To Chat with me click here

Friday, January 31, 2014

KIONGOZI WA KUNDI LA WATOTO “MBWA MWITU ATIWA MIKONONI MWA POLISI



Habari zilizotufikia katika mtandao wetu ni kuwa, aliyekuwa kiongozi na mwanzilishi wa kundi la vijana ambao wamekuwa wakijiita “MBWA MWITU” ambaye anafahamika kwa jina la bandia kama KASELA amekamatwa jana majira ya saa 7 mchana, maeneo ya Yombo Buza, ambako alikutwa akicheza POOL TABLE. 

Mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa, Kasela alikutwa akicheza pool table na baadhi ya raia wema, ndipo walipoamua kuwataarifu polisi juu ya uwepo wake eneo hilo. Polisi hawakuchukua muda wakawa wamefika eneo la tukio kabla mshukiwa hajastukia mpango huo. Baada ya kijana huyo kuwatambua askari polisi, alitimua mbio ambazo hazikufua dafu kwa askari hao ambao walikuwa na bunduki zao mkononi pamoja na baadhi ya raia wema waliojitolea kusaidia polisi. Polisi walifanikia kumnasa Kasela baada ya kujisalimisha kwao, alipoamrishwa kusimama.  

Yasemekana kijana huyu alizaliwa tarehe 28 December 1995 na anaishi na wazazi wake wote wawili (Baba na Mama) ambao nao walikwisha onja joto ya jiwe ya motto wao, baada ya kuwachapa makonde kwa kuwa walimsema katika kumrekebisha tabia. 

Mbali na kuwa yeye ndiye muasisi wa kundi hilo la vijana wadogo wa mbwa mwitu, kijana huyo amekwisha shiriki katika matukio mbalimbali ya wizi na umwagaji damu katika maeneo ya Yombo Vituka Lumo, Kiwalani na Buza. Matukio hayo ndiyo yaliyopelekea wananchi wa maeneo tajwa kujawa na hasira kiasi cha kuwasaka mbwa mwitu hao na kupelekea vifo vya wanakundi hilo wawili waliotambulika kwa majina ya Mpolendi na Traveller, huku wengine wakikimbilia mikoa ya jirani kama vile Tanga na Pwani.  

Kwa sasa hali ni swali katika maeneo hayo, na wananchi wamepokea kwa furaha sana taarifa za kukamatwa kwa kiongozi huyo wa kundi la mbwa mwitu. 

Mwisho kabisa kwa niaba yangu binafsi pamoja na wadau wengine wote wa blog yetu, napenda sana kulipongeza jeshi la polisi, kwa kuweza kufanikisha kumkamata kijana huyo ambaye amekuwa tishio na gumzo kwa wakazi wa maeneo taja. Ni matumaini yangu kuwa sharia itachukua mkondo wake. 

Tuesday, January 28, 2014

DENI LA TAIFA: WAFAIDI WACHACHE, TWALIPA WOTE!




Jana Zitto Zuberi Kabwe (Mb) aliandika kuhusu Deni la Taifa kukua kwa kasi na kufikia Tshs 27 trilioni mpaka Desemba 2013 kutoka Tshs 10 trilioni mwaka 2005. Baadhi ya Watalaamu wanajenga hoja kuwa kukopa sio shida, bali kukopa kwa ajili ya nini. Nikakumbuka mzigo wa madeni ambao Taifa lilibeba miaka ya sabini na themanini kiasi cha Tanzania kukoswa koswa kuwa nchi ya Kwanza duniani kushindwa kuhudumia madeni yake. ‘heshima’ hiyo ilikwenda kwa nchi ya Nicaragua mwaka 1982. Mikopo ya nini?

Mwishoni mwa miaka ya sabini Tanzania ilikopa dola za kimarekani milioni sitini (USD 60m) kwa ajili ya mradi wa Kiwanda cha viatu Morogoro. Lengo la kiwanda kiwanda kile ilikuwa ni kuuza viatu nchini Italia. Mwaka mmoja baada ya kiwanda kuzinduliwa kilikuwa na uwezo wa kuzalisha kwa ufanisi wa asilimia 4 tu ya uwezo wake na hakikuweza kuuza hata jozi moja ya kiatu nje ya nchi. Miaka ya tisini kiwanda kile kiliuzwa katika mpango wa ubinafsishaji na hivi sasa kimegeuzwa kuwa ghala. Hata hivyo Deni hili lilipwa na kila Mtanzania kupitia kodi.

Leo Jumanne tarehe 28 Januari, 2014 Kamati ya Bunge ninayoongoza ya Hesabu za Serikali (PAC) inapokea taarifa ya ukaguzi maalumu uliofanywa kuhusu Mfumo na Mchakato wa kusambaza pembejeo za ruzuku kwa wakulima. Ukaguzi huu umefanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali (CAG). Nimeipitia Taarifa hii na kukumbuka habari ya ‘Morogoro Shoe Factory’.

