Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudumu ya
Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge
|
WAKATI
Watanzania wakisubiri hatima ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo, ambaye Rais Jakaya Kikwete alisema anamuweka kiporo kutokana na kashfa
ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow,
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge, ametangaza
rasmi kuachia nafasi hiyo.
Bunge
lililopita baada ya kujadili ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG), kuhusu miamala iliyofanyika kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow
iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania, lilipitisha maazimio manane ikiwa
ni pamoja na kuazimia kuwajibishwa viongozi wa Serikali na wale wa kamati za
Bunge walioonekana kuhusika katika kashfa hiyo.
Viongozi
wa kamati ambao Bunge liliazimia wawajibishwe ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Bajeti, Chenge, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba,
Sheria na Utawala, William Ngeleja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Nishati na Madini ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa
Tanesco, Victor Mwambalaswa.
Kwa
mujibu wa taarifa ambazo tulizipata jana, Chenge alitangaza kujiuzulu nafasi
yake juzi baada ya kamati yake kukutana kwenye ofisi ndogo za Bunge jijini Dar
es Salaam.
“Amejiuzulu
jana (juzi), saa tano asubuhi wakati wa kikao cha Kamati ya Bajeti
kilichokutana kwenye Ukumbi wa Mkwawa, ofisi ndogo za Bunge Dar es Salaam.
“Aliwaambia
wajumbe kuwa hataki malumbano na wabunge na hataki msuguano wowote, nafasi yake
kwa sasa inashikiliwa na Dk. Festus Limbu, ambaye alikuwa makamu mwenyekiti wa
kamati,” alisema mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo.
Mkurugenzi
wa Idara ya Shughuli za Bunge, John Joel, alipotakiwa kuthibitisha suala hilo,
alisema hayuko ofisini, hivyo hawezi kuwa na jibu la moja kwa moja juu ya suala
hilo.
Alisema
kama Chenge mwenyewe amefikia uamuzi huo, atakuwa amempunguzia kazi Spika.
Joel
alisema kujiuzulu kwake kutakuwa ni kutimiza maazimio ya Bunge jambo ambalo ni
lazima litekelezwe.
Akifafanua
juu ya kumpata mwenyekiti mpya wa kamati hiyo, Joel alisema mara baada ya
wajumbe hao kukutana kama viongozi hawapo, jambo la kwanza ni kufanya uchaguzi.
Alisema
Chenge alichaguliwa na Spika kuongoza kamati hiyo kwa kuwa ilikuwa ni kamati
mpya na ambayo ni nyeti sana.
“Wajumbe
wake ukiangalia wengi walitoka kwenye Kamati ya Kushauri Vyanzo Vipya vya
Mapato, Spika aliomba kumchagua mtu ili apate mtu makini anayejua vyanzo vya mapato,”
alisema.
Naibu
Spika wa Bunge, Job Ndugai, alipoulizwa kama ofisi yake ina taarifa za
kujiuzulu kwa Chenge, alisema yupo jimboni na hana taarifa hizo ila anachojua
suala la kuwajibika kwa wenyeviti waliotajwa kwenye ripoti ya Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) juu ya kashfa ya Escrow ni la lazima na
halihitaji mtu kuandika barua ya kujiuzulu.
“Hakuna
kuandika barua ya kujiuzulu, yale ni maamuzi ya Bunge, kinachotakiwa ni kamati
kukaa na kuchagua viongozi wengine,” alisema.
Ndugai
akizungumza alisema kamati ambazo viongozi wake walihusishwa na kashfa ya
Tegeta Escrow, zitakapokutana jukumu la kwanza litakuwa ni kuchagua viongozi
wapya kwani tayari chombo hicho kilishaazimia kuwawajibisha.
Katika
kashfa ya Escrow, Chenge anadaiwa kupokea Sh bilioni 1.6, kutoka kwa James
Rugamalira ambaye ni mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering iliyokuwa na
asilimia 30 kwenye Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL),
inayodaiwa kuuzwa kinyemela kwa Kampuni ya Pan African Power (PAP).