Jana
Zitto Zuberi Kabwe (Mb) aliandika kuhusu Deni la Taifa kukua kwa kasi na
kufikia Tshs 27 trilioni mpaka Desemba 2013 kutoka Tshs 10 trilioni mwaka 2005.
Baadhi ya Watalaamu wanajenga hoja kuwa kukopa sio shida, bali kukopa kwa ajili
ya nini. Nikakumbuka mzigo wa madeni ambao Taifa lilibeba miaka ya sabini na
themanini kiasi cha Tanzania kukoswa koswa kuwa nchi ya Kwanza duniani
kushindwa kuhudumia madeni yake. ‘heshima’ hiyo ilikwenda kwa nchi ya Nicaragua
mwaka 1982. Mikopo ya nini?
Mwishoni
mwa miaka ya sabini Tanzania ilikopa dola za kimarekani milioni sitini (USD
60m) kwa ajili ya mradi wa Kiwanda cha viatu Morogoro. Lengo la kiwanda kiwanda
kile ilikuwa ni kuuza viatu nchini Italia. Mwaka mmoja baada ya kiwanda
kuzinduliwa kilikuwa na uwezo wa kuzalisha kwa ufanisi wa asilimia 4 tu ya
uwezo wake na hakikuweza kuuza hata jozi moja ya kiatu nje ya nchi. Miaka ya
tisini kiwanda kile kiliuzwa katika mpango wa ubinafsishaji na hivi sasa
kimegeuzwa kuwa ghala. Hata hivyo Deni hili lilipwa na kila Mtanzania kupitia
kodi.
Leo
Jumanne tarehe 28 Januari, 2014 Kamati ya Bunge ninayoongoza ya Hesabu za
Serikali (PAC) inapokea taarifa ya ukaguzi maalumu uliofanywa kuhusu Mfumo na
Mchakato wa kusambaza pembejeo za ruzuku kwa wakulima. Ukaguzi huu umefanywa na
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali (CAG). Nimeipitia Taarifa hii
na kukumbuka habari ya ‘Morogoro Shoe Factory’.
Bajeti
ya pembejeo za ruzuku ya mwaka 2011/12 ilikuwa tshs 122.4 bilioni, kati ya hizo
tshs 88.9 bilioni ni mkopo kutoka Benki ya Dunia. Taarifa ya CAG inaonyesha
uvundo wa ufisadi katika mfumo mzima wa pembejeo za ruzuku. Katika kijiji cha
Lunyala wilayani Nkasi mkoa wa Rukwa asilimia 70 ya wananchi waliorodheshwa
kupata mbolea walikuwa bandia, hata hao waliopata mbolea walidai mbolea ilikuwa
haina ubora stahili na matokeo yake uzalishaji wa mazao ulikuwa mdogo. Hata
hivyo wasambaji wa mbolea walilipwa fedha zao zote. Afisa mmoja mwandamizi wa
Benki ya Dunia alipata nukuliwa kusema kuwa asilimia 60 ya Bajeti ya pembejeo
za ruzuku iliporwa na wajanja wachache.
Deni
hili nalo litalipwa na Watanzania wote japo waliofadika ni wezi wachache.
Kinachosikitisha ni kwamba masuala haya yanayohusu wananchi hayapati msukumo
kwenye mijadala ya kitaifa. Tusipobadilika tutajikuta tuna madeni mpaka kwenye
kope za macho yetu.
“…mikopo haisaidii, hata
tukiitumia kujenga shule au hospitali au viwanda lazima ilipwe. Mlipaji ni
mkulima wa vijijini…” Azimio la Arusha, 1967.
No comments:
Post a Comment