![]() |
| Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Bernard Membe |
JINA
la Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimaitafa, Bernard Membe, limeanza
kuhusishwa na tukio la kutekwa na kuteswa kikatili na watu wasiojulikana
lililomkuta Mhariri Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda.
Madai ya kulihusisha jina la Waziri Membe na tukio hilo, yalianza kuzagaa miongoni mwa watu waliofika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kumjulia hali Kibanda, muda mfupi baada ya kutendewa unyama huo.
Madai ya kulihusisha jina la Waziri Membe na tukio hilo, yalianza kuzagaa miongoni mwa watu waliofika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kumjulia hali Kibanda, muda mfupi baada ya kutendewa unyama huo.
Makundi ya watu waliokuwa hospitalini hapo walilioanisha tukio hilo na kauli iliyopata kutolewa na Waziri Membe katika mahojiano ya kipindi cha Dakika 45, kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha ITV, alipoeleza kuwa anao maadui wakubwa 11, wakiwamo waandishi wa habari wawili ambao aliahidi kuwashughulikia.
Ingawa Membe alikutana na shinikizo la watu mbalimbali lililomtaka awataje maadui zake hao 11, wakiwamo waandishi wa habari wawili ambao alikuwa na mpango wa kuwashughulikia, hadi sasa hajapata kufanya hivyo, jambo ambalo linadaiwa na wadadisi wa mambo kuwa ni uamuzi wake wa kuchukua mkondo wa kutekeleza kile alichokisema kwa vitendo.
Tamko lake hilo katika kipindi hicho kilichorushwa hewani Julai 16, 2012, ambalo limeibua hali ya sintofahamu, sasa linaonekana kuchukuliwa kwa uzito zaidi na wanahabari na wamiliki wa vyombo vya habari, baada ya kuwa moja ya mambo mazito yaliyozungumzwa jana katika mkutano wa wamiliki wa vyombo vya habari.
Kwa takribani siku mbili, Membe amekuwa akitafutwa na gazeti hili kwa ajili ya kuzungumzia madai hayo, lakini hata hivyo jitihada za kuzungumza naye hazikufanikiwa, baada ya simu yake kuita wakati wote bila majibu.
Hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno kupitia simu yake ya kiganjani, hakujibu, licha ya kuonyesha umefika.
Jana katika mkutano huo wa wamiliki wa vyombo vya habari ulioketi Hoteli ya Serena, Dar es Salaam, kujadili kuzorota kwa mazingira ya usalama ya waandishi na wanaharakati wengine, suala hilo la Membe pia lilijadiliwa.
Wakijibu maswali ya waandishi waliotaka kujua namna viongozi wa serikali na watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama wanavyohusishwa na matukio ya aina hii, wamiliki hao walieleza kuwa wapo baadhi ya watendaji waandamizi wa serikali waliokwishalitangazia taifa kuwa wanao maadui 11 hapa nchini, wawili kati ya hao ni waandishi wa habari walioahidi kuwashughulikia.
Akizungumza kwa niaba ya wamiliki wenzake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Hussein Bashe, alisema ni jambo la kushangaza kuona kauli kama hiyo iliyotolewa na kiongozi mwandamizi wa serikali haijafanyiwa kazi na vyombo vya ulinzi na usalama.
“Mfano, mwaka jana, alinukuliwa mwanasiasa na kiongozi wa Serikali kupitia kipindi cha Dakika 45, akisema kuwa ana maadui 11 ambao kati yao, wawili ni waandishi wa habari, hivi kauli hii ambayo ilikuwa ikiruka katika kituo cha luninga haikusikika au adui mwenyewe kati ya waliotajwa ndiyo Kibanda?
“Kama ni hivyo, mbona haitwi ili ahojiwe kuhusu hali hii na vyombo hivi vya ulinzi na usalama vya nchi yetu, tunahitaji kuona kuwa Serikali yetu inafanya kazi na hata kulinda maisha ya watu wake,” alidai Bashe.
Sehemu ya kauli ya Waziri Membe katika kipindi hicho kilichokuwa kikiongozwa na mtangazaji Selemani Semunyu, ambayo sasa inaonekana kuwa hatari kwake, alisema: “Lazima watu hao wajue kwamba ukikaa juu ya nyoka, ipo siku atakugonga tu. Hili nawaachia Watanzania waamue, lakini kuna watu 11, wakiwamo waandishi wawili wa habari, nitawatwanga kweupe.”







