Tumekutana leo wakati ambao Taifa letu lipo katika mpito wa mambo 
mengi sana. Kufuatia shinikizo kubwa kutoka chama chetu cha CHADEMA na 
asasi nyingine za kiraia ikiwemo viongozi wa dini, tupo katika mchakato 
wa kuandika upya katiba ya nchi yetu. Lakini pia kuna muamko mkubwa sana
 wa haki za kiraia na haki za kisiasa katika Taifa letu hivi sasa. 
Watanzania, kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya nchi yetu, 
wameamka na kutaka mabadiliko ya kisiasa na hasa kutaka kabisa uongozi 
mpya wa nchi kutoka chama kingine tofauti na chama kinachoongoza hivi 
sasa. Huu mpito pia, Mpito wa kutoka chama kimoja hodhi kwenda mfumo wa 
kweli wa vyama vingi vya siasa. Watanzania wameamka sana kujua 
rasilimali za nchi yao na kutaka kutokomeza rushwa na ufisadi na 
matumizi mabaya ya utajiri wa nchi. Huu ni mpito wa kutoka viongozi 
wanaojali maslahi yao binafsi na kwenda kwa viongozi wawajibikaji na 
wenye uchungu wa kuendeleza nchi yetu na watu wake.
Mpito wowote unapaswa kuongozwa vyema. Unapaswa kushirikisha wananchi
 wote bila kujali wapo sehemu gani ya Dunia. Chama chetu kipo mstari wa 
mbele kuongoza mpito tulionao Tanzania. Licha ya kuongoza juhudi za kuwa
 na Katiba mpya itakayohakikisha HAKI na Wajibu wa Watanzania, lakini 
pia tumekuwa tukiendelea kupambana na rushwa na ufisadi. Pia tumekuwa 
tukiendelea kuhakikisha utajiri wa nchi yetu unatumika kwa manufaa ya 
Watanzania. Hatujatetereka hata kidogo na hatutateterekea kuhakikisha 
Watanzania wanakuwa na Taifa lenye demokrasia iliyokomaa, lenye 
maendeleo na ustawi wa watu wake (Developmental Democratic State).
Licha ya kwamba tupo Upinzani, lakini hatua mbalimbali tulizochukua 
zimeleta mabadiliko makubwa katika nchi yetu. Kuanzia vuguvugu la 
Buzwagi mpaka kuibuliwa kwa maskandali ya EPA na mpaka kutajwa kwa 
orodha ya Mafisadi nchini pale MwembeYanga. Hata hivi karibuni juhudi za
 Bunge kutaka Uwajibikaji Serikalini zilizoongozwa na CHADEMA zimeleta 
mabadiliko. Inawezekana mabadiliko hayo sio kama tutakavyo, sio kamili, 
lakini ni hatua ambayo tumepiga. Tutaendelea kama chama cha siasa sio tu
 kusema na kupiga kelele kuhusu uoza uanaofanyika Serikalini (maana ndio
 kazi yetu kikanuni) lakini pia kutoa masuluhisho ya matatizo ya nchi 
yetu na kusukuma kupitia Bunge mabadiliko chanya yanayotakiwa ili kuleta
 mabadiliko nchini.
Ni matumaini yangu kwamba Watanzania wanaoishi nje ya nchi, kokote 
walipo watashiriki pamoja nasi katika vuguvugu (movement) hili la kuleta
 mabadiliko katika Taifa letu. Hampaswi kukaa na kutazama, bali mnapaswa
 kushiriki kikamilifu maana hii ni nchi yetu sote. Ni wajibu wa kila 
mmoja wetu kuhakikisha nchi yetu inakuwa na demokrasia na ustawi wa watu
 wake.
Hali ya Uchumi wa Nchi
Tumekuwa moja ya nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi zaidi 
duniani. Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita uchumi wa Tanzania 
umekuwa ukikua kwa wastani wa asilimia 6. Kazi hii ya ukuaji 
ukilinganisha na kiwango cha ukuaji wa idadi ya watu (ambacho ni 2.8%) 
ingeweza kupunguza umasikini kwa zaidi ya 50% katika kipindi hicho. Hata
 hivyo Umasikini Tanzania umebakia ni mkubwa ambapo zaidi ya Watanzania 
37 katika kila Watanzania 100 hawana uhakika wa mlo mmoja kwa siku. 
