To Chat with me click here

Thursday, November 14, 2013

KAGASHEKI ANASWA KONTENA LA PEMBE ZA NDOVU

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamisi Kagasheki
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, amekamata kontena la futi 40 likiwa limesheheni pembe za ndovu kisiwani Unguja, Zanzibar jana alasiri.
Akizungumza na vyanzo vya habari hii kwa simu jana kutoka kisiwani humo, Waziri Kagasheki alisema kuwa kontena hilo lilikuwa likitokea Bandari ya Dar es Salaam na kwamba watu wawili wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi wakilisaidia Jeshi la Polisi.
Waziri Kagasheki alisema kuwa hadi sasa haijulikani mzigo huo una thamani kiasi gani na kwamba unasadikiwa kumilikiwa na raia wa China.
Alisema kuwa operesheni hiyo ni endelevu ili kuwabaini wahusika wanaojihusisha na biashara hiyo haramu ya ujangili.
Tukio hilo linakuja zikiwa ni wiki mbili tangu waziri huyo kukamata pembe za ndovu 706 jijini Dar es Salaam zikimilikiwa na raia wa China.
Pembe hizo 706 ni sawa na tembo 353 waliouawa katika hifadhi za wanyamapori hapa nchini.
Wachina hao walikamatwa katika Mtaa wa Kifaru, Mikocheni wilayani Kinondoni chini ya operesheni iliyoongozwa na Waziri Kagasheki, ambaye aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Tarish Maimuna.
 
Waliokamatwa na shehena hiyo ya pembe za ndovu ni raia watatu wa China, ambao ni Xu Fujie, Chen Jinzha na Huang Qin wote kutoka mji wa Guandung, ambao wamefikishwa mahakamani wiki iliyopita.

KASHFA NZITO TUME YA UCHAGUZI

Naibu Katibu Mkuu Chadema - Mhe. Zitto Kabwe
TUME ya Uchaguzi nchini (NEC) inadaiwa kuingia katika mchakato wa mwisho wa kuzipa zabuni ya kuandaa vifaa vya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 kampuni za M/S Jazzmatrix Cooperation na M/S Invu IT Solution zinazodaiwa kuwa na rekodi mbaya ya utendaji.

Tanzania Daima limedokezwa kuwa mkakati huo unahusishwa na  njama za kutaka kukibeba Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi huo kwa kuchakachua matokeo ya kukibakiza madarakani.

 Kampuni hizo ambazo katika zabuni ya Tume ya Uchaguzi zimetajwa kushirikiana na Kampuni ya Kitanzania ya M/S SCI Tanzania Limited, mbali ya kutojulikana zinapotoka, pia ndizo zimekuwa na gharama kubwa kuliko kampuni nyingine zilizoomba kazi hiyo.

Kiwango ambacho kampuni hizo zilitaja na kukubaliwa na NEC kwa ajili ya kuandaa vifaa vya kielektroniki vya kusajili wapiga kura (Biometric Voters Registration) ni zaidi ya euro milioni 60, sawa na sh bilioni 126.3, wakati kampuni zinazofuata zikihitaji kuanzia euro milioni 40.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, ni mmoja wa viongozi waliofichua mkakati huo, akidai unafanywa na serikali ya CCM ili kuhakikisha wanajiandaa kudhibiti kila eneo ili waweze kubaki madarakani.

Alisema lengo ni kuhakikisha mchakato wa vitambulisho vya kupigia kura vya kielektroniki vina kuwa na faida kwa CCM na kukiingizia fedha chama hicho za kutumia kwenye uchaguzi huo kupitia mfumo huo dhaifu wa vitambulisho hivyo.

Zitto alisema kutokana na hali hiyo, amemwandikia Mdhibiti na Mkaguzi  Mkuu wa Serikali (CAG) barua ya kutaka ukaguzi wa zabuni hiyo ufanyike kwa kushirikisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na vyombo vingine vya usalama kwa ajili ya kujiridhisha.

