Aliyekuwa msajili wa vyama vya siasa nchini, John Tendwa akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwakwe. |
Dar
es Salaam.
Aliyekuwa msajili wa vyama vya siasa nchini, John Tendwa amesema Rais
Jakaya Kikwete aliteleza kueleza msimamo wake na ambao baadaye ulibainika kuwa
wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati akizindua Bunge Maalumu la Katiba, Machi
21.
Tendwa,
ambaye alistaafu Agosti mwaka jana na nafasi yake kuchukuliwa na Jaji Francis
Mutungi, alitoa kauli hiyo jana katika mahojiano maalumu na Mwananchi ofisini
kwake jijini Dar es Salaam.
Tendwa,
ambaye alikuwa Msajili kwa miaka 13, alisema akiwa kiongozi mkuu, Rais Kikwete
alipaswa kutoa mwongozo wa uendeshaji wa Bunge Maalum la Katiba.
“Sikuwapo
nchini, lakini kwa kadri ninavyoelezwa, kama hiyo ni kauli yake, basi
alijisahau kusemea msimamo wa chama chake, (CCM) na sera yake ya serikali mbili
katika bunge hilo,” alisema.
“Rais
ni mtendaji, alipaswa kutoa guidelines (miongozo) ya jinsi ambavyo Bunge Maalum
la Katiba linatakiwa kufanya. Alichokisema, aliteleza.
“Alijisahau
na kurudi kwenye chama kwa sababu hiyo ndiyo sera ya chama chake, ” alisema
Tendwa.
“Na
siyo yeye tu (Kikwete) kwani nimemsikia hata Dk Shein (Rais wa Zanzibar na
mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi), akisema kuwa msimamo wa CCM ni serikali
mbili,” aliongeza Tendwa.
“Nimemsikia
Makamu wa Pili wa Rais (Balozi Seif Ali Iddi) akisema hivyo na Rais
wangu (Kikwete) katika mikutano mbalimbali ya hadhara, naye amelisema hilo.”
Madai
ya kuibeba CCM
Tendwa
ambaye katika uongozi wake wa miaka 13 alikuwa akituhumiwa mara kwa mara na
vyama vya upinzani kuwa anakibeba chama tawala, alisema: “Nadhani na yeye (Rais
Kikwete) kasema. Nadhani alijisahau kuwa ni kiongozi wa taifa.”
“Rais
ni mtendaji na mimi nasema aliteleza. Turudi katika hoja kwa kujadili rasimu
iliyoko mezani.”
Kauli
hiyo imekuja kipindi ambacho baadhi ya viongozi wakiwamo wa vyama vya siasa
nchini, Dk Wilbroad Slaa (Chadema), Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim
Seif Shariff Hamad na pia aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Jaji Joseph Warioba, pia kumkosoa Rais Kikwete.
Kwa
nyakati tofauti, wameeleza kuwa Kikwete ndiye mtu pekee anayeweza kutuliza
mvutano ulioibuka katika mchakato huo unaoendelea kwenye Bunge la Katiba.
Ulikoanzia
mzozo
Machi
21, wakati akifungua Bunge Maalum la Katiba, Rais Kikwete aliipinga
Rasimu ya Pili ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba, akigusia
mambo saba ya msingi yaliyomo katika rasimu hiyo na kutaka yatazamwe kwa kina,
kubainisha kuwa mengine hayawezi kutekelezeka.
Miongoni
mwa mambo hayo ni muundo wa Muungano kuwa wa serikali tatu uliopendekezwa
katika rasimu hiyo.
Kikwete,
ambaye alisema anatoa maoni yake binafsi, alipinga waziwazi pendekezo la
serikali tatu na kuegemea katika muundo wa serikali mbili unaoungwa mkono na
CCM, huku akifafanua kuwa idadi ya watu waliopendekeza muundo wa serikali tatu
ilikuwa ndogo.
Walilosema
wengine
Julai
7, wakati akizungumza katika kipindi cha Dakika
45 kinachorushwa na televisheni ya ITV, Maalim Seif alimtupia
lawama Rais Kikwete kuwa amechangia kuukoroga mchakato wa katiba kwa kufuata
msimamo wa chama chake, badala ya maoni ya wananchi yaliyomo katika rasimu ya
pili ya katiba.
Maalim
Seif, ambaye alilenga kauli iliyotolewa na kiongozi huyo wa nchi wakati
akifungua Bunge la Katiba, alisema kauli ya Rais Kikwete imeondoa imani ya
wananchi kuhusu kupatikana kwa katiba inayotokana na maoni yao.
Alisema
mchakato huo hivi sasa unamtegemea Rais pekee, huku akisisitiza kuwa hakuna
binadamu aliyekamilika na kumshauri kutafuta uwezekano wa kuweka mambo sawa,
ili kujenga tena imani kwa wadau wote.
Julai
4, Dk Slaa, wakati akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili jijini
Dar es Salaam, alimtaka Rais Kikwete kujitokeza hadharani kutafuta suluhu ya
kupata mwafaka wa mchakato wa Katiba Mpya kwa kuwa hakuna mamlaka nyingine
zaidi inayoweza kuunusuru.
Naye
Jaji Warioba kwa nyakati tofauti amemshauri Rais Kikwete kuchukua hatua
zitakazoondoa matatizo katika Bunge la Katiba ili kuwezesha mchakato huo
kukamilika.
Alisema
ni muhimu kiongozi huyo mkuu wa nchi kuweka kando tofauti za mawazo na mitazamo
ili kupata Katiba Mpya kwa masilahi ya Taifa.
Mwanzoni
mwa wiki, mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mbeya na naibu waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Godfrey Zambi alifichua kuwa msimamo wa serikali mbili unaoonyeshwa
na wabunge wa chama hicho ni maagizo ya Kikwete.