewakilisha Kaunti ya Baringo, aliiambia Sabahi.

"Na kwa kikosi chetu cha upelelezi kutokuwa na fununu kuhusu mashambulizi yanayokaribia, inamaanisha [kulikuwa] na kushindwa kwa kiasi kikubwa kwa usalama ambao lazima tuchunguze na [ambapo ni lazima] kuwawajibisha watu binafsi," alisema.

Maafisa wajibu

Shambulio la Westgate sio tu lililifadhaisha taifa bali lilionekana kuwagusa watetezi wa walinzi wa nchi, maafisa waliiambia Sabahi.
"Kwa dhati kabisa, hii ni mara ya kwanza ambapo Kenya imeshuhudia shambulio la kinyama la kigaidi kama hili katika jengo la maduka kwa kutumia bunduki," alisema Mkurugenzi wa Mageuzi ya Polisi Jonathan Kosgei. "Tulikuwa tunajua kuhusu mabomu, [lakini] mtindo huu mpya ulikuwa vigumu kuweza kuubashiri. Hata hivyo, vikosi vya usalama vilifanya kazi yao vizuri ili kuidhibiti hali hii katika mazingira magumu." 

"Shambulio hili bila ya shaka litaharakisha mjadala wa kitaifa [kuhusu] kwa upande wa walinzi wa usalama au la," aliiambia Sabahi. "Wakiwa na vifimbo vya mbao tu na filimbi, walinzi walikuwa katika mazingira magumu na kushindwa kabisa kuzuia shambulio la silaha." 

Jambo jengine la kuzingatia ni jinsi gani Westgate ilivyofichua mabadiliko makubwa sana ya mbinu za kijeshi za al-Shabaab hadi kufanya operesheni kama za kikomandoo, kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Western James ole Seriani.

"Wanataka kusababisha hasara kubwa kabisa ambayo vifaa vya milipuko vya kando ya barabara vilikuwa haviwezi kusababisha," aliiambia Sabahi. "Ni mbinu ile ile waliyoitumia huko Garissa mwaka jana wakati walipovamia na kufyatua risasi katika makanisa mawili na hoteli na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 20."

Mauaji ya Westgate ni wito wa tahadhari, alisema Seriani, na umma unapaswa kujihadhari ili magaidi waweze kushughulikiwa kabla hawajakatiza Kenya.
Serikali ya Kenya ililaumiwa, pia, kwa kutoa taarifa zinazokinzana kwa vyombo vya habari kwani gaidi wa Westgate hajabainishwa.

Lakini katibu Mkuu wa Usalama wa Ndani Mutea Iringo aliitetea serikali, akisema ilikuwa mbinu iliyokusudiwa kuwapotezea mwelekeo magaidi.
"Ukimya nao ni silaha," aliiambia Sabahi. "Hupendi kujihusisha katika mtindo wa kutangaza hadharani pamoja na magaidi."

Wakati lilikuwa ni tukio la kusikitisha, Iringo alisema alikuwana matumaini kuwa shambulio la Westgate litawahamasisha viongozi wa dunia kuchukua hatua dhidi ya al-Shabaab.

"Al-Shabaab siyo tatizo kwa Somalia tu lakini ni sehemu ya mtandao wa ugaidi wa dunia ambao unahitaji serikali za dunia kuusambaratisha," alisema.
Maofisa wa ngazi za juu wa usalama wanatarajiwa kujitokeza mbele ya bunge wiki lijalo kama sehemu ya uchunguzi katika shambulio la ugaidi.

"Muda wa uwajibikaji umefika," mwenyekiti wa kamati ya ulinzi Ndung'u Gethenji alisema, kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation la Kenya.
"Tutafanya uchunguzi wa kina, shirikishi na usiokuwa na msamaha kuhusiana na tukio na udhaifu uliosababisha shambulio," alisema bungeni muda mfupi baada ya kamati yake kufanya mkutano usio wa umma Alhamisi.

Gethenji alisema kamati ya pamoja, iliyohusisha wajumbe wa kamati za ulinzi na usalama wa taifa, watatoa wito kwa mkuu wa intelijensia, Katibu wa baraza la Mambo ya Ndani, Inspekta Generali wa Polisi na viongozi wengine wa juu wa usalama kutoa taarifa wa kina wa shambulio hilo.

No comments:

Post a Comment