“Wenzetu CCM wanafanya mikakati ya kujiandaa na Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kuhakikisha wanapata fedha za kutosha na hata mazingira mabaya ya vifaa vitakavyotumika katika upigaji kura na sasa wameshaingia hata katika Tume ya Uchaguzi kwa ajili ya kutengeneza mazingira,” alisema Zitto.

Aliongeza kuwa kiasi kilichotolewa ni kodi ya Watanzania na kwamba ni vema taifa likajiridhisha kuwa matatizo yaliyotokea Kenya na Ghana hayatajirudia Tanzania, hasa wakati wa upigaji kura.

 Gazeti hili limeona barua hiyo ya Zitto kwenda kwa CAG, ya Novemba 7, 2013, yenye kichwa cha habari; ‘Zabuni ya  Biometric Voters Registration (BRV KITS) No. IE/018/2012-13/HQ/G/19 yenye thamani ya sh bilioni 126.3.’

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini anasema kuwa  NEC imekuwa katika mchakato wa zabuni tajwa hapo juu.

“Zabuni hiyo sasa imeanza kuleta malalamiko miongoni mwa wananchi kutokana na kinachosemekana kuwa kampuni iliyopewa zabuni hiyo haina uwezo kiteknolojia, pia bei zao ni kubwa.

“Katika mafunzo ya hivi karibuni ya SADCOPAC jijini Nairobi tuliazimia kuwa ni vema kwenye zabuni nyeti kama za namna hii, SAIs wawe na uwezo wa kufanya ukaguzi kabla ya zabuni kutolewa na kuanza kutekelezwa,” alisema.

Tuesday, November 12, 2013

JOHN MNYIKA AZUNGUMZA JUU TAARIFA YA SIRI YA CHADEMA KUHUSU ZITTO KABWE KUPOKEA PESA KUTOKA CCM ILI KUIHARIBU CHADEMA

Katibu Mwenezi wa Chadema; John Mnyika
Mgogoro ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), umeingia katika sura mpya baada ya viongozi wake wawili waandamizi, Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo kuuandikia uongozi wa chama hicho wakitaka uikane taarifa inayowachafua mitandaoni.
Zitto na Dk Mkumbo wanatuhumiwa kupokea fedha na kushirikiana na viongozi wa Idara ya Usalama wa Taifa na wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa nia ya kuivuruga Chadema.
Taarifa hiyo yenye kichwa cha habari 'Ripoti ya siri juu ya Zitto Kabwe’, ambayo imesambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii katika siku za karibuni inadaiwa kuwa iliandaliwa na Kitengo cha Upelelezi cha Chadema baada ya uchunguzi wa mwenendo wa Zitto ndani na nje ya nchi kuanzia mwaka 2008.
Sehemu ya taarifa hiyo ya mtandaoni inadai kuwa Zitto alipelekewa kiasi cha Dola za Marekani 266,000 (Sh416 milioni) huko Ujerumani na maofisa wa Usalama wa Tanzania, Desemba 16, 2009.
 
Ripoti hiyo inadai kuwa fedha hizo zilipitishwa katika Benki ya Berliner ya Ujerumani kwenye akaunti ya raia wa nchi hiyo, Andrea Cordes, ambaye anadaiwa kumpelelekea Zitto.
 
Taarifa zaidi zinadai kuwa fedha hizo ziligawiwa kwa wafuasi mbalimbali wa chama hicho na miongoni mwao ni Dk Mkumbo.
Zitto amlima barua Dk Slaa
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Zitto alisema amemwandikia barua Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa kumwomba athibitishe ‘Taarifa ya Siri ya Chadema’ kama ni ya kweli au chama hicho kiikanushe ili aweze kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waandishi wa kile alichokiita ‘hekaya.’