Idadi ya Watanzania masikini wa kutupwa (wenye kipato cha chini ya tshs 
500 kwa siku) imeongezeka kutoka watu milioni 12 mwaka 2007 mpaka watu 
milioni 15 mwaka 2011. Ukitaka kujua wingi huu ni wa kiwango gani, 
chukua idadi ya watu wa Nchi ya Botwasana, Namibia, Swaziland na Lesotho
 haikaribii idadi ya Watanzania wenye mashaka ya mlo mmoja kwa siku. 
Idadi ya watu wa Denmark, Netherlands, Norway na Uholanzi kwa pamoja 
ndio sawa na idadi ya Watanzania masikini. Kwa nini?
Ni kitendawili. Ni nadra kukuta uchumi unaokua kwa kasi kama wetu ukizalisha masikini zaidi. It’s a paradox of a fast growing economy and increasing poverty.
 Kwa miaka kumi ambayo tumeiangalia (2000 – 2010) tumeshuhudia kwa 
dhahiri kabisa kushindwa kwa sera za kuondoa umasikini zinazotekelezwa 
na Serikali ya CCM.
Masikini wa Tanzania wapo vijijini zaidi. Uchumi wa vijijini kwa 
kipindi cha muongo mmoja umekua kwa wastani wa asilimia moja tu. Flat lining.
 Kwa hiyo uchumi unaokua hivi sasa sio uchumi wa Watanzania bali ni 
uchumi wa watu wachache kwenye sekta chache kama madini, mawasiliano na 
ujenzi. Watanzania walio wengi walioko vijijini wanaendelea kuandamwa na
 ufukara bila juhudi mahususi za kuwasaidia. Tumesema na tunarudia 
kusema kwamba ni lazima kubadili mwelekeo wa mipango yetu na kujikita 
kwenye maendeleo vijijini. Kama chama tunaendelea kusema jambo hili 
ndani ya Bunge na pia kuwaelimisha wananchi kwenye mikutano yetu ya 
hadhara.
Mfumuko wa Bei umefikia kiwango cha juu sana cha 19% na hivyo hata 
mikopo katika mabenki imekuwa ghali hadi kufikia riba ya 23% na zaidi. 
Mfumuko wa bei unaongozwa na bei ya vyakula. Katika hali ya kawaida, 
kupanda kwa bei za vyakula kungemnufaisha mkulima lakini hali sio hiyo 
Tanzania. Mkulima bado anauza mazao yake kwa bei za vijijini ambazo ni 
ndogo na zinaamuliwa na wachuuzi wa mijini. Lakini mkulima huyu 
anaponunua bidhaa za matumizi yake kama sukari, mafuta ya taa, nguo nk 
ananunua kwa bei za mijini ambazo zimeathiriwa vikali na mfumuko wa bei.
 Hivyo mfumuko wa Bei unamuathiri zaidi mwananchi masikini kabisa. 
Serikali imekuwa mlalamikaji kama wananchi wengine. Mfumuko wa Bei 
utapungua kwa kuongeza uzalishaji wa chakula, kuimarisha miundombinu ya 
vijijini na kupunguza gharama za Nishati kama hasa Umeme. CHADEMA 
inaendelea kuisukuma Serikali kuchukua hatua ili kupunguza makali ya 
maisha kwa wananchi. Hatua za muda mfupi zihusishe nafuu ya kodi kwenye 
bidhaa zinazotumiwa na wananchi kwa wingi.
Hata hivyo bado matumizi ya Serikali ni makubwa mno kwenye masuala 
ambayo hayana uhusiano na kuendeleza watu. Bado bajeti ya posho 
mbalimbali, safari za nje na hata matumizi makubwa ya magari ya serikali
 ni kubwa mno kulinganisha na hali yetu ilivyo. Katika matumizi haya pia
 kuna ufisadi mkubwa sana. CHADEMA inaendelea kuanisha masuala haya na 
kukemea na kuchukua hatua pale inapobidi.