Bajeti ya pembejeo za ruzuku ya mwaka 2011/12 ilikuwa tshs 122.4 bilioni, kati ya hizo tshs 88.9 bilioni ni mkopo kutoka Benki ya Dunia. Taarifa ya CAG inaonyesha uvundo wa ufisadi katika mfumo mzima wa pembejeo za ruzuku. Katika kijiji cha Lunyala wilayani Nkasi mkoa wa Rukwa asilimia 70 ya wananchi waliorodheshwa kupata mbolea walikuwa bandia, hata hao waliopata mbolea walidai mbolea ilikuwa haina ubora stahili na matokeo yake uzalishaji wa mazao ulikuwa mdogo. Hata hivyo wasambaji wa mbolea walilipwa fedha zao zote. Afisa mmoja mwandamizi wa Benki ya Dunia alipata nukuliwa kusema kuwa asilimia 60 ya Bajeti ya pembejeo za ruzuku iliporwa na wajanja wachache.

Deni hili nalo litalipwa na Watanzania wote japo waliofadika ni wezi wachache. Kinachosikitisha ni kwamba masuala haya yanayohusu wananchi hayapati msukumo kwenye mijadala ya kitaifa. Tusipobadilika tutajikuta tuna madeni mpaka kwenye kope za macho yetu.

…mikopo haisaidii, hata tukiitumia kujenga shule au hospitali au viwanda lazima ilipwe. Mlipaji ni mkulima wa vijijini…” Azimio la Arusha, 1967.

Saturday, January 25, 2014

HABARI MBAYA KWA WALAJI WA NYAMA YA NGURUWE KITIMOTO!



Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimehadharisha walaji wa nyama ya nguruwe nchini, kuwa wanakabiliwa na hatari ya kupata kifafa.

Utafiti wa kisayansi uliofanywa na SUA, umebaini kuwa baadhi ya nguruwe wana minyoo aina ya tegu ambao nyama yao ikiliwa bila kuiva vizuri, mlaji atapata minyoo hiyo ambayo huingia kichwani na kusababisha kifafa.

Akizungumza na mwandishi hivi karibuni, Mhadhiri na Mtafiti wa Idara ya Sayansi ya Wanyama na Uzalishaji ya SUA, Profesa Faustine Lekule, alisema sampuli za utafiti huo kutoka Mbeya, zimebaini nguruwe wengi wakiwamo wanaosafirishwa katika miji mikubwa wameathirika na minyoo hiyo.

Kwa mujibu wa Profesa Lekule, wataalamu wa SUA wanaosimamia Mradi wa Utafiti wa Kuboresha Ufugaji wa nguruwe kwa mkoa wa Mbeya ili kuinua pato la kaya, unaofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Denmark (DANIDA), walibaini hatari hiyo baada ya kuchukua sampuli ya nyama ya nguruwe kwa ajili ya vipimo.

“Majibu ya sampuli ambazo wataalamu wamezichukua kutoka kwa nguruwe wa wafugaji kwenye baadhi ya vijiji, wamebainika kukumbwa na hatari hii. 

“Lazima jitihada za makusudi zichukuliwe katika kutafuta ufumbuzi wa pamoja wa tatizo hili kati ya watafiti na Serikali,” alisema Profesa Lekule.

Alisema maambukizi ya tegu au minyoo ya nguruwe yanatokana na tabia za baadhi ya wafugaji kutozingatia ufugaji bora kwa kuwaacha kujitafutia chakula na maji mitaani na kula kinyesi cha binadamu.

Kwa mujibu wa Profesa Lekule, baadhi ya wafugaji wamekuwa wakijisaidia vichakani na kuwaacha nguruwe kutafuta malisho katika vichaka na kula kinyesi chao, hali inayochangia ongezeko la maambukizi ya minyoo ya tegu hao.

Baada ya kula kinyesi minyoo humwingia mwilini na kumdhoofisha na baadaye binadamu anapokula nyama ambayo haijaiva vizuri, minyoo hiyo humwingia na kusababisha kifafa baada ya kuingia kichwani.

Alisema athari za kuenea kwa maambuziki hayo inaweza kutokea katika miji mikubwa ikiwamo Dar es Salaam kwa kuwa nguruwe wa Mbeya husafirishwa na kuuzwa maeneo hayo.