“Taarifa ya Chadema inasema kwamba chama hicho (chama changu), kilikuwa kimechunguza mwenendo wangu tangu mwaka 2008 hadi 2010 na kubaini kuwa mimi ninapokea fedha kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuivuruga Chadema,” alisema Zitto kwenye taarifa yake.
Zitto alisema taarifa hiyo ni ya kutunga na iliyojaa uongo wa kiwango cha kutisha, imemfedhehesha, imemsikitisha na kumkasirisha.
Alisema taarifa hiyo iliibuliwa katika kipindi ambacho alikuwa ziarani barani Ulaya katika nchi za Uswisi na Uingereza ambako alikuwa anafuatilia fedha zilizofichwa na Watanzania katika nchi hizo.

“Pengine lengo la ripoti hiyo lilikuwa ni kutaka kunipoteza kutoka katika nia na dhamira yangu ya dhati ya kutaka Watanzania wafaidike na utajiri wao. Muda ambao watunzi wa ripoti hiyo waliamua kutoa taarifa yao unazua maswali mengi kuliko majibu,” alieleza Zitto katika taarifa yake.
 
Dk Mkumbo alia na uenezi
Dk Mkumbo alieleza kusikitishwa na Idara ya Uenezi ya Chadema kwa kukaa kimya bila kutoa maelezo juu ya suala hilo.
“Hasa pale ambapo tumeambiwa waraka huu umetoka makao makuu. Hii si kawaida kwa idara yetu hii nyeti iliyosheheni watu mahiri. Mara zote huwa wepesi kabisa kwa vijana wetu katika idara hii kutoa ufafanuzi, tena kwa mambo mepesi kabisa yanayokigusa chama, vipi makamanda kwenye jambo hili imekuwaje?” aliandika Dk Mkumbo kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Facebook jana na kuthibitisha kwa simu. Dk Kitila alisema pamoja na umaskini wake, hajawahi kuhongwa popote na wala hatarajii.
 
“Taarifa zinazosambazwa kuhusu mimi ni za uongo wa kijinga na uzushi wa kitoto kwa malengo ya siasa nyepesi. Ni wazi kwamba wanaosambaza habari chafu kunihusu hawanijui na ndiyo maana wanaweza kudiriki kuzusha kwamba mimi Kitila Mkumbo naweza kuhongwa Sh200,000.”
 
Alihoji pia Chadema ilikuwa na siri gani za hatari kiasi cha kumfanya Zitto, ambaye ni rafiki yake wa siku nyingi kuhongwa kiasi hicho kikubwa cha fedha.

Mnyika awajibu
Hata hivyo, Katibu Mwenezi wa Chadema, John Mnyika ameikana ripoti hiyo na kueleza kuwa haijaandikwa na makao makuu ya Chadema.
Mnyika alisema Zitto ameibua kitu ambacho anafahamu kuwa kimeshughulikiwa na uongozi wa chama hicho.
 
“Zitto anajua kuwa Andrea Cordes aliniandikia baruapepe na nakala kwake nikawajibu kuwa ripoti hiyo haijaandikwa na Makao Makuu ya chama na tukipokea malalamiko rasmi tutachunguza kwa sasa chama kinaichukulia ripoti hiyo kama ripoti nyingine zinazosambazwa mitandaoni,” alifafanua Mnyika.

Akizungumzia malalamiko ya Dk Mkumbo, Mnyika alisema alikuwa anapaswa kufuata taratibu za chama kama alikuwa na malalamiko.
Alisema baada ya taarifa hiyo ya siri kusambaa mtandaoni, Zitto alitoa kauli na kama Dk Mkumbo hakuridhika, alipaswa kuonana na watu wa Idara ya Uenezi ya Chadema.

“Idara ingetoa ufafanuzi zaidi. Mjadala huu usikuzwe bila sababu za msingi na kufunika masuala mengine muhimu ya kitaifa,” alisema Mnyika. 
Chanzo: Mwananchi