Uwezo wetu wa kukusanya mapato ni changamoto kubwa. Mapato mengi 
yanapotea kama misamaha ya kodi ambayo sasa imefikia tshs 1.3trn kwa 
mwaka. Mapato mengine hayakusanywi kwa sababu ya ukwepaji kodi 
uliokithiri. Kodi kwenye Sekta ya Madini imekuwa ni mjadala wa muda 
mrefu sana. Sheria ya madini ya mwaka 1998 na Sheria za Fedha ya mwaka 
1997 ziliweka mfumo wa kinyonyaji kabisa ambao ulikuwa unafaidisha 
makampuni ya uchimbaji madini kuliko Taifa. Sheria mpya ya madini ya 
mwaka 2010 ambayo ilitokana na kazi kubwa tuliyofanya ndani ya Bunge 
pamoja na Mashirika yasiyo ya kiserikali imeweka mfumo bora zaidi. Hata 
hivyo makampuni ya Madini yaliweka mgomo kwenye sheria mpya kwa kukataa 
kuanzisha miradi mipya na hata kukataa kuhamia kwenye sharia mpya. 
Sheria mpya inataka Serikali kuwa na hisa kwenye kila mgodi, hisa za 
kampuni za madini kuorodheshwa katika Soko la hisa la Dar es Salaam na 
kulipwa kwa mrahaba mpya wa asilimia 4 kwa kanuni mpya ya kukokotoa 
mrahaba (from Netback Value to Gross value) ambayo ingeongeza mapato ya 
Serikali maradufu. Kwa miaka Serikali imekuwa inapoteza mapato kwa 
kutotekelezwa kwa sharia mpya. Nimesikia kuanzia mwezi huu kampuni ya 
Barrick imeanza kulipa mrahaba mpya. Tutataka maelezo ya Serikali kuhusu
 kampuni nyingine na pia mrahaba wa miaka ya nyuma. Ni lazima Serikali 
ihakikishe nchi inafaidika na rasilimali zake.
Tunaenda kwenye Uchumi wa Gesi Asilia. Makampuni mawili makubwa 
duniani yamegundua Gesi Asilia nchini kwa kiwango kikubwa sana. Hivi 
sasa Tanzania ina Utajiri wa Gesi ulitothibitishwa wa 20TCF na makadirio
 yanaonyesha kuwa tutafika 85TCF katika kipindi kifupi sana. Bado kuna 
meneo yanaendelea kufanyiwa utafutaji kutokanana vitalu vilivyogawiwa. 
Hata hivyo hatuna Sera na Sheria ya kusimamia vema sekta hii na hasa 
yenye kuhakikisha Uwazi na Uwajibikaji. Hatuna pia Sheria ya kusimamia 
mapato yanayotokana na Gesi Asilia (Petroleum Revenue Management Act). 
Hatutaki kurudia makosa yaliyofanyika kwenye sekta ya Madini. Tunataka 
Gesi Asilia itumike kwa maendeleo ya watu wetu.
Tumependekeza kwamba Vitalu vipya vya kutafuta mafuta visitolewe kwa 
sasa (moratorium) mpaka hapo Sera mpya, Sheria mpya na mfumo bora wa 
matumizi ya Fedha zitakazotokana na Mafuta na Gesi ziwepo. Pia shughuli 
za utafutaji katika vitalu vya sasa zitaongeza thamani ya vitalu vijavyo
 na hivyo nchi kufaidika zaidi. Tumependekeza pia kwamba ni lazima 
kuweka mfumo mzima wa uwazi na uwajibikaji katika sekta ili kujipanga 
vyema na kuepuka yaliyowakuta wenzetu wenye utajiri kama huu ambao 
uligeuka balaa. Tatu tumependekeza kusomesha Watanzania kwa ngazi zote. 
Mafundi mchundo kupitia VETA na Mafundi wa kati kupitia Vyuo vya Ufundi.
 Muhimu zaidi tunataka kijengwe Chuo Kikuu kikubwa Mtwara chenye Kampasi
 Lindi ambacho kitakuwa ni kituo cha kufundisha sio watanzania tu bali 
Waafrika wengine kuhusiana na masuala haya. Ujenzi wa Chuo Kikuu Mtwara 
unapaswa kuanza mara moja bila kuchelewa.
Kutokana na uzoefu tuliupata katika sekta ya Madini na kupitisha 
sharia mbaya Bungeni, tunaona kwamba suala la Gesi tukabe kila mahala 
ili kuhakikisha nchi inafaidika. Historia inatuonyesha kwamba Nchi 
nyingi za Kiafrika zenye utajiri wa Gesi na Mafuta hazina demokrasia, 
zimegubikwa na uvundo wa ufisadi na watu wake ni masikini. Tunataka 
kuonyesha Dunia kwamba inawezekana kuwa nan chi ya Kiafrika yenye 
utajiri mkubwa wa Mafuta na Gesi na ikawa ya kidemokrasia, isiyo na 
ufisadi na yenye watu wenye ustawi. Sio kazi rahisi lakini tumedhamiria.