“Hatua hii inaweza kusababisha kusambaa kwa ugonjwa huu, hivyo ushirikiano kati ya wafugaji, wafanyabiashara, Serikali na wataalamu wa afya katika kufikia hatua ya kumaliza changamoto hii unahitajika,” alibainisha Profesa Lekule

Friday, January 24, 2014

ZIJUE AHADI ZA SERIKALI KWENYE SEKTA YA ELIMU 2012/2013



Kila mwaka, katika mikutano ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge, ambao ni wawakilishi wa wananchi, huiuliza Serikali maswali mbalimbali kuhusu mipango iliyopo kwenye sekta mbalimbali, ikiwemo elimu.

Mawaziri husika au wawakilishi wao hutoa majibu ambayo mara nyingi huambatana na ahadi. Je, baada ya hapo, nani ana jukumu la kufuatilia utekelezaji wa hizi ahadi? Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano (1977), wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi. Pia, lengo kuu la Serikali ni ustawi wa wananchi na itawajibika kwao. 

Hii ina maana mwananchi yuko ndani ya wajibu na mamlaka yake akihoji na kufuatilia ahadi za serikali, kwani zinatolewa na viongozi wanaopaswa kuwajibika kwake. Ndiyo maana, tangu January 2014, nimeamua kuwaelimisha na kuwashirikisha watanzania ili waweze kutimiza wajibu wao wa kufuatilia ahadi za serikali na kuhakikisha vipaumbele vyao vimefikiwa.

ELIMU KWA WASICHANA, UFUNDI STADI, VIFAA VYA SHULE N.K


Baadhi ya wanafunzi wa kike wakiwa darasani wakifuatilia kipindi.
Kwa mujibu wa taarifa za Bunge, ahadi zifuatazo zilizotolewa Bungeni na Ummy A. Mwalimu, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto (4 Februari 2013), Hawa Ghasia, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (10 Aprili 2013) na Aggrey Mwanri, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (10, 19 na 23 Aprili 2013):

Serikali itaanza rasmi kujenga shule ya wasichana Borega (Halmashauri ya Wilaya ya Tarime) mwezi June, 2013. Ujenzi huu utakamilika ifikapo Novemba, 2014. Halmashauri kupitia mapato ya ndani imechangia shilingi milioni 28 na eneo la ujenzi limeshapimwa. Kwa sasa utaratibu wa kutangaza zabuni unaendelea.

Serikali imepanga kuviboresha vyuo vya maendeleo ya wananchi (FDCs) kwa kuvikarabati, kuvipatia watumishi na vyombo vya usafiri.

Serikali itatumia fedha za malipo ya fidia ya rada kwa ununuzi wa vitabu na madawati katika shule za msingi Tanzania Bara. Fedha itakayotumika kwa ajili ya ununuzi wa vitabu ni karibia shilingi bilioni 59 na fedha kwa ajili ya ununuzi wa madawati ni karibia shilingi bilioni 20. Mchakato wa ununuzi wa vitabu umekamilika ambapo Serikali imeingia mikataba yenye thamani ya shilingi bilioni 57 na wachapishaji wa vitabu. Kulingana na mikataba, kazi hii inategemewa kukamilika ndani ya miezi sita tangu tarehe ya kuweka saini mikataba tarehe 18 Machi, 2013. Kwa upande wa ununuzi wa madawati, mchakato umeanza ambapo katika Kikao cha Bunge la Bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013 iliazimiwa kuwa madawati yanunuliwe na kusambazwa katika halmashauri zote kwa usawa.

• Katika juhudi za kutatua tatizo la madawati nchini, Serikali imekuwa ikipeleka fedha katika halmashauri kwa ajili ya ununuzi na utengenezaji wa madawati. Mwaka 2010/2011 shilingi bilioni tatu zilipelekwa katika halmashauri zote kwa ajili ya madawati ambapo Mkoa wa Mara ulipata shilingi milioni 197 na mwaka 2012/2013 shilingi bilioni moja zilipelekwa katika halmashauri zote kwa ajili ya madawati na Mkoa wa Mara ukapata shilingi milioni 68.

• Kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi Serikali imekuwa ikitoa fedha za uendeshaji wa shule (ruzuku) kwa kiwango cha shilingi 10,000 kwa kila mwanafunzi. Hadi kufikia mwezi Machi, 2013 Serikali imeshatoa jumla ya shilingi bilioni 60 za ruzuku kwa shule za msingi nchini kote. Kiasi hiki ni sawa na shilingi 7,565 kwa mwanafunzi ambayo ni sawa na asilimia 75.


Je, ahadi hizi zimetekelezeka? wananchi husika wa maeneo ambako ahadi hizi zililengwa kwao wana wajibu wa kufuatilia na kuhakikishwa zimetekelezwa. Tafakari na chukua hatua kwa maendeleo ya Taifa lako sasa.

Unaweza kupata habari hizi kila wakati kwa ku-click “LIKE” au katika “facebook page” yangu: Maxmillian Kattikiro FB-Page