Kila
mwaka, katika mikutano ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge,
ambao ni wawakilishi wa wananchi, huiuliza Serikali maswali mbalimbali kuhusu
mipango iliyopo kwenye sekta mbalimbali, ikiwemo elimu.
Mawaziri
husika au wawakilishi wao hutoa majibu ambayo mara nyingi huambatana na ahadi.
Je, baada ya hapo, nani ana jukumu la kufuatilia utekelezaji wa hizi ahadi? Kwa
mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano (1977), wananchi ndio msingi wa mamlaka
yote na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi.
Pia, lengo kuu la Serikali ni ustawi wa wananchi na itawajibika kwao.
Hii
ina maana mwananchi yuko ndani ya wajibu na mamlaka yake akihoji na kufuatilia
ahadi za serikali, kwani zinatolewa na viongozi wanaopaswa kuwajibika kwake.
Ndiyo maana, tangu January 2014, nimeamua kuwaelimisha na kuwashirikisha watanzania
ili waweze kutimiza wajibu wao wa kufuatilia ahadi za serikali na kuhakikisha
vipaumbele vyao vimefikiwa.
ELIMU
KWA WASICHANA, UFUNDI STADI, VIFAA VYA SHULE N.K
Baadhi ya wanafunzi wa kike wakiwa darasani wakifuatilia kipindi. |
Kwa mujibu wa taarifa za Bunge, ahadi zifuatazo zilizotolewa Bungeni
na Ummy A. Mwalimu, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto (4
Februari 2013), Hawa Ghasia, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (10 Aprili 2013) na Aggrey Mwanri, Naibu Waziri,
Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (10, 19 na 23
Aprili 2013):
• Serikali itaanza rasmi kujenga shule ya
wasichana Borega (Halmashauri ya Wilaya ya Tarime) mwezi June, 2013. Ujenzi huu
utakamilika ifikapo Novemba, 2014. Halmashauri kupitia mapato ya ndani
imechangia shilingi milioni 28 na eneo la ujenzi limeshapimwa. Kwa sasa
utaratibu wa kutangaza zabuni unaendelea.
• Serikali imepanga kuviboresha vyuo vya maendeleo
ya wananchi (FDCs) kwa
kuvikarabati, kuvipatia watumishi na vyombo vya usafiri.
• Serikali itatumia fedha za malipo ya fidia ya rada
kwa ununuzi wa vitabu na madawati katika shule za msingi Tanzania Bara. Fedha
itakayotumika kwa ajili ya ununuzi wa vitabu ni karibia shilingi bilioni 59 na
fedha kwa ajili ya ununuzi wa madawati ni karibia shilingi bilioni 20. Mchakato
wa ununuzi wa vitabu umekamilika ambapo Serikali imeingia mikataba yenye thamani
ya shilingi bilioni 57 na wachapishaji wa vitabu. Kulingana na mikataba, kazi
hii inategemewa kukamilika ndani ya miezi sita tangu tarehe ya kuweka saini
mikataba tarehe 18 Machi, 2013. Kwa upande wa ununuzi wa madawati, mchakato
umeanza ambapo katika Kikao cha Bunge la Bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013
iliazimiwa kuwa madawati yanunuliwe na kusambazwa katika halmashauri zote kwa
usawa.
• Katika juhudi za kutatua tatizo la madawati nchini, Serikali
imekuwa ikipeleka fedha katika halmashauri kwa ajili ya ununuzi na utengenezaji
wa madawati. Mwaka 2010/2011 shilingi bilioni tatu zilipelekwa katika
halmashauri zote kwa ajili ya madawati ambapo Mkoa wa Mara ulipata shilingi
milioni 197 na mwaka 2012/2013 shilingi bilioni moja zilipelekwa katika halmashauri
zote kwa ajili ya madawati na Mkoa wa Mara ukapata shilingi milioni 68.
• Kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi Serikali imekuwa
ikitoa fedha za uendeshaji wa shule (ruzuku)
kwa kiwango cha shilingi 10,000 kwa kila
mwanafunzi. Hadi kufikia mwezi Machi, 2013 Serikali imeshatoa jumla ya shilingi
bilioni 60 za ruzuku kwa shule za msingi nchini kote. Kiasi hiki ni sawa na shilingi
7,565 kwa mwanafunzi ambayo ni sawa na asilimia 75.
Je, ahadi hizi zimetekelezeka? wananchi husika wa maeneo ambako ahadi
hizi zililengwa kwao wana wajibu wa kufuatilia na kuhakikishwa zimetekelezwa.
Tafakari na chukua hatua kwa maendeleo ya Taifa lako sasa.
Unaweza kupata habari hizi kila wakati kwa ku-click “LIKE” au katika “facebook
page” yangu: Maxmillian Kattikiro FB-Page
No comments:
Post a Comment