 CHADEMA haitakaa tu kuona utajiri wan chi unatapanywa hovyo. Tumesema 
na kusimamia kwenye Madini, tunatoa mwongozo kwenye Mafuta na Gesi.
Katiba
Ninajua Watanzania mnaoishi nje mna shauku kubwa ya kujua ushiriki 
wenu na hatma yenu kwenye Katiba mpya. Kwa muda mrefu mmekuwa 
mkishawishi haki ya kupiga kura, haki ya kuwa na uraia zaidi ya mmoja 
(Dual Nationality) na hata namna gani mnashiriki katika kujenga uchumi 
wa nchi.
Kwanza nataka niwapongeze kwa kuchukua uamuzi mzito wa kuondoka 
nyumbani kuja ughaibuni kutafuta maisha au maarifa au vinginevyo. 
Nawapongeza zaidi kwa juhudi mnazofanya kusaidia familia zenu nyumbani, 
vijiji vyenu na hata Taifa kwa ujumla. Takwimu zilizotangazwa na Benki 
Kuu ya Tanzania zinaonyesha kwamba Watanzania mliopo nje ya Tanzania 
mlituma nyumbani fedha (remittances) zaidi ya Dola za kimarekani 350 
milioni mwaka 2011. Hii ni sawa na asilimia 5 ya mapato yote ya Fedha za
 kigeni zilizoingia Tanzania mwaka huo na ni zaidi ya Fedha za kigeni 
zilizoingizwa na Chai, Kahawa, Pamba na Korosho kwa ujumla wake. Kwa 
hiyo ‘Diaspora’ ni sehemu muhimu sana ya Uchumi wa Taifa ni muhimu Dola 
iwawekee mazingira mazuri ya kuweza kufanikisha mambo yenu huku ili 
mshiriki vema maendeleo ya nchi yetu.
CHADEMA tunatambua umuhimu wenu hata kama msingekuwa mnatuma fedha 
nyumbani. Ninyi ni Watanzania na ni jukumu la Dola ya Jamhuri ya 
Muungano wa Tanzania kuwalinda popote mlipo duniani. Mtakumbuka mwanzo 
mwa miaka ya 2000 kulikuwa kuna ‘petition’ ya kudai Uraia wan chi mbili 
kwa Watanzania. Dkt. Willibrod Slaa alikuwa ni mmoja wa Wabunge 
waliokuwa wanauliza maswali Bungeni kuhusu jambo hilo. Wengi tuliweka 
sahihi katika ‘petition’ ile ambayo ilianzishwa na Watanzania wanaoishi 
nje. CHADEMA inaunga mkono haki ya Watanzania kuwa na uraia wa nchi 
nyingine. CHADEMA inataka suala hili lifikie mwisho kwenye mjadala wa 
Katiba. Kuna watu wanasema sio uzalendo Mtanzania kuchukua uraia wa nchi
 nyingine. Ninasema sio uzalendo pia kuacha raia wako wanateseka nchi 
nyingine kwa sababu tu wamechukua uraia wa huko au wanashindwa kuchukua 
uraia wa huko. Sheri zetu za Uraia ni gandamizi hasa kwa wanawake wa 
Tanzania. Tumepoteza dada zetu wengi sana na watoto wao kwa sababu 
wakiolewa na wageni watoto wao hawana haki ya kuwa raia. Wakinyanyaswa 
na wageni na kutaka kurudi nyumbani wao na watoto wao wananyanyaswa pia 
kwao. Haikubaliki na tutakabili suala hili kwa nguvu zetu zote. Tunataka
 Watanzania walioko nje wapate kila aina ya msaada kutoka Dola yetu ili 
wafanikiwe.
CHADEMA inataka pia Watanzania waliopo nje waruhusiwe kupiga kura 
nyakati za uchaguzi. Ni suala la ushamba tu kuendelea kujadili jambo 
hili la uwazi kabisa. Kuna teknolojia za kisasa kabisa kuhakikisha watu 
wanapiga kura kokote walipo. Mwaka 2004 Chama rafiki cha CHADEMA kutokan
 Msumbiji RENAMO kiliniteua kuwa wakala wa kura katika kituo cha Ubalozi
 wa Tanzania Msumbiji uliopo Dar es Salaam. Raia wa Msumbiji wanaoishi 
Tanzania wanapiga kura nje, seuze Tanzania? CHADEMA inawahakikishia 
kulisimamia jambo hili.
Katika mkutano wa Bajeti ujao Bajeti Kivuli itazungumzia namna ya 
kuimarisha uwekezaji wa Watanzania wanaoishi nje katika uchumi wa nchi. 
Siku zote tunazungumzia mitaji kutoka nje kwa maana ya ‘Foreign Direct 
Investments’ peke yake na kwa kweli tunasahau kwamba kuna ‘Diaspora 
Direct Investments’. Tumetoa vivutio vingi sana kwa Wawekezaji kutoka 
nje. CHADEMA inakwenda kupendekeza kuwepo kwa vivutio vya kikodi na 
kirasimu kwa Watanzania wanaoishi nje wanaotaka kuwekeza nyumbani. 
Ninawashawishi muangalie namna ya kujikusanya na kuwa na ‘Investments 
Funds’ ili kununua ‘equties’ kwenye miradi mbalimbali. Uwekezaji 
Tanzania unalipa sana (Return on Investments goes up to 25%) kwenye 
baadhi ya maeneo. Huduma katika sekta zinazoinukia kama Mafuta na Gesi 
ni eneo ambalo mnapaswa kuliangalia tusiachie wageni tu. Mnakumbuka 
wakati wa mwanzo wa Sekta ya Madini hata huduma za kufua nilikuwa 
zinatolewa na kampuni kutoka Australia! Mtwara hakuna vyumba vya kutosha
 vya mahoteli na hata nyumba za kupanga, angalieni maeneo haya maana 
Mtwara is booming. Sisi kama wanasiasa jukumu letu ni kuwawekea 
mazingira mazuri. Ninyi mnapaswa kuzileta hizo Dola kidogo mpatazo 
nyumbani na kuwekeza kwenye maeneo yatakayozalisha ajira na hivyo 
kuondoa umasikini kwa ndugu zenu. Ninaamini mtachukua changamoto hii na 
kuangalia namna ya kuitekeleza. Wenzetu kutoka Ethiopia na Kenya 
wanafanya hivi.
Mjadala wa Katiba pia na hatimaye Katiba mpya itaamua hatma ya 
Muungano wetu. Muungano pekee katika Bara la Afrika ambao umedumu na 
umeonyesha nia ya Mwafrika kukataa mipaka ya kikoloni. Kuna Watu wanaona
 Muungano huu haina manufaa hivyo uvunjwe. Kuna watu wanaona ni bora 
kuurekebisha ili uweze kufaidisha Jamhuri mbili zilizoungana. Mchakato 
wa Katiba mpya kupitia Tume ya Katiba ambayo CHADEMA tumeshiriki, ni 
nafasi ya kuandaa mustakabali wa Tanzania ijayo. Tanzania tunayoitaka 
kwa miaka mingine hamsini, mia moja au hata alfu moja. Watanzania wawe 
huru kusema wanataka Muungano au hawautaki, wanataka Muungano wa namna 
gani na wanataka Tanzania ya namna gani.
Ni Haki ya Watanzania wanaoishi nje kutoa maoni yao kuhusu Katiba. 
CHADEMA inakusudia kwanza kukusanya maoni ya wanachama wake walioko nje 
kuhusu Katiba lakini pia kuitaka Tume ya Jaji Warioba kuja huku kukutana
 na Watanzania na kupata maoni yao. Ni Haki yenu kutoa maoni na 
ninawaomba mtumie haki yenu vizuri. Mtupe uzoefu wa nchi nyingine ambazo
 mmeishi na kuweza kuona ni vipi tutaimarisha Dola imara ya Kidemokrasia
 yenye kuleta ustawi wa watu wake.
Msimamo wa CHADEMA ni Muungano wa Serikali Tatu. Hata hivyo katika 
mchakato tulio nao sasa wanachama wa CHADEMA wana uhuru wa kutoa mawazo 
mapya na kuboresha sera hii ya CHADEMA kuhusu Muungano. Muwe huru kabisa
 kutoa maoni yenu.
Haki na Wajibu
Watanzania mnaoishi nje mna haki na lazima Dola ilinde haki hizo 
lakini pia kama Watanzania mna wajibu kwa nchi yenu. Ni wajibu wenu 
kushiriki kikamilifu katika kuimarisha demokrasia nchini. Sisi wenzenu 
tumejitoa muhanga katika eneo hili. Tumejenga taasisi zinazoitwa vyama 
vya siasa kwa zaidi ya miaka ishirini sasa. Hatuchoki lakini tunahitaji 
ushiriki wenu. Jambo hili sio kwa wanachama wa CHADEMA peke yake bali 
pia hata wanachama wa vyama vingine mnaoishi hapa Marekani.
Hutakuwa mwanachama bora wa CCM kwa kufanya kazi ya kuwachoma 
Watanzania wenzako ambao ni wana mageuzi kwa viongozi kila wanapokuja 
kwenye ziara nje ya nchi. Utakuwa mwanachama mzuri wa chama chako iwapo 
utawaambia viongozi ukweli wa mambo na namna bora ya kuongoza nchi yetu.
Hamuitendei haki Tanzania kwa kusemana, kusingiziana, kutetana na 
hata kugombana.  Wakati mwingine unapoona mijadala ya watu kwenye 
mitandao ya kijamii unasinyaa. Unajiuliza sasa kama hawa ndio wapo 
kwenye mwanga sisi tulio kwenye giza inakuwaje?
Fanya kazi. Furahia maisha. Lakini kumbuka kuna nchi yenye barabara 
za mashimo, yenye giza muda mwingi wa mwaka kuliko mwanga, yenye 
umasikini, yenye viongozi wasiwajibika na wala rushwa. Ni nchi yako. 
Usiseme hii ni kazi ya kina Zitto, Slaa, Mbowe, Nassari, Leticia na 
Msigwa. Kila mtu ana wajibu wa kufanya kuisogeza mbele nchi yetu. Timiza
 wajibu wako kwa namna unavyoona inafaa.
Nkrumah once said ‘organise, don’t agonise’ narudia hivyo kwa Watanzania mliopo Marekani. Organise for your motherland.
Tanzania yenye usawa wa fursa
Nimalizie kwa stori yangu. Nilizaliwa katika umasikini wa kutisha 
kama Watanzania wengi wa vijijini. Nimekwenda shuleni bila viatu na 
wakati mwingi tumbo likiwa tupu ama nimekunywa uji wa unga wa Yanga 
uliotiwa chumvi. Darasani nilikuwa ninasoma na watoto wa watu wote wenye
 mamlaka pale mjini Kigoma. Wote tulikuwa tunafundishwa na Mwalimu huyo 
huyo na tunakaa darasa hilo hilo, tunapata elimu hiyo hiyo. Leo mimi ni 
msomi mwenye shahada ya Uzamili na Mbunge nawakilisha watu wa kwetu. 
Wenzangu wengi pia wanaendesha maisha yao na wengine wapo hapa Marekani 
wakitafuta maisha.
Leo mtoto wa masikini Tanzania hapati elimu anayopata mtoto wa mwenye
 uwezo. Mtoto wa masikini hakutani na mtoto wa mwenye uwezo. Wanasoma 
shule tofauti. Wanafundishwa na walimu tofauti. Hawachezi pamoja. Wote 
wakimaliza kidato cha Sita, mtoto wa mwenye uwezo ana nafasi kubwa zaidi
 ya kupata mkopo kwenda Chuo Kikuu kwa sababu amesoma shule bora zaidi 
hivyo anapata daraja kubwa zaidi la kupewa mkopo na Bodi ya Mikopo.
Wakati nasoma, kikwazo kilikuwa uwezo wako tu kichwani. Hivi sasa 
kikwazo ni kipato pia. Tofauti ya kipato nchini ni kubwa lakini sisi 
wanasiasa hatuioni. Wakati wenzetu wanajiandaa kufaidika na ‘demographic
 dividend’ kwani watoto wao wanapata elimu bora, sisi hata hatujiandai 
na ‘demographic Bomb’ litakaloletwa na kundi kubwa la vijana wasio na 
elimu wala ujuzi.
Shiriki kurejesha Tanzania yenye kutoa fursa kwa kila raia bila 
kujali hali yake ya kipato. Shirika kurejesha Tanzania yenye Usawa 
kwenye fursa na yenye demokrasia. Jiunge na CHADEMA tuendeleze 
mapambano.
Nawashukuru kwa kunisikiliza
Zitto Kabwe, Mb
Naibu Katibu Mkuu CHADEMA


 
